Monday, May 4, 2009
Rostam amvurumishia makombora Mengi
Mfanyabiashara bunge wa Igunga, Rostam Aziz, amemuelezea Mwenyekiti Mtendaji wa IPP, Reginald Mengi kuwa ni nyangumi wa ufisadi na akatangaza kupeleka faili lenye ushahidi wa matendo yake maovu kwa vyombo husika ili vimchunguze.
Katika kujibu madai ya Mengi kuwa mbunge huyo ni miongoni mwa mafisadi papa watano nchini, Rostam alidai Mengi ni nyangumi wa ufisadi anayewahujumu masikini huku akijidai kwamba anawaonea huruma na wakati huo huo kuomba huruma ya wananchi.
Sanjali na hilo, Rostam anakusudia kumshitaki Mwenyekiti Mtendaji huyo wa IPP baada ya kushindwa kukanusha na kumwomba radhi katika muda wa saa 48 alizompa wiki iliyopita kutoka na madai hayo aliyoyatoa katika mkutano wake na waandishi wa habari Aprili 23, mwaka huu jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari jana Dar es Salaam, Rostam ambaye pia ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) na Kamati Kuu (CC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), alitoa nyaraka mbalimbali za kuunga mkono madai yake ya Mengi kufilisi mali za Watanzania ukiwamo ubadhirifu katika iliyokuwa Benki ya Taifa ya Biashara (NBC).
“Mengi ni nyangumi wa ufisadi nchini, alianza kushiriki kuifilisi nchi kwa kushiriki katika vitendo vya ufisadi vilivyochangia kuifilisi iliyokuwa Benki ya Taifa ya Biashara (NBC), ambayo ni mali ya Watanzania na hatimaye kupelekea kubinafsishwa kwake kwa bei poa,” alisema Rostam katika mkutano huo.
Huku akitaja akaunti namba za kampuni zinazodaiwa kuwa za Mengi ikiwamo Anche Mwedu Limited (AML), Rostam alidai Mengi alichukua mkopo mwanzoni mwa miaka ya 1980 wa mabilioni ya shilingi na amegoma kuyalipa hadi leo na kulazimisha suala hilo kufikishwa mahakamani.
“Jumla ya fedha zote za NBC ambazo akidaiwa Mengi kupitia kampuni yake ya Anche Mwedu Limited (AML) hadi kufikia Januari 1996 zilikuwa ni Sh 5,863,002,196.45. Fedha hizi hadi kufikia sasa 2009 pamoja na hesabu ya riba zinafikia takriban bilioni 28,” alidai Rostam.
Alidai kuwa mbali na fedha hizo za NBC, alimtuhumu Mengi kwa kuchukua fedha nyingi kupitia msaada wa nchi wafadhili wa kuagiza bidhaa kutoka nje (CIS), ambazo anadai hajazilipa hadi leo.
“Wafanyabiashara wengi tulikopa, lakini tumelipa na tunaendelea kulipa. Mengi anayedai ana uchungu na Watanzania anawaongezea umasikini kwa kuchota fedha hizo na baadaye kuruka na kukataa kuzilipa hadi leo,” alidai Rostam na kuorodhesha kiasi hicho cha fedha alichokopa Mengi.
Aidha, alimtuhumu Mengi kwa kutumia nafasi yake ya Mwenyekiti wa Kamati ya Uwekezaji ya Kampuni ya NICO kukiuka maadili ya kibiashara na kuitumbukiza katika kununua hisa za kiwanda cha Interchem Pharma Ltd ambacho alisema kinamilikiwa na familia ya Mengi, wakati akijua kilikuwa njiani kufilisika.
“Huku akijua hali mbaya ya kiwanda hicho alitumia nafasi yake kuziteketeza Shilingi bilioni 2.558 fedha za Watanzania masikini wasiopungua 22,000 wenye hisa katika NICO kwa kuifanya inunue asilimia 51 ya hisa (majority shareholding). Kiwanda hicho sasa kimewekwa kwenye orodha ya kufilisiwa baada ya kushindwa kujiendesha chini ya mwaka mmoja tokea Mengi kuizamisha NICO,” alidai.
Alimtuhumu pia akiwa mbia na serikali katika kiwanda cha TANPACK, alitumia dhamana ya kiwanda hicho kisirisiri kwenda kukopa Sh milioni 600 kwa NBC na kuzitumia kwa njia anazozijua, na alitaka deni lilipwe na mbia mwenzake, ambaye alikataa kulitambua na hivyo TANPACK ikafilisiwa.
Mbali na hayo, Rostam alidai kwa ujumla Mengi si msafi kama anavyotaka jamii iamini, ikiwamo kutaja ugomvi wake na watu mbalimbali, uanzishaji wa magazeti kwa nia ya kuwachafua wagomvi wake na zaidi akadai ndiye kinara wa kuchafua wenzake kwa lengo la kuleta chuki na mifarakano nchini.
“Najua atakanusha haya kwa sababu yeye ni mwepesi wa kulalamika kuwa anaonewa huku akidhani amepewa haki na Mungu ya kuonea wengine,” alisema Rostam na kuongeza kuwa hatua ya Mengi kuwaita wengine wauaji pasipo kutoa ushahidi wowote na pia kurejea madai ya kutaka kuuliwa au kudhuriwa mara kwa mara ni dalili ya kuchanganyikiwa.
Alisema mbali ya Mengi kumtuhumu yeye na wengine kuwa na akaunti ya fedha za kigeni nje ya nchi ambako ndiko wanakoweka fedha zao, alidai Mengi ndiye mwenye akaunti ya fedha za kigeni nje ya nchi. “Nampa changamoto akanushe kwamba hana akaunti ya fedha za kigeni nje ya nchi,” alisema.
“Niseme kwamba tofauti na yeye ambaye ameishia kutoa porojo zake bila ya kufikisha hoja na ushahidi wake kwa vyombo vya sheria vinavyohusika au kutoa ushahidi, mimi nawagawia hapa baadhi tu ya ushahidi wa ufisadi wa Mengi ambao pia nakusudia kuuwasilisha pamoja na maelezo haya kwa vyombo husika ili wamchunguze Mengi na kuchukua hatua zipasazo,” alisema Rostam.
“Kwa upande mwingine, nimewaagiza wanasheria wangu kuzifanyia kazi tuhuma za uzushi alizozitoa na kuchukua hatua za kisheria zinazofaa dhidi yake,” alisema Rostam na kuongeza kuwa atawasilisha ushahidi huo kwa vyombo husika ndani ya saa 48.
Alisema aliamua kumjibu Mengi kwa sababu alishindwa kuwasilisha ushahidi wa tuhuma alizotoa dhidi yake kwa vyombo vya sheria vinavyohusika na pia kumwomba radhi.
“Na nilimwambia wazi kuwa asipofanya mojawapo kati ya hayo, nitakuwa na haki ya kumuanika ili Watanzania waelewe tabia na hulka ya mtu huyu. Hakufanya chochote kati ya hayo. Na hawezi kufanya hivyo kwa sababu anaelewa alichokisema ni uzushi alioutunga mwenyewe,” alisema Rostam na kuongeza kuwa hiyo ndiyo sababu ya kuitisha mkutano wa jana ili kuweka kumbukumbu sahihi.
Mbunge huyo akijibu maswali ya waandishi wa habari, alisisitiza kwamba hahusiki na kashfa mbalimbali zinazotajwa kumhusisha naye na kueleza kuwa kashfa hizo zimeenezwa ili jamii iamini ni za kweli, wakati ni uongo. Alirudia kutoa changamoto kwa ye yote mwenye ushahidi kumpeleka mahakamani.
Wiki iliyopita, Mengi aliitisha mkutano na waandishi wa habari na pia kusoma taarifa katika televisheni anayoimiliki ya ITV, akiwatuhumu wafanyabiashara watano wenye asili ya Kiasia akiwamo Rostam, kuwa ni mafisadi papa, lakini pia kutaja ushahidi akisema yuko tayari kushitakiwa.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment