Serikali inatarajia kuandaa muswada wa sheria kwa lengo la kuwahakikishia hifadhi na usalama zaidi watu wenye ulemavu nchini wakiwamo maalbino.
Kwa sasa iko katika mchakato huo ambao baada ya kukamilika, muswaada huo utawasilishwa bungeni na kutungiwa sheria.
Mpango huo wa serikali ulitangazwa jana na Makamu wa Rais, Dk. Ali Mohammed Shein wakati akihutubia Maadhimisho ya Nne ya Siku ya Maalbino nchini yaliyofanyika katika Uwanja wa CCM Kirumba, jijini Mwanza.
Dk. Shein alisema hatua hiyo ni miongoni mwa jitihada za serikali za kutekeleza kwa vitendo Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara 14.
Alifafanua kuwa mchakato huo unafuatia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuridhia Mkataba wa Kimataifa wa Hifadhi ya Watu Wenye Ulemavu ambao utekelezaji wake unasadifu matakwa ya Ibara ya 14 ya Katiba inayotamka kuwa kila mtu anayo haki ya kuishi na kupata kutoka katika jamii, hifadhi ya maisha yake kwa mujibu wa sheria.
``Serikali inaamini katika suala la utawala bora na mfumo wa sheria hivyo haitavumilia kuona kuwa haki za raia wake zinavunjwa au zinapuuzwa,`` alisema.
Alisema vitendo wanavyofanyiwa albino nchini sio tu visivyovumilika bali pia ni vya uvunjaji wa Katiba na sheria ya nchi na kwamba serikali itaendelea na vita dhidi ya watu wanaofanya vitendo hivyo.
Makamu wa Rais alisisitiza kuwa serikali itaendeleza mapambano makali dhidi ya vitendo hivyo kwa uwezo wake wote katika jitihada za dhati za kutokomeza udhalimu dhidi ya utu wa albino.
Hata hivyo, alisema ili kufanikisha azama hiyo, hapana budi kuwepo Katika maadhimisho hayo yaliyohudhuriwa na maelfu ya wakazi wa Jiji la Mwanza, Makamu wa Rais alitoa tena wito wa serikali kwa Watanzania wa kuacha kuendeleza imani potofu za kishirikina ambazo zinasababisha janga kwa albino.
Awali, Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Profesa David Mwakyusa,alitaja hatua zaidi zinazochukuliwa na serikali katika kuhakikisha walemavu na albino wanapata fursa na huduma zaidi na bora kuzingatia mahitaji yao.
Profesa Mwakyusa alizitaja miongoni mwa hatua hizo ni kupitisha baadhi ya miongozo ikiwamo ya elimu shirikishi na mwangozo wa kuwatambua mapema watoto wenye ulemavu.
Kuhusu ombi la kutaka matibabu ya albino yasilipiwe, alisema suala hilo limezingatiwa katika sheria mpya lakini aliongeza kuwa tayari huduma hizo hutolewa bure katika kituo cha Mkindo kilichopo mkoani Mwanza ambako kuna albino 92.
No comments:
Post a Comment