Na Jenarali Ulimwengu
Februari 9, 2011
MJADALA kuhusu uandishi wa Katiba mpya ya Tanzania umeanza, na nina imani utaendelea kwa muda mrefu kidogo, na urefu huo wa muda utasababishwa na mambo kadhaa.
Jambo la kwanza linaloweza kusababisha muda wa mjadala huu kuwa mrefu ni kwamba miongoni mwetu kuna watu wasioona umuhimu wake, watu wanaodhani kwamba madai ya Katiba mpya ni wale wenye kile kinachoitwa “uchu wa madaraka.”
Mara nyingi yanapotumika maneno kama haya walengwa wake ni wale walio nje ya madaraka ambao wanadhaniwa kwamba wana “uchu wa madaraka” kwa sababu wanataka kuwang’oa walio madarakani ili waingie wao.
Inawezekana, kweli, kwamba wale walio nje ya madraka wakawa na “uchu wa madaraka”, lakini hiyo haina maana kwamba wale waliomo madarakani hawana huo “uchu wa madaraka.”
Kimantiki tungemwangalia yule aliye madarakani na anayeng’ang’ania kubakia humo kwamba ndiye mwenye uchu wa madaraka (kwa kuendelea kung’ang’nia humo) na yule aliye nje kuwa pia ana uchu wa madaraka (kwa kukazania kumng’oa yule aliye ndani).
Wanasiasa ni watu wanaojulikana kuwa na huo uchu, na kwa kundi moja kuwasema wenzao eti wana uchu wa madaraka na kutaka kusema kwamba hao wanaowasema wenzao hawana uchu wa madaraka. Huo ni uongo na unafiki.
Ni katika jitihada za kusuluhisha na kuratibu aina mbalimbali za uchu wa madarka wa wanasiasa, ndipo Katiba ya nchi inapokuwa na umuhimu, kama kielelezo cha utashi uliobainika na kujengeka miongoni mwa matabaka ya kijamii kuhusu jinsi ya kuendesha utawala, uongozi, uchumi, utamaduni na mambo mengine mengi yanayoihusu jamii husika.
Utashi ninaoujadili hapa una madaraja mengi, na kadri jamii zinavyokomaa na kupevuka, madaraja hayo hunyumbuka na kuchukua sura mpya ambazo awali hazikutambulika hata kama zilikuwa na watetezi wake.
Kwa mfano, Mapinduzi ya Marekani (1776) yalikuwa na dibaji ya Tamko la Uhuru, lililounguruma na kusema, “Tunatambua haya mambo kama yanayojidhihirisha yenyewe, kwamba wanaume wote wameumbwa sawa, na kwamba wamejaliwa na Muumba wao haki sizizoondosheka, na kwamba haki hizi ni pamoja na Maisha, Uhuru na Usasi wa Furaha”
Katika tamko hilo, wanawake hawatambuliki, na nchini Marekani wanawake hawakupata haki ya kupiga kura hadi mwanzoni mwa karne ya 20. Wala tamko hilo halikuwajumlisha wanaume watumwa, na wajukuu zao walikuja kupiga kura kwa mara ya kwanza katika nusu ya pili ya karne hiyo ya 20.
Hiki ni kielelezo kwamba aina na umbo la utashi wa kisiasa hubeba hali halisi ya wale wanaouunda, maslahi yao, uzoefu wao, matumaini yao na hofu zao. Isingekuwa rahisi kwa akina George Washington na Thomas Jefferson, wakombozi wa Marekani dhidi ya ukoloni wa Uingereza, kuwajumuisha wanawake na watumwa katika madai yao. Wakati ule, Uhuru ulikuwa ni kwa ajili ya mabwanyenye wanaume, wenye mali.
Ilichukua muda mrefu kuibadilisha hali hiyo, hadi leo tunashuhudia Mwafrika akiwa rais na amirijeshi mkuu wa Marekani, ukweli ambao hakuna aliyeuota hata miaka 20 tu iliyopita.
Ndiyo kusema, basi, kwamba hakuna hali katika maisha ya binadamu itakayobaki imetulia tuli kwa muda mrefu. Mazingira ya maisha yetu hubadilika siku zote, na juu wa wajuzi wa mambo pamoja na viongozi wa jamii kulitambua hilo ili waweze kuwaongoza wenzao katika kufanya mabadiliko mwafaka na kwa wakati unaofaa. Kutolitambua hilo kunaweza kusabababisha hasara kubwa katika mfumo wa kiutawala na wa kijamii.
No comments:
Post a Comment