WANASIASA na taasisi mbalimbali nchini wamepinga maandamano yanayoendeshwa na Chadema kuhamasisha wananchi kuipinga Serikali na kuiondoa madarakani kuwa ni uhaini na inapaswa kushitakiwa.
Aidha, wamemtaka Msajili wa Vyama vya Siasa, kuangalia uwezekano wa kukisimamisha au kukifuta chama hicho kwa usalama wa Taifa na kudai kuwa maandamano hayo ni chanzo cha vurugu na kuvunjika kwa amani, ambazo ni dalili zinazopaswa kuchukuliwa hatua za kiusalama haraka ili Taifa lisiingie katika machafuko ya kisiasa.
Katika siku za karibuni Chadema imekuwa ikifanya maandamano na mikutano ya hadhara kwa lengo la kupinga ufisadi serikalini, hali ngumu ya maisha inayotokana na kupanda kwa bei ya vyakula, malipo kwa Kampuni ya Dowans na tatizo la umeme.
Wakizungumza na wanahabari Dar es Salaam jana, Wanaharakati wa Haki za Watu Wenye Ulemavu nchini, walisema kinachofanywa hivi sasa na vyama vya siasa na wanasiasa kuzunguka nchini kuhamasisha wananchi wakubali kuondoa Serikali halali madarakani, kinaweza kusababisha madhara makubwa.
Walipongeza hotuba ya Rais Jakaya Kikwete aliyoitoa wiki iliyopita na kupinga maandamano yanayoendelea katika mikoa tofauti na kusema madhara hayo waathirika wake ni jamii ya watu wenye ulemavu.
Msemaji wa wanaharakati hao, Abubakar Rakesh, alisema wanampongeza Rais kwa kuona kwamba amani ya Watanzania ambayo ni tunu inaanza kutoweka kwa kusema kwake na kuwaondoa hofu Watanzania, imeonesha jinsi anavyowajali wananchi wake.
“Uzoefu na ushahidi unatuonesha, kwamba nchi nyingi duniani zilizokabiliwa na migogoro na uvunjifu wa amani, wahanga wakubwa wa kupoteza maisha ni watu wa jamii ya walemavu, hivyo tunamwomba Rais aendelee kukemea lakini pia asiyumbe katika kulinda amani ya nchi yetu,“ alisema Rakesh.
Walimtaka Rais Kikwete pamoja na kuendelea kukemea hali hiyo, lakini pia asiyumbe katika kulinda amani ya nchi na kuhakikisha kuwa Katiba iliyopo inaheshimiwa na kila mmoja, kwani Katiba ya nchi si ya chama.
Katibu wa Kamati ya Amani Umoja na Mshikamano wa Kitaifa (UPF), Risasi Mwaulanga, alisema wanachofanya Chadema ni uhaini wa wazi, kwani umma utakapokasirika utapata hamasa na kugomea sera ya chama tawala na kuacha kushiriki shughuli za maendeleo.
“Vyombo vya usalama vinatakiwa kuchukua hatua dhidi ya Mwenyekiti wa Chadema na Katibu Mkuu wake wakamatwe na kufunguliwa mashitaka ya uhaini, ikiwa ni pamoja na Bunge kutoa onyo kwa wabunge wake na Msajili kuangalia vifungu vya Katiba kuona uwezekano wa kukisimamisha au kukifuta chama hicho,” alisema Mwaulanga.
Pia aliwataka wananchi kupuuza mikutano yao ya hadhara bila kujali itikadi, kujenga ushawishi wa kutengwa na taasisi mbalimbali hadi watakaporekebisha mustakabali wa siasa zao za uchochezi nchini .
Mwenyekiti wa TLP, Augustino Mrema, alisema maandamano hayo yanahamasisha wananchi kuiga mifano ya nchi za Kaskazini mwa Afrika, ambazo chanzo cha maandamano na hatimaye vifo yametokana na vyama vya upinzani.
“Maandamano hayawezi kutuondolea matatizo tuliyonayo, bali yatasababisha maafa makubwa yasiyoweza kulipika, kama ilivyotokea kwenye nchi nyingine duniani, ni wazi tunaweza kuiondoa Serikali iliyoko madarakani kwa kutumia njia za kikatiba na kisheria kwa ridhaa ya wananchi kwa kura zao,” alisema Mrema.
Aliwasihi wapinzani wenzake kuwa kwa kutumia njia sahihi wana uwezo wa kuingia madarakani, ndiyo maana walipata asilimia 40 ya kura za urais na wana wabunge na madiwani.
“Wapinzani tuko bungeni, kwenye halmashauri za miji, serikali za vijiji na vitongoji, kwa nini tusitumie fursa hizo? Baada ya uchaguzi siasa zihamie bungeni na kwenye mabaraza ya halmashauri na miji na si kuishia maandamano na mikutano tu,” alisema Mrema.
Alisema wapinzani wana wenyeviti katika kamati mbalimbali za Bunge, hivyo wanaweza kupambana na ufisadi na wakishindwa ni uzembe wao, kwani hawana kikwazo, aliwataka kukamata mafisadi na kuwapeleka kwenye vyombo vya sheria kwani ufisadi hauwezi kuondolewa kwa maandamano.
“Kwa mfano mimi nilishakabidhiwa vitabu vya ukaguzi kutoka kwa Mkaguzi Mkuu wa Serikali vinavyoonesha kwenye halmashauri za miji kuna ubadhirifu wa kutisha, kuliko hata ubadhirifu unaodaiwa kufanywa na Dowans,” alisisitiza Mrema.
Aliwataka Watanzania wasidanganywe na kufananisha Tanzania na nchi nyingine kama Libya na Misri, kwani matatizo hayafanani na nchini tatizo ni umasikini, hali ngumu ya maisha, umeme na ufisadi, wakati nchi hizo zingine, matatizo yao ni mfumo mbaya wa kiutawala tofauti Tanzania.
No comments:
Post a Comment