Tuesday, March 1, 2011

Lowassa awataka viongozi waseme ukweli

WAZIRI Mkuu wa zamani Edward Lowassa amewataka viongozi wa Serikali na siasa wajitokeze hadharani na kusema ukweli kuhusu hali mbaya ya uchumi nchini.

Lowassa amesema, hali hiyo kwa sasa lazima iendane na kupanda kwa mishahara kwa wafanyakazi wa umma kote nchini.

Lowassa alizungumzia pia mgogoro wa dini ulioibuka katika mji wa Mto wa Mbu wilayani Monduli mkoani hapa na kuwataka wananchi kutulia kwani suala hilo linashughulikiwa na waendelee na kazi zao bila bughudha.

Mbunge huyo wa Monduli alisema hayo jana kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), muda mfupi alipotua hapo akienda jimboni mwake kuhudhuria mazishi ya Diwani wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Magdalena Shoo aliyefariki ghafla juzi nyumbani kwake na anatarajia kuzikwa kesho mjini Moshi.

Aliwaambia waandishi wa habari kuwa hali iliyopo sasa ya uchumi kuyumba nchini ni hali iliyopo kote duniani, hivyo viongozi wa Serikali na siasa wanapaswa kujitoa hadharani kwa kusema ukweli bila ya woga.

Alisema bei ya nafaka katika soko la dunia imepanda kwa asilimia kubwa na pia mafuta yatapanda vivyo hivyo, “hivyo basi viongozi hatuna budi kupandisha mishahara ya wafanyakazi kutokana na hali iliyopo kuliko kuwalipa mishahara ya zamani ambayo haikidhi mahitaji kwa asilimia kubwa.”

Alisema, itakuwa sio jambo la busara kuona hali ya maisha inazidi kuwa mbaya na ngumu, lakini mishahara ibaki pale pale akiongeza kuwa “hapo hatutawatendea haki wafanyakazi na malalamiko yataendelea kote nchini wakati sababu za msingi zipo.”

Alisema kuacha kupandisha mishahara kwa sasa ni suala lisilowezekana na kiongozi yeyote awe wa Serikali na wa siasa atayepingana na hilo, anapaswa kuwa na takwimu za ukweli kwani hali hiyo iko kote duniani.

Alishauri kuundwa kwa tume huru juu ya kutafuta namna gani mishahara itapandishwa na tume hiyo inapaswa kuundwa kwa kushirikisha wataalamu waliobobea wa uchumi, viongozi wa vyama vya wafanyakazi na Serikali kwa ujumla.

Alisema tume hiyo pia itaangalia vyanzo vyote vya mapato vya Serikali ikiwa ni njia mojawapo ya kutaka kupanga mshahara wa dhati wa mfanyakazi kwa hali iliyopo kwa sasa ya uchumi.

“Tujitoe na kusema ukweli juu ya hali mbaya ya kupanda kwa maisha iliyopo sasa na dawa ya hiyo kwa sasa ni kupandishwa kwa mishahara tu ili twende na hali vinginevyo tunajidanganya na hilo linaweza kuwa na athari hapo baadaye,” alisema Lowassa ambaye katika Mkutano wa Pili wa Bunge la 10 uliomalizika hivi karibuni, alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama.

Akizungumzia ugomvi wa kidini katika mji wa Mto wa Mbu, alisema amesikitishwa na hali iliyojitokeza na kuwataka wananchi kutulia na kutafakari kwa kina ni shetani gani amewafikia na kuchukua hatua hiyo.

Aliahidi kwenda kukutana na wazee wa mji huo na kukaa nao ili kutatua suala hilo ili lisijirudie kwani waumini kupigana na kufikia hatua ya kutoana damu ni hatari kwa sababu Watanzania hawana tabia hiyo.

Alisema mji wa Mto wa Mbu wenye makabila zaidi ya 120, ni mji wa kitalii hivyo amani inapaswa kuwepo kwa asilimia 100, hivyo aliwataka wananchi hao kutulia na kuendelea kufanya kazi zao.

1 comment:

Ndugu Nkwazi N Mhango said...

Lowassa angeanza kusema ukweli yeye kuhusiana na alivyopata mali aliyojilimbikizia. Pia angekwenda hatua moja mbele kwa kumweleza rafiki na mshirika wake Jakaya Kikwete na genge lake kufanya hivyo. Je huu hauwezi kuchukuliwa kama unafiki? Au ndizo hizo kampeni za 2015 zinaanza kinamna?