MASHIRIKA sita yasiyo ya Serikali yamefungua shauri la kikatiba Mahakama Kuu kutaka ibatilishe Sheria ya Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo, kwa yanachodai kuwa inapingana na Katiba ya nchi.
Katika madai hayo dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali yanayohoji uhalali wa kikatiba wa Sheria hiyo namba 16 ya mwaka 2009, mashirika hayo yanadai kwamba ina athari kutokana na kudhoofisha majukumu ya wabunge na kukinzana na dhana ya kikatiba ya mgawanyo wa madaraka.
Mashirika husika ni Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), The Leadership Forum, Ulanga West Development Organisation, Haki Development Organisation, Uchungu wa Mwana na Mtandao wa Policy Forum.
“Tunapenda kusisitiza kuwa japo Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo unaweza kuonekana kama jambo zuri, tumebaini kuwa utekelezaji na usimamiaji wa Mfuko huo utakuwa na kasoro nyingi na hasa nafasi wanayopewa wabunge kuwa wasimamizi wake wakuu,” alisema Israel Ilunda wa Policy Forum.
Ilunda ambaye alisoma taarifa ya mashirika hayo jana Dar es Salaam kabla ya kwenda Mahakama Kuu kuwasilisha shauri lao, alisema sheria hiyo ikiendelea kutumika, itadhoofisha nguvu ya wabunge bungeni katika kuisimamia Serikali.
Alifafanua: “Na endapo wabunge watajiingiza katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo wenyewe badala ya kuziachia Serikali na halmashauri za wilaya, watakuwa wamedhoofisha uhuru na nguvu yao ya kuihoji Serikali kwenye masuala ya utekelezaji wa bajeti.”
Pamoja na kufungua shauri hilo, mashirika hayo yameishauri Serikali iwawezeshe wabunge kutekeleza wajibu wao kwa kuhakikisha wanapata ofisi majimboni, wanaboresha mfumo wa mawasiliano kati ya wabunge na wananchi majimboni na iwezeshe kila mbunge kuwa na wasaidizi rasmi wanaoweza kufanya utafiti, kufuatilia masuala na kutekeleza majukumu yao.
Sheria ya Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo ilitungwa Julai mwaka juzi na kusainiwa na Rais, Agosti 21 mwaka huo kwa lengo la kuchochea maendeleo jimboni.
Hata hivyo, tangu sheria hiyo ilipokuwa kwenye mchakato wa kutungwa, wanaharakati waliipinga wakidai inakiuka Ibara za 63 na 64 za Katiba zinazobainisha kazi za wabunge. Pia wanadai inapingana na Ibara ya 4 ya Katiba kuhusu mgawanyo wa madaraka.
No comments:
Post a Comment