RAIS Jakaya Kikwete amesema hataingilia kamwe uhuru wa Mahakama na badala yake ameitaka taasisi hiyo kuongeza kasi ya kutoa elimu kwa wananchi, kuhusu umuhimu na mipaka ya kiutendaji ya muhimili huo wa Dola.
Amesema kazi hiyo ya elimu itampunguzia adha anayoipata ya kuombwa aingilie kati uhuru huo kwa baadhi ya hukumu za kesi zinazotolewa.
Ingawa haukuwa utaratibu wake kuzungumza katika sherehe za Siku ya Sheria nchini, Rais Kikwete jana alilazimika kufanya hivyo katika viwanja vya Mahakama Kuu ya Tanzania, Dar es Salaam alipoombwa na Jaji Mkuu, Mohamed Chande Othman, kusalimia hadhara katika sherehe hizo.
Akitoa salamu hizo, Rais ambaye alikuwa mgeni rasmi alisema: “Nashukuru Jaji Mkuu kunipa heshima ya kusalimia, nakubaliana nawe kuwa ni kweli wananchi wengi hawajui umuhimu wa Mahakama na elimu ni muhimu sana katika hili, natambua juhudi kubwa mlizofanya mpaka sasa, lakini ziongezwe, mahakama zipo kwa ajili ya kutumikia wananchi.
“Binafsi elimu ikifika sawa sawa itanipunguzia tabu hasa kwa wanaonitumia ujumbe wa kutaka niingilie kesi zao zilizotolewa hukumu, huwa nawajibu lililoamuliwa na mahakama sina uwezo nalo, lakini hawaamini, wananishangaa, mtu mmoja akaniambia ‘acha tumchague mwenzako, ndiyo maana tunataka Katiba mpya (kicheko), ndiyo maana nasisitiza elimu ni msingi wa ufafanuzi wa haya,” alisema Kikwete.
Alisema mahakama zipo kwa ajili ya kutumikia wananchi na kusisitiza kuwa Serikali itafanya kwa sehemu yake, kwa kuwa ni jukumu lake, lakini mahakama kwa kushirikiana na wadau kama vyombo vya habari, wana nafasi nzuri zaidi kutoa elimu hiyo.
Kauli ya Rais imekuja huku baadhi ya watu na taasisi zikimshinikiza atoe kauli ya Serikali kuhusu malipo ya Sh bilioni 94 ambazo zinatakiwa kulipwa na Tanesco kwa kampuni ya kufua umeme ya Dowans , ilyoshinda kesi ya kuvunjiwa mkataba.
Rais Kikwete pia aliuagiza uongozi wa Mahakama kuhakikisha utendaji wa uadilifu na haki, kwa kuwa bado kuna malalamiko kwa wananchi, kuwa baadhi ya mahakimu na majaji wanatumia uwezo wa fedha wa mtu, kama kigezo cha kupewa haki na kutaka kasi ya kuwashughulikia wanaoharibu taswira ya chombo hicho, iongezeke.
“Si mara ya kwanza kusema hili, nafahamu pia kuwa si wote wako hivyo, lakini kuna baadhi uadilifu wao una shaka, natambua pia kuwa wapo wawajibikaji wazuri, na pia nafahamu wapo waliogundulika na kuwajibishwa kwa kukosa uadilifu, juhudi ziongezwe ili kujenga taswira nzuri mbele ya wananchi na dunia,” alisema Rais.
Akizungumzia changamoto, Kikwete aligusia pia Mfuko wa Mahakama, na kusema utekelezaji wake uko katika hatua za mwisho na Muswada wa Sheria utapelekwa katika Bunge la Aprili mwaka huu, ili ufanyiwe kazi na matarajio ni kuanza katika mwaka wa fedha ujao (2011/12).
“Ni matumaini yangu kuwa Mfuko huo utakuwa ni maisha mapya kwa mahakama na uendeshaji mzima wa shughuli zake na mambo mengine yatashughulikiwa na Mfuko, mengine kama maslahi ya majaji tutayashughulikia katika mwaka huo huo wa fedha,” alisema Rais Kikwete.
Jaji Mkuu alimwomba Rais mara baada ya kuanzishwa Mfuko wa Mahakama, kianzio kiwe ni asilimia mbili ya bajeti ya Serikali. Hata hivyo, Rais katika salamu zake hakuzungumzia ombi hilo.
Pamoja na kueleza hayo, Rais aliitaka Mahakama kuongeza kasi ya utekelezaji wa programu ya maboresho ya sekta ya sheria, kwani wabia wa maendeleo wanalalamika na wengine wamerudisha fedha zao ambazo zingetatua matatizo mengi.
Akigusia changamoto zilizobainishwa na Jaji Mkuu, Rais alimhakikishia kuwa Serikali itaendelea kuongeza bajeti kwa mhimili huo, ili haki itendeke ipasavyo na katika kupunguza msongamano wa kesi, ataendelea kuteua majaji kadiri atakavyoletewa mapendekezo.
“Nitaendelea kuteua majaji mkiniletea mapendekezo, maana watu wanadhani mimi ndio nawachagua, nitatekeleza uteuzi baada ya utaratibu wa uadilifu … katika miaka mitano mahakimu 256 waliajiriwa, mahakama 34 za mwanzo zilijengwa na tunaahidi tutaongeza bajeti,” alisema Kikwete.
Katika awamu yake ya uongozi wa nchi mpaka sasa Rais Kikwete ameteua majaji 52.
Rais Kikwete alisema hadi sasa Serikali imejenga Mahakama Kuu katika mikoa ya Kagera na Shinyanga katika miaka mitano iliyopita na kuahidi kuwa lengo ni kila mkoa uwe na mahakama hiyo.
Aliiagiza Mahakama kuharakisha utekelezaji wa mpango maalumu wa uendelezaji wa mahakama nchini, ili kuwezesha kujengwa kwa nyumba za mahakimu na mahakama na kuahidi kuhamasisha wananchi waliojitokeza kujenga sekondari 3,000 za kata nchini waone umuhimu pia wa kujenga mahakama.
Awali Jaji Mkuu alisema miongoni mwa changamoto zinazoikabili Mahakama ni upungufu wa mahakama hasa za mwanzo, na kutolea mfano kuwa majengo ya mahakama zilizopo mengi ni ya ‘mbavu za mbwa’ na mengine yapo katika majengo ya klabu za pombe, magulio na maghala
ya vijiji.
Akitoa kilio chake mbele ya Rais Jaji Mkuu alisema, “kwenye sera ya mikakati ya elimu, Serikali imeleta matumaini ya kishindo, hakuna Mkuu wa Shule ambaye anasimamia kwa wakati mmoja shule mbili ambazo ziko umbali wa kilometa 130 baina yao, kwa mantiki hiyo, hili la mahakama na mahakimu kuhudumia mahakama kwa umbali huo, linatibika.”
Alisema miongoni mwa mambo yanayowakwamisha ni kutopewa bajeti kamili kama wanavyoomba ambapo mwaka 2008/09 mahitaji yalikuwa ni Sh bilioni 93 lakini walitengewa Sh bilioni 50.2 sawa na asilimia 54 na kati yao zilizowafikia ni Sh bilioni 44.4.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema alisisitiza elimu zaidi itolewe kwa wananchi kuhusu mhimili huo na usuluhishi uanzie nje ya mahakama kupunguza mlundikano wa kesi.
Rais wa Chama cha Mawakili Tanzania Bara (TLS), Felix Kibodya, akihutubia sherehe hizo, alisema Watanzania wachache wanazijua hivyo kuongeza ugumu katika utekelezaji wake na kudhihirisha hilo, ni katika suala la uundwaji wa Katiba mpya.
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, akiwa mmoja wa viongozi wa kisiasa waliohudhuria sherehe hizo, aliliambia gazeti hili mara baada ya hafla hiyo kuwa utawala wa sheria utafanikiwa ikiwa watawaliwa watazijua sheria, hivyo kuitaka Serikali kuhakikisha hilo
linafanyiwa kazi.
No comments:
Post a Comment