SAKATA la malipo ya kampuni ya kufua umeme ya Dowans Tanzania Limited, limechukua sura tofauti baada ya Bunge kutupilia mbali hoja binafsi ya Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila (NCCR) ya kutaka lijadaliwe bungeni.
Wakati Bunge likitoa uamuzi huo Dodoma, Mbunge wa Bumbuli, January Makamba (CCM) amepeleka hoja nyingine, kuitaka Serikali itoe tamko bungeni kuhusu lini hali ya umeme itatengemaa nchini, huku akitaka hoja hiyo itolewe ufafanuzi katika tamko hilo.
Katika hoja hiyo ya January, alisema “jambo hili likibaki bila maelezo, inaweza kujengeka sura kwamba Serikali ilikosa umakini na maadili hayakuzingatiwa.”
Jijini Dar es Salaam nako wanachama wa CUF, wakiongozwa na Mwenyekiti wao, Profesa Ibrahim Lipumba, waliandamana kupinga malipo ya kampuni hiyo, huku wakitoa mwito wa suala hilo kupelekwa kwenye Baraza la Mawaziri ili Rais apate ushauri wa chombo mahususi kwa kazi hiyo.
Lakini katika barua ya January, ya Februari 3 mwaka huu kwenda kwa Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja yenye kichwa cha habari ‘Taarifa ya Serikali Bungeni Kuhusu Umeme Nchini’, anaitaka Serikali kutoa taarifa ikibainisha ni lini itapeleka mahakamani pingamizi dhidi ya utekelezaji wa hukumu ya kuilipa Dowans.
Hukumu hiyo iliyotolewa mwishoni mwa mwaka jana na Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi (ICC) inalitaka Shirika la Umeme (Tanesco) kuilipa kampuni hiyo Sh bilioni 94.
“Mheshimiwa Waziri, mnamo tarehe 6 Januari 2011 ulizungumza na waandishi wa habari na kueleza kwamba Serikali inajipanga kuilipa Dowans tuzo iliyoamuliwa na ICC, lakini kwa kuwa mzigo huo ni mzito kwa umma, kumekuwa na fikra, likiwamo pendekezo la Kamati ya Wabunge wote wa CCM kwamba ni muhimu kutumia mianya ya sheria iliyopo kupinga rasmi kutekelezwa kwa hukumu hiyo,” alisema.
Aliitaka pia Serikali iueleze umma kupitia Bunge kuwa ni wanasheria gani waliotumiwa na Tanesco kwenye kila hatua katika shauri la Dowans, kuanzia kwenye ushauri kabla ya kuvunjwa mkataba wa kufua umeme, hadi ushauri baada ya kesi kuamuliwa na kiasi cha fedha walizolipwa kwa kila hatua na utaratibu uliotumika kuwalipa.
“Ili kuwaondolea wasiwasi Watanzania ambao wengi wao wanaamini Tanesco ilishindwa kesi ya Dowans kutokana na upungufu wa weledi kwa wanasheria walioiwakilisha kwenye kesi, nashauri taarifa ya Serikali ieleze utaratibu unaotumika kuwapata wanasheria wanaoiwakilisha Serikali na Tanesco kwenye mashauri yake,” alieleza January.
Miongoni mwa mashauri hayo ni pamoja na lile lililofunguliwa na Benki ya Standard Chartered (Hong Kong) dhidi ya serikali na Tanesco kwenye Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Kesi za Uwekezaji (ICSID).
Kesi dhidi ya Tanesco ni ya Oktoba mosi mwaka jana na dhidi ya Serikali ni ya Juni 11 mwaka huo huo. January anataka wananchi waelezwe ni nini hasa kinachodaiwa katika kesi hizo.
Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashillilah akizungumza juu ya ratiba nzima ya vikao vya Bunge hilo alisema hoja ya kampuni hiyo pamoja na kupelekwa kwa maelezo ya Kafulila, haiwezi kujadiliwa kutokana na Bunge hilo kushindwa kuingilia Mahakama.
“Kwa kawaida na kwa mujibu wa kanuni, Bunge haliwezi kujadili hoja ambayo tayari iko mahakamani na hata Mahakama yenyewe huwa haina nguvu kujadili hoja inayojadiliwa bungeni, kifupi hoja hii kwa bahati mbaya haitajadiliwa, kwa sababu tayari iko mahakamani,” alisema.
Kwa upande wa hoja ya kuundwa kwa Katiba mpya, Kashillilah alisema hoja hiyo pia haitawasilishwa bungeni hapo kutokana na kukiuka Katiba hasa baada ya mmoja wa wabunge waliowasilisha makusudio yao kuhusu hoja hiyo, kutaka Katiba ya sasa ifutwe.
Aliwataja baadhi ya wabunge ambao waliwasilisha kusudio lao la kutaka Katiba mpya kuwa ni Mbunge wa Wawi, Hamad Rashid Mohammed (CUF) na Mbunge wa Viti Maalumu, Angela Kairuki (CCM).
Alisema kwa mujibu wa kanuni za Bunge, hoja yeyote ili iweze kupitishwa na kujadiliwa na Bunge, lazima ikidhi vigezo ikiwamo kutokiuka Katiba.
Pamoja na hayo, tayari Serikali imeanza mchakato wa kupeleka hoja bungeni kwa ajili ya kubadili Katiba hivyo hakuna haja ya kuendeleza mjadala huo.
Kuhusu ratiba nzima ya mkutano wa pili wa Bunge hilo la 10 alisema Spika wa Bunge atawasilisha hoja ya kufanya mabadiliko ya kanuni za Bunge baada ya Rais kubadilisha Baraza la Mawaziri.
“Pia kuna baadhi ya wizara ambazo zimebadilishwa na kusababisha baadhi ya idara nazo kuhamishwa hivyo kutokana na mabadiliko hayo inabidi Kanuni zibadilishwe na kusaidia uundwaji wa Kamati za Bunge ambazo nazo zinatakiwa kuendana na mfumo wa wizara zilizopo,” alisema.
Aidha, alisema kwa mujibu wa ratiba hiyo Spika wa Bunge atatangaza Kamati mpya za Bunge hilo, kujadili hotuba ya Rais Jakaya Kikwete aliyoitoa wakati wa ufunguzi wa Bunge ambapo alitoa vipaumbele 13 vya kufanyiwa kazi na kusomwa kwa maazimio mawili.
“Hakuna muswada utakaojadiliwa, ila mitatu itasomwa kwa mara ya kwanza na kurejeshwa katika mkutano wa tatu wa Bunge hili la 10 utakaofanyika Aprili,” alisema.
Alisema pia kutafanyika uchaguzi wa wenyeviti watatu watakaomsaidia Spika na Naibu Spika na wajumbe wa Tume ya Utumishi wa Bunge.
No comments:
Post a Comment