WATOTO 10 waliofukuliwa kwenye shimo la takataka kwa pamoja wakiwa wamekufa katika kitongoji cha Msisiri, Mwananyamala katika Manispaa ya Kinondoni mkoani Dar es Salaam juzi, wakiwa wamezungushiwa shuka la Hospitali ya Mwananyamala, inadaiwa walizaliwa wafu na miili yao kukabidhiwa kwa wazazi wao.
Kutokana na kadhia hiyo iliyoshitua wengi, uongozi wa Wilaya ya Kinondoni umeunda timu ya watu watano wakiwamo madaktari wawili kutoka hospitali hiyo kuchunguza tukio hilo.
Akizungumza na waandishi wa habari jana juu ya tukio hilo, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Jordan Rugimbana, alikiri kuwa watoto hao walitokea Hospitali ya Mwananyamala ambayo ndiyo hospitali ya wilaya na baada ya vifo vyao, hospitali hiyo ilikamilisha taratibu zote zinazohusika kwa wazazi wa watoto hao.
“Ni kweli tukio hili tumelisikia na kwa uchunguzi wetu wa awali tumebaini kuwa watoto hawa hawakuuawa, bali walizaliwa wakiwa wamekufa na kukabidhiwa kwa wazazi wao kama taratibu zinavyosema,” alieleza Rugimbana.
Alisema ,kati ya watoto hao 10, saba walikuwa ni watoto waliotokana na kuharibika kwa mimba na watatu walizaliwa katika mimba zilizokamilika, lakini walikufa kutokana na matatizo ya kiafya akiwamo mmoja aliyezaliwa nje ya hospitali hiyo.
Hata hivyo, alisema pamoja na taarifa hizo za awali, ofisi yake imeunda timu ya madaktari wakiwamo wa nje ya Hospitali ya Mwananyamala kwa ajili ya kuchunguza kitaalamu zaidi juu ya kilichosababisha watoto hao kuzikwa nje ya utaratibu wa hospitali tena kwenye shimo moja la takataka.
“Inaelekea baada ya wazazi kukabidhiwa maiti za watoto wao kutokana na uwezo mdogo wa kifedha, walitafuta msaada nje ya hospitali wa mazishi na mtu aliyepewa dhamana hiyo kutokana na kutaka urahisi, aliamua kutumia shimo lililochimbwa na kuwazika watoto hawa kinyama,” alieleza Rugimbana.
Alisema, suala la shuka ya hospitali hiyo ambayo imekutwa kwenye miili ya watoto hao, ni moja ya hadidu rejea ya timu iliyoundwa ambayo imepewa siku saba kukamilisha kazi yake na itaongozwa na Dk. Charles Kamhando kutoka Kituo cha Afya cha Sinza wilayani humo.
DC alisema watachunguza uhalali wa shuka hiyo “japokuwa katika hospitali zote za Dar es Salaam wana utamaduni wa kusaidia mtu asiye na uwezo wa sanda na kumpatia shuka.”
Naye Mganga Mkuu wa hospitali hiyo, Dk. Saphonias Ngonyani, alisema watoto hao saba waliotokana na kuharibika kwa mimba, walikuwa ni wa kuanzia wiki 28 na tayari walikuwa wameshabadilika na kuwa binadamu.
Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela, alisema tayari polisi inamshikilia na kumhoji mtu mmoja kwa sababu za uzembe kutokana na tukio hilo na mtuhumiwa mwingine anatafutwa.
“Siwezi kuwataja majina yao kwa sasa kwa sababu za uchunguzi, lakini mmoja tunamhoji na mwingine bado tunamtafuta. Na ninawaahidi kuendelea kulichunguza suala hili kwa kushirikiana na timu iliyoundwa hadi pale ukweli utakapobainika,” alisema Kamanda Kenyela.
Aidha, Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni, Raphael Ndunguru, alisema timu hiyo iliyoundwa itachunguza kitaalamu kuanzia vifo vya watoto hao, utaratibu mzima wa makabidhiano ya maiti kwa mujibu wa taratibu za hospitali na kilichotokea hadi kuzikwa kwenye shimo moja.
“Pia kwa vile hospitali ina anuani za wazazi wa watoto hawa, kamati itawasiliana nao ili wawataje waliowasaidia kuhifadhi maiti za watoto wao na hapo ndipo ukweli utakapojulikana,” alisema Ndunguru.
Alisema anachofahamu yeye ni kwamba iwapo mtu atakumbwa na tatizo la kifedha juu ya maziko katika hospitali hiyo, Manispaa inayo bajeti ya kusaidia. “Tunaomba wale wote ambao wanakumbwa na matatizo haya wafuate mamlaka husika na kutoa taarifa, lakini si watu baki,” alisema Ndunguru.
Katika mkutano huo yalizuka malumbano baina ya waandishi wa habari na timu ya madaktari akiwamo Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Dk. Judith Kahama, juu ya taarifa za madaktari hao kuhusu umri wa watoto waliokutwa kwenye shimo hilo.
Waandishi walidai kuwa umri wa watoto unaonekana ni mkubwa na si kama madaktari hao wanavyodai kuwa ni mimba zilizoharibika kwani wapo watoto ambao hata nywele zao zinaonekana zimeshakatwa.
“Mimi nazungumza kitaalamu, watoto hawa ni wa kuanzia wiki ya 28 na si premature (njiti) kama watu wanavyodai,” alisema Dk. Kahama.
Katika taarifa ya polisi iliyotolewa jana Dar es Salaam, ilifafanua kuwa mkazi wa Msisiri Mwananyamala, Amour Mbaga katika shimo lake la takataka, alikuta watoto wachanga 10, watano wa kike na watano wa kiume na kati ya watoto hao watatu walizungushiwa kwenye khanga zenye majina ya mama zao.
Majina ya akinamama hao ni Furaha Rajabu mkazi wa Manzese aliyejifungua mtoto wa kiume Januari 24, mwaka huu na kwa mujibu wa taarifa za hospitali, inaonesha alichukuliwa na baba yake, Idrisa Zuberi siku hiyo hiyo.
Pia Ruth Mtanga ambaye kumbukumbu za hospitali zinaonesha alijifungulia njiani mtoto wa kiume Januari 27, mwaka huu na mtoto huyo kufariki, kumbukumbu hazioneshi maiti hiyo kuingia wala kutoka hospitalini hapo, ingawa kumbukumbu za mama huyo kupokewa na kutibiwa zilikuwapo.
Aidha, mwingine ni Regina Samweli wa Kimara, ambaye kumbukumbu zinaonesha alijifungua hospitalini hapo mtoto wa kike mfu, lakini kumbukumbu za chumba cha maiti hazioneshi maiti hiyo kuingia wala kutoka.
“Watoto wengine saba walikuwa wamefungwa kwenye shuka la Hospitali ya Mwananyamala Wodi namba 1A na hakuna kumbukumbu yoyote inayoonesha kuwa wamezaliwa na kufa hospitalini hapo,” ilisema Polisi.
No comments:
Post a Comment