-Asema Katiba inawapa nguvu wananchi
-Wavuta watu Mwanza, Mara na Shinyanga
KATIBU Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Dk. Willibrod Slaa amemtaka Rais Jakaya Kikwete, kusoma alama za nyakati badala ya kulaumu wapinzani kwa mawimbi ya kisiasa nchini kwa vile mazingira ya sasa yanasukumwa na nguvu ya wananchi wanaotaka kupata maisha bora waliyoahidiwa.
Akizungumza na Raia Mwema kwa simu akiwa njiani kuelekea Maswa mkoani Shinyanga, jana Jumanne, Dk. Slaa alisema wimbi la mageuzi la sasa katika Tanzania na duniani halitokani na CHADEMA bali linasababishwa na wanasiasa walioshindwa kuusikiliza umma, kwamba Serikali na Chama cha Mapinduzi (CCM) vimewachosha wananchi na wao kama chama cha siasa kilichobaini mapungufu hayo, hawatasitisha vuguvugu la sasa.
Alisema Rais Kikwete ana haki ya kuwa na hofu kuhusu hali ya sasa lakini kwamba anapaswa kusikiliza kilio cha wananchi walio wengi kwani “ndiyo salama yake, vinginevyo hatakuwa salama”.
Akihutubia Watanzania kupitia vyombo vya habari Juzi Jumatatu, Rais Kikwete alielekeza lawama zake kwa CHADEMA kuwa ni chama kinachotaka kuleta vurugu nchini kwa nia ya kuiondoa Serikali halali madarakani kwa kuhamasisha wananchi nchi nzima wakati uchaguzi ukiwa umemalizika.
“Siyo sawa hata kidogo kuchochea ghasia ati kwa nia ya kuiondoa Serikali madarakani. Ni kinyume cha Katiba na ni kuiingiza nchi katika mgogoro usiokuwa wa lazima. Tutasababisha umwagaji wa damu, watu kupoteza maisha na mali zao kuharibiwa bila sababu yoyote ya msingi,” alisema Kikwete katika sehemu ya hotuba yake hiyo.
“Nadhani Bwana Mkubwa (Rais Kikwete) kateleza juu ya Katiba aliyoapa kuilinda na kuitetea. Anaanza kusema kwamba uchaguzi umeisha na CHADEMA inafanya vurugu; anasahau uchaguzi mmoja ukiisha unaanza mwingine na kazi yetu si kumpigia makofi tu bali kazi yetu ni kuikosoa Serikali.
“Nadhani anajenga hofu, ambayo ni hofu ya hakika na ni halali kwa sababu ya udhaifu wa Serikali yake na udhaifu wa wanaomshauri. Sisi CHADEMA hatuna namna ya kumsaidia. Serikali imara ni ile ambayo haihitaji kunyooshewa vidole bali inachukua hatua kwa kila jambo linalohusu maslahi ya watu wake,” anasema Dk. Slaa.
Dk. Slaa ambaye alikuwa mgombea Urais mwaka 2010, katika uchaguzi ambao Kikwete aliibuka mshindi, anasema Serikali ijue kwamba mwisho wa uchaguzi mmoja ni mwanzo wa mwingine na kwamba hiyo ndiyo kazi inayofanywa na CHADEMA sasa nchi nzima.
“Kikwete anaona tunasababisha vurugu, lakini walipokuwa wakichezea uchaguzi hawakugundua kwamba wanaanzisha vurugu? Hawakujua ndiyo matokeo yake? Akumbuke sisi hakuna mwenye uchu wa madaraka wala kukimbilia Ikulu na ajue tokea zamani hatujaikimbilia Ikulu ila ajue maisha ya umma wa Watanzania ndiyo yanatusukuma tuwafuate wananchi na kuwasikiliza.
“Wananchi wale hakuna anayebebwa na magari, hakuna maduka yanayolazimishwa kufungwa wala hakuna polisi wanaowafukuza mitaani wahudhurie mikutano yetu, bali wanatufuata kwa mapenzi yao na kwa kuchoshwa na Serikali yao. Akitaka asikilize kilio cha wananchi kwa kutekeleza matakwa yao,” anasema Dk. Slaa.
Akitoa mfano wa hatua zilizochukuliwa na Serikali baada ya kuanza kwa maandamano, Dk. Slaa amesema Serikali imechukua hatua ya kudhibiti bei ya sukari baada ya CHADEMA kutoa siku tisa kwa Serikali, wakati ilishindwa kufanya hivyo wakati wabunge walipolipigia kelele suala hilo ndani ya Bunge.
“Kama bungeni hawakusikiliza kuhusu sukari, tumempa siku tisa amesikiliza. Ajue hakuna mwenye nia ya kumuondoa ila ajue akishindwa hatuna ndoa yoyote na yeye wala CCM. Kama atashindwa kuondolewa kwa kura na kama akichakachua tena ataondolewa kwa nguvu ya umma uliochoka,” alisema Slaa ambaye alikuwa wa pili baada ya Kikwete katika uchaguzi uliomalizika Oktoba mwaka jana.
Akizungumzia hali ya maisha inayowasukuma wananchi kuichukia serikali, Dk. Slaa amesema; “Bei za bidhaa zimepanda kwa kasi zaidi, hatuwezi kufumba macho, hatuwezi kusuburi… Tunasema kwa miaka mitano iliyopita watawala watuambie wamejenga majumba mangapi wao na familia zao. Wamepata wapi ukwasi wote huo katika dimbwi la umasikini wa Watanzania?”
Anasema kwa zaidi ya miaka mitano ni suala moja tu ambalo serikali imelifanyia kazi nusu nusu na kuacha mambo mengine mengi yakielea bila kufanyiwa kazi.
“Wamezima sakata la ufisadi wa Meremeta, Kagoda na EPA, tena tuliyazungumza bungeni; Suala la EPA ameonyesha kidogo lakini hakuna alichofanya na badala yake serikali imeapa bungeni kwmaba haitajibu suala la Meremeta.
“Sasa yeye anatuambia turudi bungeni akijua wao wako wengi na watamtumia Spika kuzima hoja zetu, tunakataa na tunaamua kutumia Ibara ya 8 (a) ya Katiba ambayo inatoa mamlaka ya juu kwa wananchi ambao ndio wanaoliweka Bunge na serikali,” anasema.
Ibara ya 8 (a) ya Katiba inasema, “Wananchi ndio msingi wa mamlaka yote, na Serikali itapata madaraka na mamlaka yake kutoka kwa wananchi kwa mujibu wa katiba hii.”
CHADEMA wameanza kampeni kali wakianzia na mikoa ya kanda ya Ziwa ya Mwanza, Mara na Shinyanga, kampeni ambazo zimepata mwitikio mkubwa kutoka kwa wananchi, hali inayotishia watawala akiwamo Rais Kikwete aliyejikuta akishindwa kujizuia kuonyesha hofu yake katika hotuba yake ya Juzi Jumatatu.
Akizungumza na jarida la mtandao la FikraPevu, Dk. Slaa alisema maandamano na mikutano ambayo chama hicho kimefanya na kinaendelea kufanya ni mwanzo tu wa shinikizo la umma dhidi ya Serikali ya Rais Kikwete kuitaka serikali hiyo kuchukua hatua mara moja na kali dhidi ya ufisadi, mfumuko wa bei, na kuweka ratiba wazi ya mchakato utakaohakikisha kuwa uchaguzi mkuu ujao wa 2015 unafanyika chini ya Katiba mpya.
Dk. Slaa amesema kuwa chama chake kimefikia uamuzi wa kutumia nguvu ya umma kuongeza shinikizo hilo hasa baada ya kuona kuwa serikali ya CCM haichukulii kwa uzito unaostahili madai na malalamiko ya wananchi.
Akijibu swali ya kwanini wanafanya maandamano hayo sasa badala ya kusubiri uchaguzi mkuu ujao kwani nchi imetoka tu kwenye uchaguzi mwingine Dk. Slaa alisema kuwa “uchaguzi siyo mwisho; mwisho wa uchaguzi mmoja ni mwanzo wa maandalizi ya mwingine na shughuli za kisiasa hazikomi kwa sababu uchaguzi umefanyika.”
Kiongozi huyo wa CHADEMA ambaye katika ziara hizi za maandamano ameungana na Mwenyekiti wa Chama hicho na Mbunge wa Hai, Freeman Mbowe pamoja na baadhi ya wabunge, amesema kuwa hoja ambazo wanazijenga sasa hivi zinahitaji maamuzi ya haraka.
Dk. Slaa alizungumzia pia suala la malipo ya Dowans na kwanini chama chake kimechukua msimamo wa kutaka majenereta ya kampuni hiyo yakamatwe mara moja. “Hili linaendana na ukweli kuwa suala la Dowans limefungamana na kuingia kwa kampuni ya Richmond nchini na vile vile hoja nzima ya jinsi gani kampuni ya Dowans iliweza kuchukua kiulaghai mkataba wa Richmond na TANESCO”. Dk. Slaa alisema pia kuwa “serikali ina jukumu la kukamata mitambo hiyo na hakuna sababu ya kuilipa kampuni hiyo”
Akifafanua kama itakuwa vizuri kukamata mitambo hiyo wakati kuna tozo iliyotolewa na Mahakama ya Usuluhishi wa kibiashara Dk. Slaa alisema kuwa “kwa vile Dowans ilitumia ulaghai kushinda kesi hiyo serikali haitakiwi kufungwa na hukumu hiyo”. “Ni bora kuzuia malipo hayo sasa badala ya kusubiri miezi sita au saba baadaye ndipo tuje kugundua tumefanya makosa kuwalipa. Fedha hizo zingeweza kutumiwa katika kuboresha maisha ya watu wetu, wanafunzi, wafanyakazi na wakulima wa nchi yetu”.
Vile vile, Dk. Slaa alizungumzia suala la haraka ya kuwasha mitambo ya Dowans hata ikibidi kwa mkataba wa muda mfupi kama inavyopendekezwa na baadhia ya watu ili kupunguza ukali wa tatizo la ukosefu wa nishati kwa maisha ya watu na shughuli mbalimbali za uzalishaji mali. Dk. Slaa hata hivyo alitupilia mbali pendekezo hilo.
“Ni lazima kuelewa kwanza maudhui ya mambo yanayoendelea kabla ya kufikia hitimisho hilo. Tayari nchi inapoteza kiasi kikubwa cha fedha kwa kulipia gharama ya kutumia mitambo ya IPTL. Serikali ilishauriwa karibu miaka mitano iliyopita inunue moja kwa moja mitambo ya IPTL lakini haikufanya hivyo. Mwaka 2007 serikali iliambiwa kuwa mitambo ipo na kuwa ifanye ununuzi wa kimataifa lakini serikali haikufanya lolote vile vile.”
Dr. Slaa aliendelea kusema kuwa “tunaamini kabisa kuwa juhudi za kutaka mitambo ya Dowans iwashwe na mkataba mwingine uingie ni sehemu ya ufisadi ule ule unaondelea nchini. Tukumbuke kuwa mwezi wa Machi umeshafika na ndio kipindi cha kuanza kwa mvua za masika nchini na hivyo ni wazi baada ya muda si mrefu mabwawa yetu ya kufua umeme yatakuwa yamejaa maji. Sasa kwanini tuingie mkataba wakati huu?” aliendelea “tukumbuke pia kuwa wakati majenereta haya hatimaye yanaanza kufanya kazi mwezi Machi mwaka 2007 mvua zilikuwa zimeanza na mabwawa yalikuwa yamejaa maji lakini tulikuwa tumefungwa na mkataba. Fedha ambazo tungetumia kuingia mkataba na Dowans wakati huu zingeweza kabisa kutumika kununua mitambo mipya tena ya kwetu bila ya kuja kulazimika kulipia gharama ya matumizi ya mitambo hiyo”.
Ameendelea kwa kusema “tayari nchi inapoteza umeme sasa hivi, ni bora basi kupoteza umeme huo kwa wiki mbili zijazo na kupata suluhisho la kudumu kuliko kujiingiza katika mkataba mwingine utakaotugharimu kwa muda mrefu ujao.”
Akizungumzia suala la Katiba Mpya Dk. Slaa alisema kuwa chama chake kiliandika katika ilani yake ya uchaguzi suala la Katiba mpya na kiliweka ahadi ya kuwa uchaguzi ujao ungefanyika chini ya Katiba mpya endapo chama hicho kingeshika madaraka. “Sasa kwa vile serikali imekubali kimsingi suala la Katiba Mpya hakuna jinsi nyingine isipokuwa kuhakikisha kuwa kunakuwepo na Katiba mpya ambayo itaweka vyombo na taratibu ambazo zitazuia kabisa uwezekano wa kutokea machafuko na umwagikaji damu nchini”.
Dk. Slaa alizungumzia hekima na umakini mkubwa uliotumika kuzuia munkari wa vijana wengi baada ya uchaguzi ambao walikuwa wanataka kuingia mitaani kupinga kile ambacho waliamini kuwa kilikuwa ni uchakachuaji wa matokeo ya uchaguzi yaliyompatia ushindi hafifu Rais Kikwete kulinganisha na ushindi wake wa 2005. “Watu walikuwa wanasubiri kabisa wasikie nitasema nini, lakini sikuwa tayari kusukumiza watu katika kudai kwa nguvu haki yao. Sasa kama hatukufanya hivyo wakati ule hatuna sababu ya kutumia nguvu sasa hivi” alisema Dk. Slaa.
Akizungumzia kile ambacho serikali inaonekana kukihofisa sasa hivi hasa baada ya matukio ya Misri na Tunisia ambapo viongozi wa muda mrefu wa nchi hizo walijikuta wanaondolewa madarakani kwa nguvu za umma Dk. Slaa alisema kuwa wakati wowote wananchi wanaona kuwa haki zao zinapuuzwa wanaweza kujikuta wanalazimika kuzidai kwa nguvu.
“Kile kilichotokea Misri ndicho kilichotokea Arusha vile vile, na ndicho kilichotokea Geita na sehemu nyingine nchini mara baada ya uchaguzi mwaka jana na katika maeneo mbalimbali wananchi walikuwa tayari kwenda kudai haki zao na kama siyo hekima tuliyotumia kwa kweli hali ingekuwa mbaya kwani hata watu waliotaka tuitishe maandamano makubwa tuliwakatalia kwa sababu hatukuwa tayari kufanya hivyo wakati huo”.
Dk. Slaa alisema kuwa “ili kuepusha yanayotokea huko Libya, Misri, Tunisia, Bahrain, Yemeni na nchi nyingine za Kiarabu ni lazima serikali na chama tawala wasikilize kilio cha wananchi na mara moja waanze kutenda kufuatana na madai tunayoyatoa kwani hatutoi madai ya kibinafsi bali madai ambayo ni maslahi ya taifa. Sisi sote ni wadau katika maslahi ya taifa hili; tunataka kuona amani na utulivu lakini wakati huo huo hatuwezi kuwaacha watu wachache waendelee kuliharibu taifa letu”.
Pamoja na hayo Dk. Slaa amesema kuwa wamejaribu mara kadhaa kuanzisha mawasiliano na serikali ya Kikwete ili kusaidia kutoa ufumbuzi wa masuala mbalimbali yanayoendelea nchini.
Dk. Slaa na timu nzima ya viongozi wa CHADEMA wameendelea na maandamano na mikutano huko Shinyanga na baadaye wanaendelea na mikutano hiyo huko Kagera kabla ya kurudi Dar-es-Salaam kwa mapumziko mafupi siku chache zijazo.
Chanzo: Raia Mwema
No comments:
Post a Comment