RAIS Jakaya Kikwete ameitaka Wizara ya Ujenzi, kutotumia ubabe katika ubomoaji wa nyumba za wananchi kwenye hifadhi ya barabara, iweke mbele maslahi ya wananchi hao.
Ameagiza Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, iandae taarifa na kutangaza maeneo yote ya wazi nchi nzima, ili iwaondoe kirahisi waliovamia maeneo hayo.
Ametoa maagizo hayo jana alipofanya ziara katika Wizara hizo kwa nyakati tofauti, na kusisitiza kuwa ubabe na haraka viepukwe katika ubomoaji nyumba za wananchi zilizopo katika hifadhi ya barabara.
“Undeni tume ya kuchunguza kwanza historia ya barabara ndipo mtoe amri ya kubomoa nyumba za wananchi na suala la fidia lazima lizingatiwe,” alisema Rais Kikwete.
Alisema, barabara nyingi zinazojengwa, kihistoria zilikuwa za asili na wananchi wengi walijenga kabla ya kupandishwa hadhi, hivyo si haki kuwabomolea bila kuwalipa fidia au kuwapa muda wa kubomoa wenyewe.
“Jamani hawa ni wananchi ambao wengi ni wanyonge, chochote mtakachowafanyia wao hawana pa kukimbilia, lakini ninyi mna uwezo wa kutotumia ubabe katika suala hili, ingawa mnafuata sheria,” alisema Rais Kikwete.
Aliiasa Wizara ya Ujenzi kutotafuta unafuu kwa kuwatupia mzigo wanyonge na badala yake izingatie zaidi haki za wananchi.
“Huwezi kumpa mtu saa 48 abomoe nyumba yake hata kama yuko kwenye hifadhi ya barabara, naomba katika ile miradi ambayo inachukua muda kuanza, basi wapeni muda angalau hata wa miaka miwili.”
Alisema, wananchi wengi wamejenga katika maeneo hayo miaka mingi iliyopita, wamezaa na watoto wao wamezaa na kuwa na vitukuu, hivyo si haki leo kuwaondoa bila fidia au kuwapa muda mfupi wa kuondoka wakati barabara husika imewafuata.
Aidha, aliitaka Wizara hiyo kuangalia maeneo ya kuwabomolea wananchi nyumba zao na kupitisha barabara, kwani si maeneo yote yanayopaswa wananchi kuondolewa ili kupisha barabara, akitolea mfano wa maeneo ya milimani kuwa ardhi yake ni ndogo na hata wananchi wakiondolewa barabara husika huenda isiwe na maana.
Kauli ya Rais inaonekana kuiunga mkono ile ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda aliyoitoa siku za karibuni akizuia kasi ya bomoabomoa iliyokuwa inatekelezwa na Waziri Magufuli kwa mujibu wa sheria.
Uamuzi wa Pinda ulizusha malalamiko miongoni mwa wananchi hata kufikia hatua ya kuvumisha kuwa Waziri Magufuli amejiuzulu wadhifa wake kutokana na kitendo hicho, lakini Wizara yake ikakanusha siku moja baada ya uvumi huo kuripotiwa magazetini.
Rais Kikwete jana pia alihimiza wizara hiyo na Mfuko wa Fedha za Barabara kuwa mstari wa mbele kukagua ujenzi wa barabara pale unapokamilika na si kutegemea zaidi taarifa za vitabu ambazo mara nyingi huandikwa vizuri kuliko uhalisia.
Alikiri kuwa, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) hukagua matumizi ya fedha za miradi, lakini kwa kupitia vitabu na kwamba hali halisi ya barabara husika huwa haiangaliwi, jambo linalosababishwa kuwapo kwa barabara nyingi zisizo na kiwango kinachotakiwa cha kudumu kwa muda wa miaka 15.
“Sitaki tujenge barabara ambazo baada ya miaka mitatu zinabanduka, watu watasema tunaiba, tafuteni wakandarasi na wasimamizi wazuri, msiwe walegevu wala kujivua hili.
“Kagueni barabara, ndiyo maana wakati mwingine msingi unachimbwa, nyumba inajengwa na watu wanahamia kwenye hifadhi ya barabara na ninyi mnapita tu bila taarifa,” alisema.
Alitolea mfano barabara ya Kilwa kuwa imekuwa ikilalamikiwa na wananchi kuhusu ubora wake, jambo ambalo ni aibu kwa kuwa barabara hiyo iko ndani ya Jiji la Dar es Salaam, ambako wizara na wahandisi wote wapo.
Kuhusu msongamano, alisema, mradi wa mabasi yaendayo kasi utamaliza hali hiyo kwa muda na suluhisho pekee ni kubuni usafiri wa kisasa unaoendana na uwezo wa nchi, akitolea mfano wa matumizi ya reli kwa wakazi wa Kimara, Ubungo hadi katikati ya Jiji - Stesheni.
Kuhusu suala la ardhi, aliitaka Wizara ya Ardhi, kuondoa taswira mbaya ya kukosa uaminifu na kupenda rushwa waliyonayo baadhi ya maofisa wa ardhi kwa wananchi ambapo pia aliwasisitizia maofisa hao kujali zaidi taaluma yao badala ya kujineemesha.
“Haya mambo yanasikitisha, watu wanaweka mbele maslahi yao na kusahau kabisa taaluma yao, sisemi hili kwa kuambiwa, mimi mwenyewe nina mifano halisi iliyonitokea, hata migogoro mingi ya ardhi ukifuatilia chanzo ni hawa maofisa ardhi … wakati mwingine nalazimika hata kuweka saini yangu hadi nihakikishe ukweli wa hati husika,” alisema Rais Kikwete.
Alitoa changamoto kwa wizara hiyo kupitia miradi yake ya kuendeleza miji ya Kigamboni na Kawe, kutowaweka pembeni wenyeji wa maeneo hayo miradi itakapokamilika na badala yake kuwapa kipaumbele kwa kuwarejesha ili kuwalipa fadhila.
Pia alitoa changamoto kwa Shirika la Taifa la Nyumba (NHC), kujenga nyumba ambazo wananchi watamudu gharama kwa kuwa lengo la kuanzishwa kwa shirika hilo ni kusaidia wananchi wenye kipato cha chini na si matajiri.
Waziri wa Ujenzi, John Magufuli, wakati akiwasilisha taarifa yake kwa Rais, alitaja miradi ya barabara ambayo ipo katika hatua ya utekelezaji ukiwamo wa magari yaendayo kasi na kwamba kwa sasa kinachokwamisha ni ubomoaji wa nyumba za wananchi walio ndani ya eneo la mradi.
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, alisema wizara yake ina mpango wa kutumia ramani ya zamani katika kutambua maeneo ya wazi nchini na kuonya hata walioko kwenye maeneo hayo wakiwa na hati halali hazitawasaidia.
No comments:
Post a Comment