RAIS Jakaya Kikwete amekionya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kuacha vitendo na kauli za kuwajengea wananchi hofu kuhusu usalama wa nchi yao.
Amesema, vitendo hivyo vya Chadema vina dhamira ya kutaka kuleta machafuko makubwa na uvunjifu wa amani nchini.
“Kufanya maandamano na mikutano ni haki ya msingi ya vyama vya siasa na raia. Lakini, kuigeuza fursa hiyo kuwa jukwaa la kuchochea ghasia kwa nia ya kuiondoa Serikali iliyoko madarakani kwa mabavu, ni matumizi mabaya ya fursa hiyo,” amesema Rais.
Rais Kikwete alikuwa akilihutubia Taifa jana katika utaratibu wake wa kuzungumza na wananchi kwa njia ya televisheni na redio.
Alisema, Tanzania ni nchi ya kidemokrasia na kila miaka mitano uchaguzi wa viongozi unafanyika na wa mwisho ukiwa ni uliofanyika Oktoba 31 mwaka jana.
“Kabla ya hapo tulikuwa na kampeni zilizochukua karibu miezi miwili na nusu. Kila chama kilielezea jinsi kitakavyokabiliana na matatizo ya wananchi wa nchi yetu, ikiwa ni pamoja na haya wanayoyazungumza sasa.
“Iweje leo, miezi mitatu baadaye kwa mtu au chama cha siasa kufanya maandamano kwa masuala yale yale waliyoyasema kwenye kampeni? Si sawa hata kidogo. Kuchochea ghasia eti kwa nia ya kuiondoa Serikali madarakani ni kinyume cha Katiba na ni kuiingiza nchi katika mgogoro usiokuwa wa lazima. Tutasababisha umwagaji wa damu, watu kupoteza maisha na mali zao kuharibiwa bila sababu yoyote ya msingi,” alihadharisha Rais.
Aliwaasa Chadema kutumia Bunge na halmashauri za wilaya kuboresha sera na hoja zao na kuziwasilisha kwa watu badala ya kuzunguka nchi nzima kuchochea ghasia kwa lengo la kuingia madarakani.
“Tutajenga misingi ya hovyo na nchi yetu itakosa amani na utulivu daima. Hebu fikirieni, kama kila atakayeshindwa uchaguzi anafanya hivyo tutakuwa nchi ya namna gani? Tanzania yetu hii yenye sifa na heshima ya kuwa nchi ya amani na utulivu itapoteza kabisa sifa hiyo, na badala yake umwagaji damu na mateso kwa watu wasiokuwa na hatia vitageuka kuwa maisha ya kawaida,” alisema Rais.
Alikiri kuwa hali ya maisha ni ngumu na kukabiliana nayo ndiyo kazi inayofanywa kila siku na Serikali na ndiko ilikoelekeza nguvu zake na mafanikio yanaonekana katika nyanja mbalimbali na maeneo mbalimbali.
“Kikwazo si upungufu wa sera wala dhamira, bali kikubwa ni kiwango cha maendeleo madogo ya uchumi wetu na hivyo uwezo wetu si mkubwa wa kuyakabili na kuyamaliza matatizo yote haraka kama ambavyo tunapenda iwe.
“Hayo si matatizo ya kumalizika ndani ya siku tisa. Mzee Nyerere aliongoza kwa miaka 23 na hakuyamaliza matatizo ya maendeleo ya nchi hii. Na wale wa umri wangu au kunizidi, wanakumbuka hali ilivyokuwa wakati anang’atuka. Hakuacha nchi ikiwa tajiri.
“Mzee Mwinyi kakaa miaka 10 hakuyamaliza, Mzee Mkapa naye miaka 10 hakuyamaliza.
Miye nimekaa miaka mitano hayakwisha na nitamaliza mitano hayataisha yote. Lililo muhimu kuliko yote ni kuwa katika kila awamu nchi yetu imekuwa inapiga hatua ya kusonga mbele katika kujiletea maendeleo,” alisema.
Viongozi wa Chadema wanazunguka mikoani wakifanya mikutano ya kuhamasisha wananchi kuichukia Serikali iliyoko madarakani kwa madai kuwa imeshindwa kumaliza matatizo ya wananchi na hata kufikia kumwekea Rais muda wa kutatua matatizo hayo.
Rais Kikwete alisema ni kweli kuna hali ngumu ya maisha, na kwamba kukabiliana nayo ndiyo kazi wanayoendelea nayo kufanya kila siku.
"Tumeelekeza nguvu zetu na rasilimali zetu huko na mafanikio yanaonekana katika nyanja mbalimbali na maeneo mbalimbali. Kikwazo siyo upungufu wa sera wala dhamira, kikwazo kikubwa ni kiwango cha maendeleo madogo ya uchumi wetu na hivyo uwezo wetu siyo mkubwa wa kuyakabili na kuyamaliza matatizo yote haraka kama ambavyo tunapenda iwe.
Lakini, pia ni muhimu watu kutambua ukweli kwamba uchumi kama wetu ambao haujajenga uwezo wake wa ndani wa kujitosheleza kwa mahitaji yake, huathirika sana na yale yanayotokea katika uchumi wa dunia. Unapoyumba na sisi tunayumba. Bei za mafuta katika soko la dunia zikipanda na kwetu kupitia gharama za uchukuzi na uzalishaji huongezeka na kusababisha bei za bidhaa kupanda," alieleza Rais.
"Mfumuko wa bei ukipanda China, nguo na bidhaa tunazonunua kutoka China hupanda bei. Hivi sasa mataifa yote makubwa tunakonunua bidhaa mfumuko wa bei umepanda na sisi tunaathirika. Mvua ikikosekana kunakuwa na uhaba wa chakula, bei za vyakula hupanda na watu wengine hukosa chakula
"Lawama kwa Serikali au Rais Kikwete inaanzia wapi? Hata kwa matatizo yote hayo na mengine tumekuwa tunatafuta nafuu kwa kiwango tunachoweza. Aghalabu, hutoa nafuu ya kodi kama tulivyofanya kwa sukari na tulivyowahi kufanya kwa saruji na kadhalika. Tutaendelea kufanya hivyo inapobidi."
Kuhusu umeme, Rais alisema imekubalika kukodi mitambo ya megawati 260, lakini ikasisitizwa kuwa pamoja na udharura uliopo, sheria na taratibu za ununuzi wa umma vizingatiwe. Pia, ihakikishwe kuwa mikataba inayoingiwa iwe ni yenye maslahi kwa Taifa.
Vilevile, watoa huduma wawe ni kampuni zinazofahamika na zenye sifa stahiki na kuaminika.
“Bahati mbaya sana tatizo la ukame limetukuta tena wakati mipango mingi ya umeme imeanza lakini haijakamilika. Miaka miwili ijayo, hali itakuwa tofauti sana, kwani miradi hii na mingine kadhaa itakuwa imekamilika na kulihakikishia Taifa uhakika wa umeme,” alisema.
Alisema miradi hiyo ya umeme huchukua muda kukamilika. Mitambo huchukua muda kutengenezwa na ujenzi wa vituo pia. “Ingekuwa ni mitambo ya kununua tu dukani tungefanya hivyo na kulimaliza mara moja tatizo hili. Tena lingeisha zamani na wala sisi tusingelikuta,” alisema.
Akizungumzia chakula, Rais alisema hali ya upatikanaji wa chakula nchini katika maeneo mengi ni ya kuridhisha isipokuwa katika maeneo machache. Taarifa ya Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika, inaonesha kwamba kuna akiba ya kutosha ya chakula katika maghala ya Serikali, ya wafanyabiashara wakubwa na ya wakulima mashambani.
“Maghala ya Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula yana tani 216,012 za mahindi na mpunga, nafaka ambazo zinatuhakikishia kuwa upungufu wowote wa chakula tutaukabili bila matatizo. Kiasi hicho ndicho kikubwa kuliko chote kilichowahi kuhifadhiwa tangu hifadhi hiyo ianzishwe na shabaha yetu ni kufikia tani 400,000 mwaka 2015,” alisema.
Kuhusu waathirika wa mabomu, Rais alisema maiti wote 25 wameshazikwa kwa gharama ya Serikali kule ambako ndugu waliamua wakazikwe. Kwa ajili hiyo maiti 10 wamezikwa Dar es Salaam na wengineo mikoani kama ifuatavyo.
Mara walizikwa wanne, Pwani watatu, Tanga wawili, Lindi mmoja, Kagera mmoja, Kilimanjaro mmoja, Mbeya mmoja na Mtwara mmoja. Majeruhi wameendelea kupatiwa matibabu na huduma stahili.
Mpaka sasa alisema kuna majeruhi 36 ambao bado wamelazwa katika hospitali za Amana, Temeke na Muhimbili.
Watoto 857 waliopotezana na wazazi wao wameshaunganishwa na familia zao. Hata hivyo, 15 bado hawajatambuliwa na wazazi au walezi wao. Kwa sasa watoto hao wamepelekwa kwenye kituo cha kulelea watoto cha Kurasini.
Kuhusu nyumba zilizobomoka kutokana na milipuko hiyo ya Februari 16, Rais Kikwete alisema utekelezaji wa agizo la kutambua na kufanya tathmini ya nyumba zilizoharibiwa unaendelea kwa nia ya kuwafidia ipasavyo.
“Kwa upande wa fidia, tumeamua kuwa Serikali ibebe jukumu la kujenga upya nyumba hizo kwa mujibu wa kiwango cha uharibifu. Nimeagiza Jeshi la Kujenga Taifa lifanye kazi hiyo kupitia Shirika lake la Uchumi. Nimeamua hivyo ili kuhakikisha kuwa maisha ya ndugu zetu waliokumbwa na maafa haya, yanarejea kuwa ya kawaida mapema iwezekanavyo.
Hata hivyo, aliwasihi Watanzania kuwa na subira na kuacha tabia za kueneza uvumi kwenye vijiwe vya kahawa na kwenye vikao vya kinywaji, kuhusu chanzo cha milipuko hiyo.
“Wakati mwingine watu wanageuza dhana zao kuwa ndiyo ukweli na kupotosha au hata kuwatia watu hofu. Wataalamu wamekwishafika, ukweli wenyewe utajulikana baada ya muda si mrefu,” alisema
No comments:
Post a Comment