Monday, February 14, 2011

Makinda azuia posho mara mbili kwa wabunge

SPIKA wa Bunge, Anne Makinda amegeuka 'mbogo' na kueleza msimamo wake kwamba hatawavumilia wabunge ambao ni wajumbe wa Kamati za Kudumu za Bunge, watakaopokea posho mara mbili wanapotembelea taasisi au mashirika yaliyo chini ya kamati hizo.

Uchunguzi wa HabariLeo umebaini kwamba Spika Makinda alitoa onyo hilo alipofanya kikao kwa mara ya kwanza na Kamati ya Uongozi ya Bunge inayoundwa na wenyeviti wa Kamati 18 za Kudumu za Bunge mwishoni mwa wiki mjini hapa.

Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya kikao hicho, kilieleza kuwa Spika amesema kwake litakuwa ni kosa kubwa kwa wabunge kupokea posho mara mbili wanapofanya ziara kukagua uendeshaji wa mashirika mbalimbali na idara za Serikali.

"Ametuambia wazi kwamba kitendo cha kupokea posho mara mbili kinaathiri kwa kiwango kikubwa usimamizi na ukaguzi katika mashirika haya maana wabunge wakipokea posho za Bunge na zile zinazotolewa na mashirika yanayokaguliwa hushindwa kutimiza wajibu wao
ipasavyo," kilisema chanzo hicho.

Kwa mujibu wa habari hizo, Spika amesema atatumia Kanuni za Bunge zinazozuia wabunge kupokea takrima yoyote wanapotembea mashirika wakati tayari ziara zao zinakuwa zimelipiwa na Bunge.

Mmoja wa wajumbe wa Kamati ya Uongozi ya Bunge ambayo Mwenyekiti wake ni Spika na Makamu wake ni Naibu Spika Job Ndugai, January Makamba alikiri Spika kueleza msimamo wake huo juu ya wabunge kupokea posho mara mbili.

January ambaye ni Mbunge wa Bumbuli (CCM) ni Mjumbe wa kamati hiyo kutokana na wadhifa wake wa Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini.

Alisema suala hilo ni mojawapo ya masuala yaliyopewa msisitizo mkubwa na Spika Makinda alipokutana na wajumbe wa Kamati ya Uongozi mwishoni mwa wiki.

"Unashangaa kuona wajumbe wanafanya ziara katika shirika fulani halafu wanapewa bahasha kwa maelezo kwamba ni posho ya chakula, lakini ukiangalia ndani unakuta ni shilingi milioni moja…Sasa sijui ni chakula gani kinachouzwa kwa bei hiyo. Spika amelikemea vikali suala hili," alisema January.

Wajumbe walioshiriki kikao hicho cha Kamati ya Uongozi mbali ya Spika, Naibu Spika na January ni Edward Lowassa (Mwenyekiti Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama); Dk. Abdalah Kigoda (Mwenyekiti Kamati ya Fedha na Uchumi); John Cheyo (Mwenyekiti Kamati ya Hesabu za Serikali); Augustino Mrema (Mwenyekiti Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa); George Simbachawene (Mwenyekiti Kamati ya Sheria Ndogo) na Margaret Sitta (Mwenyekiti wa Kamati ya Huduma za Jamii).

Wengine ni Kabwe Zitto (Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Mashirika ya Umma); Jenista Mhagama (Mwenyekiti Kamati ya Maendeleo ya Jamii); James Lembeli (Mwenyekiti Kamati ya Ardhi, Maliasili na Mazingira); Profesa David Mwakyusa (Mwenyekiti wa Kamati ya Kilimo, Mifugo na Maji); Mahmoud Mgimwa (Kamati ya Viwanda na Biashara); Peter Serukamba (Mwenyekiti wa Kamati ya Miundombinu); Pindi Chana (Mwenyekiti wa Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala); Hassan Ngwilizi (Mwenyekiti wa Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge) na Lediana Mng'ong'o (Mwenyekiti wa Kamati ya Masuala ya Ukimwi).

Sakata la wabunge kulipwa posho mara mbili, liliibuka wakati wa Bunge la Tisa chini ya Spika Samuel Sitta, ambapo wabunge walilalamikiwa kupokea posho mara mbili, hatua ambayo ilisemwa na Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Dk. Edward Hoseah, kwamba ni sawa na kupokea rushwa.

Kauli hiyo ya Dk. Hoseah iliibua mgongano mkubwa baina yake na wabunge kabla ya Spika Sitta kulitolea maelezo kwamba kwa mujibu wa Kanuni za Bunge ni marufuku kwa wabunge kupokea posho wanapofanya ziara katika mashirika hayo huku tayari ziara hizo zikiwa
zimelipiwa posho na Bunge lenyewe.

No comments: