Wednesday, May 6, 2009
WAKULIMA WADAI MBOLEA YA MINJIGU KWA WAZIRI MKUU
WAKULIMA wa kijiji cha Mtama wilayani Mbinga, Ruvuma, wamemwomba Waziri Mkuu Mizengo Pinda ahakikishe kuwa wataendelea kupatiwa mbolea ya Minjingu kwa sababu imewasaidia kuongeza mavuno ya mahindi kwa karibu mara tatu.
Ombi hilo lilitolewa kwa Waziri Mkuu jana (Jumatatu, Mei 4, 2009) mara baada ya kukagua shamba la mahindi la majaribio ya matumizi ya mbolea mbalimbali katika kurutubisha ardhi kwenye kijiji hicho ambako alishuhudia mahindi yaliyopandwa kwa kutumia mbolea tofauti.
Akitoa taarifa mbele ya Waziri Mkuu, Mwenyekiti wa kikundi cha majaribio ya mbolea Mtama (KIMTA), Bw. Gizla Mbugu alisema wanahitaji zaidi mbolea ya Minjingu kwa sababu wamebaini wakiichanganya na mbolea ya kukuzia aina ya urea wanapata mavuno mengi zaidi.
“Ukipanda kwa mbolea ya Minjingu na kutumia mbolea ya urea kukuzia una uwezo wa kuvuna si chini ya magunia 16 kwa ekari moja wakati ukipanda bila mbolea na usipotumia mbolea ya kukuzia unapata magunia matatu hadi matano kwa ekari moja, ukitumia DAP peke yake unavuna magunia 17 kwa ekari moja lakini tatizo ni bei kubwa ya mbolea hiyo,’’ alisema.
Alimweleza Waziri Mkuu kwamba katika majaribio yao wamebaini kwamba wasipotumia mbolea wakati wa kupanda mahindi lakini wakatumia mbolea ya kukuzia aina ya urea wanaweza kuvuna magunia matano hadi nane kwa ekari moja.
Lakini alimtahadharisha Waziri Mkuu kwamba walijaribu pia kutumia mbolea ya urea kupandia na kukuzia kwa sababu kuna wakulima ambao walikuwa wakifanya hivyo na mwaka jana waliweza kuvuna magunia nane kwa kila ekari lakini mwaka huu mahindi yameota bila kuzaa chochote kwa hiyo hawatavuna kitu.
Naye mkulima wa kijiji cha mtama, Bw. Allen Nombo alisema wanaomba uamuzi wa kuleta mbolea ya Minjingu usiwe ni wa majaribio bali uwe endelevu kwa sababu wameweza kumudu bei ya mbolea hiyo. Hivi sasa bei ya mfuko wa kilo 50 ni sh. 25,000/- hadi 30,000/- bila ruzuku wakati mbolea ya ruzuku inauzwa kati ya sh. 15,000/- hadi 18,000/- kwa mfuko huo huo wa kilo 50.
Taarifa kutoka ofisi ya kilimo zinasema wakulima wengi wanashindwa kumudu mbolea ya DAP kwa sababu mfuko mmoja wa kilo 50 unauzwa kati ya sh. 90,000/- hadi 120,000/- bila ruzuku wakati mfuko wa urea kilo 50 unauzwa kati ya sh. 40,000 na sh. 50,000/- kwa hiyo wakulima wanaona ni nafuu kuchanganya mbolea zaminjingu na urea.
Waziri Mkuu pia amekagua shamba la mahindi la majaribio ya matumizi ya mbolea mbalimbali katika kurutubisha ardhi katika kijiji cha Mtama; kukagua mtambo wa kukoboa kahawa katika kijiji cha Utiri na kutembelea kituo cha utafiti wa Kahawa cha TACRI katika kijiji cha Myangayanga.
Leo (Jumanne, Mei 5, 2009) Waziri Mkuu atakwenda Kigoma kwa ziara ya siku mbili ambako atazuru wilaya za Kigoma na Kasulu kwa kutembelea miradi ya kilimo na umwagilaijai ikiwa ni pamoja na kukabidhi power tillers.
Ziara ya Waziri Mkuu katika mikoa ya Ruvuma, Kigoma na Rukwa ni mfululizo wa ziara zake za kufuatilia maagizo ya kilimo yaliyofikiwa katika mkutano aliouitisha Oktoba mwaka jana kuweka malengo ya kuinua kilimo katika mikoa sita ya Morogoro, Iringa, Mbeya, Ruvuma, Kigoma na Rukwa.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMANNE, MEI 5, 2009.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment