Thursday, February 17, 2011

Wanasheria wapinga mkataba mpya na Dowans

WANASHERIA nchini wameonya kuwa kutaifisha mitambo ya kampuni ya kufua umeme wa dharura ya Dowans, au kuingia nayo mkataba mpya kwa madai ya kulinusuru Taifa na mgawo wa umeme, ni kujitia kitanzi cha kuilipa kampuni hiyo mabilioni mengine ya fedha.

Wameeleza kuwa endapo mpango wa mkataba mpya utawasilishwa bungeni na kupitishwa ili utekelezwe na Serikali, utalisababishia Taifa hasara kubwa, kwa kuwa Dowans haitaupinga kwa kuwa inafanya biashara na kujali maslahi yake zaidi ya Watanzania.

Wakizungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti, kwa masharti ya kutotajwa gazetini, wataalamu hao waliishauri Serikali iwe makini na mapendekezo au ushauri inayopewa na wabunge wake, ili kuepuka ‘mitego’ inayoweza kuingia kwa kivuli cha maslahi ya Taifa.

Mtaalamu wa kwanza alihoji uhalali wa Serikali kutumia Sheria ya Uhujumu Uchumi kwa kuuliza kama kampuni hiyo iliwahi kushitakiwa kwa kosa la jinai la kuhujumu uchumi wa Tanzania na kushindwa.

“Ninachofahamu ni kwamba Dowans hawajahujumu uchumi wala kushitakiwa kwa kosa hilo la
jinai, sasa sheria ya kuhujumu uchumi kwa suala lao itaingilia mlango gani?

Unataka kuniambia Serikali itatumia ubabe kuwataifishia mitambo? “Wakati huo sheria itakuwa wapi?

Hamwoni hapo ndipo tutakapoharibu na kudaiwa mabilioni mengi zaidi ya tunayodaiwa sasa na kampuni hiyo? Au ilikwishawahi kuisamehe Tanesco (Shirika la Umeme Tanzania) ili tuseme Serikali ilimalizana nayo?”

Alihoji mtaalamu huyo wa sheria. Mtaalamu mwingine wa masuala ya sheria pia akifafanua kuhusu suala hilo la uhujumu uchumi, alisema wabunge wanapaswa kukumbuka kuwa Dowans ndio walioshinda kesi ya madai iliyoamuliwa na Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Migogoro ya Kibiashara (ICC) kuitaka Tanesco iilipe.

“Sasa haya yatakuwa ni maajabu kwa Serikali kushauriwa kuitaifisha Dowans kwa sababu haijahujumu uchumi.

Na kisheria, anayehujumu uchumi ndiye anayepaswa kuwajibishwa kwa sheria hiyo tena kwa kutaifishiwa mali, sasa labda watwambie kama kuna kilichohujumiwa na kampuni hiyo, halafu tukafichwa, ili tusidhani kuwa Serikali inawekewa mtego,” alisema.

Alieleza kuwa kwa mujibu wa sheria, endapo Serikali itakubali kutumia sheria hiyo,
italazimika kuilipa Dowans fidia ya mitambo yake kulingana na bei inayotumika sokoni, ambayo hata hivyo alisema inaweza kuwa mzigo mkubwa tofauti na inavyofikiriwa na wanaotoa ushauri huo.

Mtaalamu huyo wa sheria, alitaja Ibara ya 24(1) na (2) ya Katiba na kuonya kuwa kipengele hicho kikitafsiriwa vibaya au kuchukuliwa kiholela, kinaweza kuleta matokeo mabaya.

“Katiba ya Jamhuri ya Muungano inatamka wazi kwenye ibara niliyoitaja pamoja na ibara zake mbili ndogo kuwa; kila mtu ana haki ya kumiliki mali, na ya kuhifadhi mali aliyonayo kwa mujibu wa sheria.

“Ibara ndogo ya 2 inasema; bila ya kuathiri masharti ya ibara ndogo (1), ni marufuku kwa mtu yeyote kunyang’anywa mali yake kwa madhumuni ya kuitaifisha au mengineyo bila idhini ya sheria ambayo inaweka masharti ya kutoa fidia inayostahili,” alisema.

Kuhusu wazo la kuingia mkataba mpya na Dowans wa kuwasha umeme japo kwa miezi mitatu ili kunusuru hali ngumu ya umeme iliyopo nchini kwa sasa, wataalamu hao walisema kushauri hivyo ni kuiingiza Serikali kwenye mtego wenye maslahi ya watu binafsi na wala si ya Taifa.

“Nilisikiliza hotuba ya Rais siku fulani na kumsikia akisema kuwa wataalamu wa sheria watatumika kuona watakavyofanya ili Tanesco isilipe deni hilo.

Rais aliitaka isiharakishe malipo hayo na nadhani alifanya hivyo kiuzalendo. “Sasa hawa wanaotaka Dowans ikodishwe tena na kuzalisha umeme wakati shauri la kwanza bado
halijaisha na Mahakama inayolishughulikia haijatoa uamuzi, wanalitakia mema Taifa hili kweli?

Au wanafanya hivyo bila kujua madhara yake baadaye kwa kampuni inayoidai Serikali?” Alihoji mtaalamu huyo.

Alionya kuwa kitendo hicho kitaipa kampuni hiyo nguvu maradufu za kusimamia uhalali wake na kusisitiza juu ya malipo yake ya awali.

“Nashauri busara itumike katika suala hili, kwa sababu linamgusa kila Mtanzania, mambo yachunguzwe kwa kina na mwenye maslahi yake asipewe nafasi ya kutoa ushauri, sidhani
kama Serikali haina namna nyingine zaidi ya Dowans. Nashauri iepukwe ili kutowachanganya wananchi,” alisema.

Vyombo mbalimbali vya habari nchini jana vilimnukuu Mbunge wa Bumbuli na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, January Makamba, akisema kuwa Kamati yake inajadiliana juu ya uwezekano wa kuishauri Serikali iingie mkataba na Dowans wa kuzalisha umeme wa dharura kwa miezi mitatu ili kumaliza tatizo la nishati hiyo.

Pamoja na mambo mengine, alikaririwa akisema itakapobidi, watatumia Sheria ya Kuhujumu Uchumi ili kutaifisha mitambo ya Dowans.

No comments: