KUNA kila dalili kuwa watawala wetu wana tatizo la kuheshimu utawala wa sheria.
Kuheshimu huko kunaonyeshwa kwa njia moja tu nayo ni kuifuata sheria na kutekeleza kile sheria inataka kwa namna yoyote ile.
Matukio kadhaa ya hivi karibuni yanazidi kunifanya niamini kuwa watawala wetu wanataka kutawala kwa hisia, vionjo na mitazamo yao binafsi, wakiamini kuwa vitu hivyo kwa namna moja au nyingine vina uhusiano wowote ule na sheria.
Sasa, kama mtu anayeonyesha kutokujali sheria ni mtu wa ngazi ya chini, ambaye hana madaraka makubwa, tunaweza kusema kuwa anahitaji kupelekwa semina au mafunzo fulani au kupewa maelekezo ya nini cha kufanya.
Lakini inapotokea kuwa mtu anayeonyesha kutokufuata sheria na kuheshimu utawala wa sheria ni waziri au kiongozi wa ngazi za juu serikalini, basi kiwango cha matatizo kinakuwa kimeongezwa kwa kasi ya ajabu.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Utumishi) Hawa Ghasia wiki iliyopita alisema kitu bungeni ambacho kilinikumbusha alichosema Waziri Mkuu miezi michache iliyopita pale alipohalalisha uvunjaji wa sheria tena kwa machozi.
Wote wawili japo kwa namna mbalimbali wameendelea kuthibitisha kila ambacho wengi tunakijua, tumekishuhudia na kwa muda mrefu tumekivumilia yaani, sheria inafuatwa pale wanapojisikia, na pale wanapotakiwa kuifuata wanajizuia kwa kusingizia kujisikia.
Kwa Waziri Mkuu alipozungumzia lile suala la mauaji ya albino tulipiga kelele na kwa machozi yake akatutuliza. Lakini baadaye akaenda Iringa ambako huko nako akasema maneno fulani ambayo japo hayakupata mbiu kubwa kwenye vyombo vya habari lakini kimsingi yalikuwa yanaingilia utendaji kazi wa Mahakama kuhusiana na viongozi wa serikali kumfungulia mashtaka kiongozi mmoja wa CCM.
Lakini kilichonishtua zaidi ni haya ya mama Ghasia. Wengi walioandika juu ya kauli yake walikwazwa zaidi na suala la nyaraka kuwa ni za siri na wanaovujisha watachukuliwa hatua. Binafsi kilichonikwaza zaidi ya hicho ni madai kuwa kwenye Bunge letu kuna wezi!
Soma zaidi
No comments:
Post a Comment