MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi mkoani Iringa imeifuta kesi ya kutoa rushwa iliyokuwa ikimkabili aliyekuwa Mbunge wa Mufindi Kaskazini kwa miaka 35, Joseph Mungai.
Hakimu Mary Senapee wa Mahakama hiyo, alisema jana kwamba, pingamizi la kisheria lililowasilishwa Oktoba mwaka jana na mawakili wa Mungai, lilionesha kwamba mawakili wa upande wa mashitaka walifanya makosa wakati wa kufungua kesi hiyo.
Kwa mujibu wa Hakimu Senape, mawakili hao Alex Mgongolwa na Basil Mkwata, walionesha kuwa upande wa mashitaka uliowakilishwa na mawakili wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), ulikosea kumfungulia Mungai na wenzake mashitaka 15 kwa kutumia hati moja ya mashitaka.
“Naitupilia mbali kesi hii kwa sababu upande wa mashitaka umetumia hati moja ya mashitaka, kumfungulia Mungai na wenzake wawili mashitaka tofauti yanayohusisha sheria mbili tofauti,” alisema Hakimu Senape wakati akitoa uamuzi huo.
Akiwa ameunganishwa na makada wengine wawili wa CCM, Fidel Cholela na Moses Masasi, Mungai alishitakiwa na Takukuru kwa makosa 15 ya kutoa rushwa kinyume na Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ya mwaka 2007.
Pia alishitakiwa kukiuka Sheria ya Gharama za Uchaguzi ya mwaka 2010 kwa wapiga kura wa jimbo hilo.
Katika hati ya mashitaka hayo, ilidaiwa na Takukuru kwamba Julai 08, mwaka jana, katika Kata ya Ihalimba, Wilaya ya Mufindi, Mungai akiwa mmoja wa makada wa CCM waliokuwa wanawania kupitishwa katika kura za maoni kugombea ubunge wa jimbo hilo alitoa rushwa.
Kwa mujibu wa madai hayo, Mungai pamoja na watuhumiwa wenzake, walitoa rushwa ya kati ya Sh 5,000 na Sh 20,000 kwa wajumbe wa CCM tawi la Vikula kama kishawishi cha kumpigia kura wakati wa upigaji wa kura za maoni.
Hata hivyo, Hakimu Senape alisema Takukuru wanaweza kurekebisha hati hiyo ya mashitaka au kufungua hati mpya ya mashitaka kama wataona kuna haja ya kuendelea na kesi hiyo.
Baada ya hukumu hiyo, Mgongolwa alisema mbali na kufarijika kwa uamuzi huo, Takukuru walifanya kosa kubwa la kisheria wakati wakifungua mashitaka hayo.
“Katika mashitaka hayo, Takukuru walitumia Sheria ya Gharama za Uchaguzi ya mwaka 2010 na Sheria ya Kupambana na Rushwa ya mwaka 2007, jambo lisilokubalika.
Alifafanua kuwa matumizi ya sheria hizo kwa pamoja ni kosa kwa kuwa zina makosa tofauti ndio maana hakimu amekubaliana na pingamizi lao kwa kutupilia mbali kesi hiyo.
Wakili wa Takukuru, Imani Nitumeni alisema Takukuru kama ilivyo kwa upande wa washitakiwa unakubaliana na uamuzi halali wa Mahakama.
“Hata hivyo ofisi yetu, itaupitia upya uamuzi wa Mahakama na kama tutaona inafaa, tutairekebisha hati hiyo ya mashitaka au kwa kuzingatia sheria hizo, kufungua upya mashitaka dhidi ya Mungai na wenzake,” alisema.
Akionekana kufurahishwa na uamuzi huo wa Mahakama, Mungai alisema ni uamuzi alioutarajia kwa sababu sheria hizo anazifahamu.
Alisema pia alipokuwa akikamatwa na Takukuru alitoa tahadhari kwa maofisa hao kwamba wanatakiwa kufanya kazi yao kwa uangalifu kwa sababu hakufanya kosa kwa mujibu wa sheria hizo.
“Kuna uwezekano uamuzi wa kunikamata ulikuwa na shinikizo la kisiasa kutoka kwa watu waliokuwa wanataka jimbo langu na nisiendelee kuwa Mbunge,” alidai.
Alisema alishangazwa sana na wepesi uliotumiwa na maofisa hao wa Takukuru wa kumkamata bila woga na kumfungulia mashitaka kwa makosa ambayo hakuyafanya hasa kwa kuzingatia kwamba yeye amekuwa mtunga sheria kwa zaidi ya miaka 35.
“Hata hivyo ninafurahi kwamba nimepata haki yangu, kitakachofuata, nawaachia wanasheria wangu, kwa sababu suala hili limenilitea matatizo makubwa mimi na familia yangu, kwa hiyo tukiiona hukumu yote tutajua nini cha kufanya,” alisema.
Kwa mara ya kwanza Mungai alipandishwa kizimbani akihusishwa na madai hayo Agosti 12,mwaka jana.
Uamuzi huo umeelezwa na baadhi ya wana CCM waliohudhuria mahakamani hapo kwamba unamfagilia njia ya kugombea uenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Iringa baada ya mkoa huo kugawanywa.
Mkoa huo umegawanywa na kuwa na mikoa ya Iringa na Njombe ambayo mpaka sasa inaongozwa na Mwenyekiti mmoja, Deo Sanga (Mbunge wa jimbo la Njombe Kaskazini) anayepewa nafasi kubwa ya kuwa Mwenyekiti wa mkoa mpya wa Njombe.
No comments:
Post a Comment