Friday, May 29, 2009

Wabunge Wawe na Ukomo wa Kuwakilisha.

TANGU ulipoanzishwa tena mfumo wa vyama vingi mwaka 1992 taratibu na sheria mbalimbali zilirekebishwa na mpya kupitishwa ili kuendana na mabadiliko hayo. Mojwapo wa sheria na mabadiliko hayo ni ile ambayo inatoa fursa kwa wabunge kuendelea kulitumikia taifa kwa vipindi zaidi ya viwili. Aidha sheria hiyo inatoa fursa kwa wabunge wetu kuwakilisha wananchbi wao kwa muda ambao hauna kikomo. Katiba ya Jumuhuri ya Muungano ya Mwaka 1977 na marekebisho yake ya 2005, sura ya tatu, sehemu ya pili, kifungu cha 71(1) kinaeleza muda wa wabunge kushika madaraka.

Kifungu hiki kinaeleza mambo takriban saba ambayo yanaweza kusababisha mbunge kupoteza sifa yake ya kuwa mwakilishi. Kati ya hayo saba hakuna ukomo unaotokana na muda wa uwakilishi, hivyo basi mbunge anaweza kuwakilisha wananchi wake mpaka utashi wake utakapoamua kuachia wengine wawakilishe.

Kupata bahati ya kulitumikia taifa lako ni kitu kizuri, na wengi tunapenda kufanya hivyo. Katika Tanzania yetu ambayo ina nafasi chache za kulitumika taifa, kila mtu angependa kulitumikia taifa hili. Wabunge wetu wamefanya kazi kubwa ya kulitumikia taifa hili tangu hapo awali, na tunawapongeza sana kwa hilo. Ila sasa wakati umefika kwa wabunge wetu ambao wameshalitumikia kwa vipindi zaidi ya viwili vya miaka mitano mitano kuachia ngazi na kuwapisha wananchi wengine wenye nia na uwezo kama wao walivyofanya.

Ipo haja kwa wadau na watetezi wa demokrasia kuangalia upya sheria hii ya uwakilishi na kurekebishwa ili iweze kutoa mwanya kwa watu wengine kuwakilisha wananchi na kuleta mawazo mbadala katika uongozi wa bunge letu na serikali yetu. Makala haya ni chachu ya kuanzishwa kwa mjadala mpana juu sheria hii, wakati huu tukielekea katika mwaka uchaguzi wa 2010. Ni vyema wadau wa demokrasia kuchukua fursa hii kuangalia upya sheria hii ili ibadilishwe na kutoa nafasi kwa wawakilishi wapya ambao watakuwa na mawazo na mbinu mpya za kuleta maendeleo ya taifa hili.

Kuachia nafasi kwa wengine nao waongoze ni uzalendo pia, kwani itasaidia kutoa fursa kwa wenye mawazo mbadala kuleta maendeleo, kutoa nafasi kwa wananchi wengi zaidi kuchangia katika maendeleo ya nchi yao, kutoa fursa kwa wazelendo wengine kuchangia katika ujenzi wa taifa lao. Pamoja na faida nyingi ambazo zitapatikana endapo sheria hii itarekebishwa, pia wabunge wetu watapata bahati ya kulitumikia taifa letu kwa vipindi visivyozidi viwili vya miaka mitano kila kimoja tofauti na sasa ambapo kuna baadhi ya wabunge wameshalitumika bunge kwa zaidi ya miaka kumi na mitano.

Miaka kumi na tano kwa namna yoyote ile ni mingi sana katika suala zima la maendeleo ya nchi husika. Watu wengi wanapenda kupata fursa hii ya kulitumikia taifa lao, lakini sheria hii inawazua kushiriki katika ujenzi huo wa taifa. Mwanzoni mwa mwa mfumo wa vyama vingi, wadau wa demokrasia waliibua hoja ya kuwa na katiba mpya ambayo itakidhi matakwa ya mfumo wa demokrasi.

Madai waliyoyatoa ni pamoja na kwamaba katiba iliyopo ina viraka vingi na iliundwa kukidhi matakwa ya mfumo wa chama kimoja, hivyo walionelea heri kuitishwa mkutano wa kitaifa kujadili uandaaji wa katiba mpya itakayokidhi matakwa ya watu wote. Jambo hili halikutokea. Kuna sababu kadhaa zilitolewa na chama tawala ili kuzuia katiba yetu isibadilishwe. Huu ni wakati mwafaka wa kuibuia hoja ya kuijadili upya katiba yetu.


Wabunge wengi wanatarajiwa kukataa sheria hii kubadilishwa. Wakati tunaelekea uchaguzi mkuu wa mwakani, ni bora wanaharakati wa maendeleo kupambana na kuwezesha kuanzishwa kwa mijadala na harakati za kitaifa za kudai wabunge wawe na uongozi wenye kikomo. Kwa haraka-haraka sheria hii ikibadilishwa itaongeza sana ufanisi kwa wabunge wetu na kuleta maendeelo haraka katika nchi yetu, pamoja na faida nyingine kibao zitafuata. Kwa nini wabunge wang’ang’anie kubaki madarakani kwa muda mrefu bila kuachia madaraka kwa wengine? Tanzania haina wawakilishi wa kutosha ama? au watu wenye uwezo wa kuongoza hawatoshi?

Mjadala huu bado upo wazi na tunatoa nafasi kwa wanaharakati na wapenda maendeleo ya nchi hii kuchangia na kuja na mawazo mbadala juu ya sheria inayonyima ukuaji wa demokrasia ya kweli ya uwakilishi.

Na aidan Mmari.


Makala haya yalichapwa katika gazeti la mwananchi la tarehe 26/05/09.

No comments: