UMOJA wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), umetangaza kuunda kamati maalumu ili kufanya mageuzi ndani ya umoja huo na kumuunga mkono Mwenyekiti wa chama hicho Taifa, Rais Jakaya Kikwete kwa kujivua gamba na kubadili mtazamo na kukidhi matarajio ya
wengi.
Aidha, umesema utahakikisha viongozi wa chama hicho wanaotoa matamko bila kufuata utaratibu, hawapati nafasi yoyote ya uongozi na chama kisiwateue kugombea nafasi yoyote katika uchaguzi ujao.
Wamekitaka chama hicho kuwaelekeza viongozi wake umuhimu wa kuzingatia maadili na nidhamu kwa kutumia vikao kuwasilisha hoja zao na si kutumia matamko kukidhoofisha na kujijengea umaarufu binafsi.
Aidha, wameitaka CCM kufanya semina elekezi kwa mawaziri na wakuu wa mikoa na wilaya baada ya kuteuliwa ili watambue dhamana na uhusiano wao na chama hicho na malengo na matarajio ya chama kutoka kwa wananchi.
Akisoma maazimio ya kikao cha Baraza Kuu la UVCCM Taifa mjini Dodoma, Kaimu Mwenyekiti wa Umoja huo, Beno Malisa, mbali na kuunga mkono dhamira ya Mwenyekiti wa chama hicho, Rais Jakaya Kikwete ya kutaka CCM ijivue gamba, vijana hao walisema hata UVCCM inapaswa kujivua gamba.
Katika maazimio hayo, likiwemo la kumpongeza Rais Kikwete kwa kudhamiria kufanya mageuzi katika chama hicho kwa lengo la kukihuisha na kukirudishia mvuto kwa wanachama na wananchi hususani vijana, UVCCM wameona na umoja huo unahitaji kubadilika na kukidhi mahitaji hasa.
Malisa alifafanua kuwa kikao hicho kilichokutana Dodoma, kimeona kuwa umoja huo unahitaji kubadilika katika eneo la uanachama, uongozi, muundo, itikadi, uimarishaji wa uchumi, maadili na utendaji.
Ili kutekeleza dhamira hiyo ya kujivua gamba kama walivyosema, umoja huo umeunda kamati maalumu itakayofanya uchambuzi yakinifu wa namna ya kufanya mageuzi hayo chini ya uenyekiti wa kada wa umoja huo, Mohamed Bashe.
Baada ya kumaliza uchambuzi huo, kamati hiyo yenye wajumbe wengine sita, itawasilisha maoni na mapendekezo hayo katika vikao vya maamuzi, Baraza Kuu la UVCCM.
Wajumbe wengine wa kamati hiyo ni Riziki Pembe ambaye ni Mjumbe kutoka UVCCM Zanzibar, Fadhili Njagilo Mwenyekiti Vijana Iringa, Rojas Shemwele Mjumbe wa UVCCM Tanga, Daud Ismail kutoka UVCCM Zanzibar, Ashura Shengondo kutoka UVCCM Bara na Anthon Mavunde kutoka UVCCM Bara.
Mbali na kujivua gamba, Baraza hilo pia limelaani maandamano ya Chadema na walichoita kitendo cha viongozi wachovu wa Chadema kuendeleza chuki dhidi ya Serikali halali ya CCM.
Katika maazimio hayo, Baraza hilo limedai kubaini hila na njama zinapangwa dhidi ya Serikali na kuwataka vijana wote wa CCM na Watanzania kwa ujumla kukiogopa chama hicho cha Chadema.
Aidha, limewataka wanachama wote wa UVCCM kuwa tayari kukabiliana na njama hizo. Kuhusu tathimini ya uchaguzi uliopita, Baraza hilo limempongeza Rais Kikwete na Rais wa
Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein kwa kuchaguliwa kushika nafasi hizo, lakini limekishauri chama hicho kutazama upya mfumo wa kura za maoni wa kupata wagombea.
Mbali na mfumo huo, Baraza hilo pia limetaka chama hicho kitazame upya mfumo wa utoaji kadi za wanachama wakati wa uchaguzi wa wagombea na kuepuka makosa yaliyojitokeza katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010.
Kutokana na ushindi huo wa 2010, baraza hilo limeandaa mkakati wa kwenda kuwashukuru wananchi na vijana kwa kukipigia kura na limeagiza viongozi wote wa UVCCM kuhakikisha wanafanya mikutano na ikibidi maandamano ya kuwashukuru Watanzania kwa kukichagua CCM.
Baraza hilo pia lilijadili changamoto zinazojitokeza serikalini na zinazojitokeza kwa vijana na kutoa baadhi ya maagizo ya kufanyiwa kazi na Serikali.
Katika maagizo hayo, lipo la kutaka Serikali kuchunguza sababu za kupungua kwa ari ya baadhi ya watendaji wa Serikali katika kutimiza wajibu wao.
Hali waliyosema imeendelea kuwakatisha tamaa wananchi na hata wanaCCM na hivyo kujenga chuki dhidi ya Serikali halali ya CCM.
No comments:
Post a Comment