Thursday, March 17, 2011

Hali ya nchi tete



-Dk. Slaa:Watanzania hawahitaji kufundishwa ya Misri
-Asema kama si CHADEMA kuwapoza “hali ingelikuwa tayari”
-Azungumzia pia CCM inafadhiliwa kutoka nje


WAKATI Kanisa Katoliki likionyesha kukerwa na mwenendo wa Serikali katika kutumikia umma, Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) umejitosa kupooza joto la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kwa kuwavaa wazee ndani ya chama hicho tawala, Raia Mwema limebaini.

Uchunguzi wa Raia Mwema kwa wiki kadhaa sasa umebaini kwamba UVCCM imekuwa katika mikakati mizito ya kufanya mageuzi makubwa ndani ya CCM kivitendo kwa kufanya mambo ambayo yamekuwa yakifanywa na CHADEMA yakiwavuta vijana wengi.

“Vijana sasa wameamua kufanya siasa za ukombozi maana tumechoka kuchekwa na kuwafanya wananchi wapoteze imani na CCM kwa sababu tu haiwatetei. Vijana wa CCM nao wameamua ‘kufanya kweli’ kuwatetea wananchi bila kujali kama Serikali ni ya CCM.

“Kama tutakosea mahali basi kazi ya wazee itakuwa kutuombea radhi maana wao ndio wamechelewa kufanya siasa. Walijisahau sana na wengine badala ya kutetea wamekuwa wakitumaliza,” anasema mmoja wa watu wenye ushawishi mkubwa ndani ya UVCCM.

Tayari kuna habari kwamba mbali ya kutoa matamko mazito, UVCCM wanapanga kufanya maandamano nchi nzima huku baadhi wakipendekeza hata kuiteka Ofisi Ndogo ya CCM-Lumumba Dar es Salaam.

Taarifa zilizolifikia gazeti hili zinabainisha kuwa vijana wa CCM wamepanga ‘kuiteka’ ofisi ndogo ya CCM-Lumumba inayotumiwa na Makamu Mwenyekiti, Pius Msekwa; Katibu Mkuu, Yusuf Makamba; Naibu Katibu Mkuu, George Mkuchika; Katibu wa Uenezi, John Chiligati na Mweka Hazina Amos Makalla.

Ukimtoa Msekwa, wanaobaki katika orodha hii ni wajumbe wa sekretariati ambayo katika siku za karibuni imekuwa ikituhumiwa kwa kushindwa kuongoza vyema chama huku ikipendekezwa kwamba wajumbe wake hao wapime wenyewe kama bado wanahitajika katika nafasi walizonazo.

Inadaiwa kuwa vijana hao wamechoshwa na namna chama chao kinavyoendeshwa na kwamba sekretariati ya sasa ya chama hicho haina uwezo tena wa kukistawisha chama.

“Tunadhani muda unazidi kupotea kwa kuendelea kuicha sekretariati hii madarakani. Vijana wanajipanga kwenda kuwaondoa ofisini kwa nguvu,” alisema mmoja wa wajumbe wa Baraza la Utendaji la UVCCM.

Lakini wakati taarifa hizo za ‘mapinduzi’ zikivuja Katibu wa UVCCM, Martin Shigela, amekanusha kuwapo kwa mpango huo na akasisitiza kuwa huo si utaratibu wa CCM.

“Ndani ya CCM hatuna utaratibu wa kuteka ofisi. Isipokuwa kiongozi anaweza kujiondoa ofisini au katika madaraka aliyonayo kwa kujiuzulu au kuondolewa. Utaratibu wetu ni kwamba mtu anakabidhiwa madaraka kwa kuchaguliwa au kuteuliwa na si kuteka ofisi.

“Ni kweli vijana wameanza kutoa maoni ya kutoridhishwa na baadhi ya watendaji ndani ya chama ngazi ya Taifa. Lakini naamini wanajua taratibu za chama na moja ya taratibu hizo ni kutoa maoni yao kwenye vikao vyao kama walivyofanya,” alisema Shigela.

Katika hatua nyingine, vijana ndani ya CCM wamepanga kukutana mwishoni mwa wiki mjini Dodoma kupitia Baraza la Utendaji la Taifa, ambako watatoa tamko kuhusu mwenendo wa chama chao.

Kikao hicho cha UVCCM kinafanyika katika mazingira ya kuzidisha shinikizo dhidi ya sekretariati ya CCM kung’olewa na kukemea baadhi ya waliopata kuwa vigogo wa serikali ambao wanadaiwa kushambulia serikali.

Shigela, amelithibitishia gazeti hili kuwa kikao cha Baraza la Utendaji UVCCM Taifa kitafanyika mwishoni mwa wiki hii mjini Dodoma na kwamba maazimio yatatolewa kuhusu msimamo wa umoja huo.

Mkutano huo utafanyika ukiwa umetanguliwa na vikao vya UVCCM ngazi ya mkoa, na baadhi ya mikoa imetoa kauli zilizotikisa sekretariati ya CCM.

Hivi karibuni, mkoani Pwani, katika hali inayoonyesha kukosa uvumilivu, UVCCM mkoani humo ulikemea kauli zilizotolewa na baadhi ya wana CCM maarufu na pia udhaifu wa baadhi ya watendaji ambao umoja huo unaamini sasa wameshindwa kumshauri Mwenyekiti, Rais Jakaya Kikwete kustawisha chama hicho.

UVCCM mkoa wa Pwani, waliwataja kwa majina Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa na Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye, ambao kwa nyakati tofauti wamekuwa wakisaidia kukielekeza chama jinsi ya kukabiliana na mapigo ya CHADEMA.

Lowassa yeye alikwenda mbali zaidi kwa kuikosoa Serikali akitaka iongeze kima cha chini cha mishahara kutokana na kupanda kwa gharama za maisha, kauli ambayo vijana wameiona ina malengo ya kujikweza kisiasa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.

Akizungumzia hali hiyo, Katibu Shigela alilieleza gazeti hili kuwa vijana hao wanao uhuru wa kuzungumza na kutoa maoni kama ambavyo wamefanya na anasubiri taarifa yao rasmi.

“Kwa sasa nami nimepata taarifa hizo kupitia magazeti tu bado taarifa rasmi naisubiri kutoka kwa Katibu. Kwa kawaida, vikao kama hivyo vinapofanyika tunaandikiwa muhtasari ngazi ya Taifa,” alisema Shigela akizungumzia kauli ya vijana wa Pwani.

Aliunga mkono vijana wa chama hicho kushangazwa na waliopata kuwa viongozi wakuu wa serikali ambao sasa wanaishambulia Serikali iliyopo madarakani hata katika mambo ambayo alisema wakati wao walishindwa kuyatekeleza kwa ufanisi.

“Vijana pia wametoa maoni yao kuhusu mwenendo wa baadhi ya viongozi waliowahi kushika nafasi za juu serikalini hasa wanaokosoa kupitia vyombo vya habari wakati huo si utaratibu wa chama.

“Ni muhimu kwa viongozi hao wakatumia taratibu za chama kutoa maoni yao. Baadhi ni viongozi bado ndani ya chama hasa vikao nyeti kama Halmashauri Kuu ya Taifa, lakini ni kama hawajui tena kanuni za chama zinasemaje. Ni kweli kuna uhuru wa kutoa maoni, lakini ndani ya vikao,” anasema Shigela.


Wakati hayo yakiendelea ndani ya CCM, vyama vya NCCR-Mageuzi na CUF kupitia wenyeviti wa vyama hivyo, James Mbatia na Profesa Ibrahim Lipumba, wameanza wakiendesha mikutano ya hadhara wakishambulia mwenendo wa viongozi wa CHADEMA kuitisha maandamano na mikutano.

Kwa mujibu wa Mbatia na Lipumba, viongozi hao wa CHADEMA wamekuwa wakihimiza uvunjifu wa amani kwa lengo la kutaka kuing’oa madarakani Serikali iliyochaguliwa kidemokrasia.

Mikutano hiyo imekuwa ikifanyika kwa siku kadhaa sasa katika maeneo mbalimbali mkoani Kigoma. Katika mwelekeo huo, CUF na NCCR-Mageuzi ni kama vimeungana na CCM na Serikali katika kukikosoa CHADEMA.

Katika ziara hizo, Mbatia ambaye hana wadhifa serikalini ametembelea miradi na maeneo mbalimbali ikiwamo uwekezaji katika Shirika la Reli (TRL), alikotoa kauli ya kutaka kukarabatiwa kwa miundombinu.

Mbali na joto hilo la kisiasa, hali ya uhusiano kati ya dola na baadhi ya viongozi wa dini nchini si shwari huku baadhi ya viongozi wa dini wakianza kutoa kauli zinazoashiria kuandamwa na hata kuwapo kwa kusudio la kuuawa.

Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki, Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo ni kati ya viongozi walioweka bayana kuwa kuna baadhi ya viongozi wa Serikali hawafurahishwi na viongozi wa dini kuwaeleza ukweli wananchi kuhusu mustakabali wa nchi yao.

Kwa mujibu wa Kardinali Pengo, baadhi ya viongozi serikalini wamekuwa hodari kuficha uozo wanaowatendea wananchi kwa gharama yoyote.

Kiongozi huyo alitoa kauli hiyo wakati wa Misa ya kuwaombea watu waliopoteza maisha kwenye milipuko ya mwezi uliopita ya mabomu Gongolamboto, jijini Dar es Salaam.

Alitaja baadhi ya uozo unaofanywa na viongozi hao kuwa ni pamoja na ufisadi wa mali za umma, akitolea mfano utayari wa ghafla wa baadhi ya viongozi kutaka serikali ilipe bilioni 94 kwa Kampuni ya Dowans.

Kwa mujibu wa Pengo, hali ni mbaya kiasi cha baadhi ya watu kutenda maovu na kufunga midomo watu na baadhi ya vyombo vya habari kuzungumzia uovu huo. Alisisitiza kuwa viongozi hao mafisadi wako tayari kutoa uhai wa watu wanaodhani ni kikwazo kwao.

Pengo alisema Nabii Yeremia alitaka kuuliwa kwa sababu tu alitoa unabii ambao si mzuri kwa taifa lake.

“Viongozi wanapenda tu habari za kuwafurahisha wao na wapambe wao. Wanapenda kusikia tu mambo mazuri hata kama ni ya kipumbavu. Yeremia alivyowaambia ukweli walifanya kila liwezekanalo kumuu, mpaka wakaenda kumtupa kwenye kisima kilichokuwa na matope,” alieleza Kardinali Pengo na kuongeza:



“Mimi nimesema haya leo. Maisha yangu yapo mikononi mwenu, lakini kwa kuwa ni Mungu kanituma nitasema. Mkiniua leo au kesho sijali. Mkisikia, msiposikia shauri yenu.”

Alifafanua: “Mkiniuwa damu yangu iko mikononi mwenu, kwa sababu mtakuwa mmemwaga damu isiyokuwa na hatia. Nasema hivi si kuwa naropoka. Najua ninachokisema. Kwanini nifungwe mdomo? Nasema haya leo na nyie mkiwa hapa, kama kuna chombo kitakacho kuwa na ujasiri wa kuandika mtaona yatakayotokea.”

Wakati hayo yakiendelea, Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa, amerejea kutoka safari ya Monrovia, Liberia na kutoa kauli nzito kuhusu hali ya kisiasa akijibu shutuma zilizotolewa dhidi ya chama chake kufadhiliwa na mataifa ya nje.

Katika maelezo yake katika mtandao wa Jamiiforums.com na katika mahojiano maalumu na Raia Mwema jana, Dk. Slaa alisema kuihusisha CHADEMA na vurugu ni ufinyu wa fikra kutokana na chama chake kujitahidi kuwasihi wananchi watulie:

“Ni upofu kujifanya huoni hali tete ya Tanzania. Watanzania huhitaji kuwafundisha kuwa ‘kama Tunisia, Misri nk…. Wanaona kwa macho yao wenyewe. Watanzania saa hizi wako mbele kuliko sisi, na kama si kuwapoza sisi hali ingelikuwa tayari. Asiyetaka kuona hilo ni ‘kipofu’ bila sababu (siyo wasioona kuna tofauti ya msingi sana).

“Unahitaji tu (kuangalia) kwenye mikutano mabango yanayoandikwa. Nani kawafundisha.Wakati wa kufanya ‘mchezo wa bundi’ umeisha. Tuwe wakweli tutoke tunduni, tutaokoa Taifa letu. Taifa haliokolewi kwa kujenga hofu bali kwa kuondoa kero, kufanyia kazi kero za watu, kujibu hoja zilizoko kwa hoja. Mbinu za mwaka 47 hazina nafasi tena”.

Katika mahojiano maalumu na Raia Mwema muda mfupi baada ya kuwasili Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere, Dk. Slaa alizungumzia shutuma za CHADEMA kufadhiliwa na mataifa ya nje ikiwamo Ujerumani akisema kwamba vyama vyote kikiwamo CCM vinashirikiana na mashirika na vyama marafiki na hakuna usiri katika hilo.

“Kwa wale wasiofahamu, ni vema wakafahamu kuwa kama ambavyo CHADEMA inashirikiana na Konrad Adenauer Stiftung (Foundation) NGO ya Kijerumani yenye Itikadi ya Mrengo wa Centre- Right kama ilivyo CHADEMA, CCM ina ushirikiano kama huo huo na Friedrich Ebert Stiftung, ambayo kwa Dar es Salaam, Mkurugenzi Mwakilishi wake ni Dk.Stefan Chrobat, aliyeko Plot 397, barabara ya Kawawa,” alisema.

Dk. Slaa na Mwenyekiti wake, Freeman Mbowe walikuwa nchini Liberia kuhudhuria Mkutano wa Mwaka wa Democratic Union of Africa (DUA) ambayo hadi mwaka 2009 CHADEMA ilikuwa sekretarieti na NPP ya Ghana ilikuwa mwenyekiti. Mbowe alitoa mada katika mkutano huo.

No comments: