MWISHONI mwa wiki hii Tanzania ilijiunga na wadau wa habari duniani kuadhimisha siku ya uhuru wa vyombo vya habari duniani. Mwaka jana juma kama la leo niliandika makala kuhusu maana ya dhana ya uhuru wa vyombo vya habari kwa ujumla na pia nikatathmini mwenendo wa vyombo vya habari nchini.
Tunapoelekea katika uchaguzi, kama nilivyoeleza katika makala zangu za hivi karibuni, vyombo vya habari vinaweza kujikuta vikichezewa na wenye maslahi ya kisiasa na kupoteza mwelekeo. Lakini daima, faida zinazotokana na uwepo wa uhuru wa vyombo vya habari ni kubwa kuliko kinyume chake. Labda nirejee tena makala yangu ya mwaka jana niliyoitoa baada ya maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani, Mei 3.
Siku hii hutumika na wanahabari duniani kote kutathmini ni kwa kiasi gani nchi husika imejitahidi kuhakikisha inalinda, au kuingilia, uhuru wa vyombo vya habari. Kwa kawaida, kama nilivyokwishasema huko nyuma, wapo watu ambao huchanganya dhana hizi mbili: Uhuru wa Habari na Uhuru wa Vyombo vya Habari.
Uhuru wa habari ni haki ya kila mtu kuwa na uhuru wa kupata taarifa, kuwa na maoni na kusambaza taarifa kupitia njia za kuhabarishana. Haki hii ni ya kila mtu, bila kujali fani yake wala hadhi yake katika jamii. Ni haki anayozaliwa nayo kila mtu.
Uhuru wa vyombo vya habari, kwa upande mwingine, unagusa moja kwa moja vyombo vya habari. Uhuru huu unahusu haki ya vyombo vya habari kufanya kazi zake kitaaluma bila kuingiliwa wala kusukumwa na mtu au taasisi yeyote.
Kwa hiyo kuwepo uhuru wa vyombo vya habari kunaweza kusaidia kushamirisha haki ya kila mtu ya kupata na kusambaza habari au maoni. Hapo ndipo dhana hizi mbili zinapokutana.
Msingi wa haki ya uhuru wa habari uko katika Ibara ya 19 ya Tamko la Kimataifa la Haki za Binadamu la 1948 (Universal Declaration of Human Rights) na ni sehemu ya haki zingine kadhaa za binadamu ambazo sehemu kubwa zimeainishwa katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Katika kuangalia Uhuru wa vyombo vya habari vipo vigezo kadhaa ambavyo ni muhimu kuvitathmini. Kwanza ni lazima sera na sheria za nchi ziendane na dhana nzima ya uhuru na haki za binadamu kama zilivyoainishwa katika matamko kadhaa ya kimataifa. Leo hii hapa Tanzania haki ya uhuru wa habari inalindwa na Katiba katika ibara ya 18 Kipengele cha (1) na (2).
Lakini bado nchi yetu iko katika mchakato wa kutunga sheria ya Uhuru wa Habari na nyingine ya mwongozo kwa vyombo vya habari ambazo zitasaidia kushamirisha uhuru wa habari kwa upande mmoja na uhuru wa vyombo vya habari kwa upande mwingine.
Soma zaidi
No comments:
Post a Comment