Wednesday, February 23, 2011

Mabaki ya mabomu makubwa 2,204 yaokotwa Dar


Spika wa Bunge la Tanzania, Anne Makinda akiwa na huzuni wakati Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadick anamsomea taarifa kuhusu milipuko ya mabomu katika kambi ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Gongo La Mboto. Makinda ametembelea kambi ya waathirika, Mzambarauni jijini humo. (Picha na Fadhili Akida).


JESHI la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), limebaini mabomu matatu yaliyotua ndani ya choo cha shimo na kwenye tangi la maji, na kwamba hayajulikani kama tayari yamelipuka au la.

Pia Jeshi hilo limesema hadi sasa limekusanya mabaki ya mabomu makubwa 2,204, risasi 303, fyuzi za mabomu 668 na bunduki ndogo nyingi zikiwa zimeteketea na hazifai kwa matumizi.

Akitoa taarifa kwa ujumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama na baadaye kwa Spika wa Bunge Anne Makinda, Mkuu wa Kikosi cha 511 cha Jeshi Gongo la Mboto, Kanali Aloyce Mwanjile, alisema hadi sasa wanashughulikia mabomu hayo na kuona namna ya kuyatoa.

“Tumejiwekea vipaumbele katika kukusanya haya mabomu na kipaumbele cha kwanza ni kuhakikisha yote yaliyoangukia kwenye makazi ya watu tunayaondoa, ila kuna changamoto tunakabiliana nazo ikiwamo hili la mabomu matatu yaliyomo ndani ya shimo la choo na kwenye simtank,” alisema Kanali Mwanjile.

Alisema pia kipaumbele kingine ni kuyafikia mabomu yaliyoruka umbali mrefu ambao wanakadiria kuwa kilometa 14 na kusafisha maghala yote ambayo yameharibiwa na mabomu hayo.

Aliyataja maeneo ambayo mabomu hayo yaliyolipuka Februari 16, yameharibiwa kuwa ni Gongo la Mboto, Pugu, Mbezi, Mnadani na Kinyamwezi.

Naye Makinda alisema Bunge limeshtushwa na taarifa hiyo ya milipuko ya mabomu na ndiyo maana liliahirisha kikao chake kimoja, ili kupisha wabunge waweze kutoa msaada wa karibu kwa ndugu na jamaa.

“Ndiyo maana nilipinga ule mwongozo wa mheshimiwa Mbunge wa kutaka Bunge lijadili suala hili, kwa kuwa msaada wetu si kujadili, bali kusaidia kwa hali na mali kwa vitendo na si maneno,” alisema Makinda.

Aidha, alitoa Sh milioni 37.8 kama msaada kutoka kwa wabunge, mawaziri na wafanyakazi wa chombo hicho cha kutunga sheria, ikiwa ni sehemu ya posho yao ya siku moja.

“Siku ya tukio tulikubaliana kila mmoja wetu achangie posho yake ya siku moja kuwasaidia wenzetu,” alifafanua Mbunge huyo wa Njombe Kusini.

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), William Lukuvi, alitoa hadhari kwa timu ya tathmini ya mali zilizoharibiwa na mabomu hayo, kuepukana na udanganyifu unaoweza kuigharimu Serikali fedha nyingi.

“Nina uzoefu na fidia ya mabomu ya Mbagala, tulilazimika kuchelewesha ulipaji fidia zile kutokana na udanganyifu uliofanywa na baadhi ya wananchi kwa kushirikiana na wataalamu wa tathmini,” alisema Lukuvi.

Alisema katika tathmini ya kwanza, ilionesha kuwa Serikali ilitakiwa iwalipe fidia wakazi wa Mbagala ya Sh bilioni 50 na fedha hiyo ilitoka, lakini kwa bahati nzuri kupitia waandishi wa habari, ilibainika kuwa kulikuwa na udanganyifu na katika tathmini ya pili, fedha halisi zilizotakiwa kulipwa zilikuwa ni Sh bilioni nane tu.

Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Sadick, alisema hadi jana watu waliokufa kutokana na tukio hilo ni 24, na maiti wengine wawili wakiwa na utata unaotokana na wasiwasi kama kweli walitokana na mabomu hayo.

Pia alisema majeruhi katika Hospitali ya Muhimbili wamepungua hadi 34, Amana 17 huku Temeke wakiruhusiwa wote.

“Tatizo lililopo sasa ni watoto wanaotafuta wazazi wao kwani wanazidi kuongezeka, juzi walibaki wanane, lakini leo asubuhi (jana) walifikia 18,” alisema.

Hata hivyo, alibaini kuwa si wote waliopo kwenye kambi hizo za watoto wanatokana na kupoteana na wazazi wao kutokana na milipuko hiyo, bali pia wapo watoto wa mitaani wanaotumia nafasi hiyo kujipatia riziki na wengine wawili wamebainika kuwa wanatafuta kazi za ndani wakitokea Iringa na Dodoma.

No comments: