WIZARA ya Fedha imetaja vipaumbele 12 katika Bajeti ijayo ya Serikali ya mwaka ujao wa fedha inayokadiriwa kufikia Sh. trilioni 11.9.
Wabunge wameitaka Serikali ivipungeze hadi vitano ili vitekelezwe kwa ufanisi kulingana na hali ya uchumi wa Taifa.
Vipaumbele hivyo kwa mujibu wa Waziri wa Fedha, Mustafa Mkulo, ni elimu, kilimo, nishati, miundombinu, viwanda, afya, maji, ardhi, raslimaliwatu, sayansi na teknolojia, huduma za fedha na masuala mtambuka.
Akizungumza Dar es Salaam jana na wabunge, Waziri Mkulo alisema makadirio ya awali ya mapato katika mwaka ujao wa fedha ni Sh. trilioni 12 ikilinganishwa na matarajio ya Sh. bilioni 11.1 mwaka huu wa fedha na zinatokana na mapato ya ndani, mapato ya Serikali za mitaa, mikopo na misaada ya wahisani.
Wabunge wengi waliochangia hotuba hiyo ya Mkulo, walisema hali ya uchumi hairuhusu kutekelezwa kwa vipaumbele vyote hivyo na badala yake wakataka vipunguzwe hadi vitano au sita ambavyo ni elimu, nishati, miundombinu, kilimo, afya na maji.
Wabunge hao pia waliitaka Serikali ichukue hatua za haraka kupunguza mfumuko wa bei ambao waliuelezea kuwa umewafanya wananchi waishi maisha ya shida kutokana na gharama kupanda kila siku.
Mbunge wa Bariadi Mashariki, Andrew Chenge (CCM), alisema amekuwa serikalini kwa muda mrefu, na anajua ujanja wa watumishi kujiwekea vipaumbele vingi kama njia ya kujitengenezea mambo yao.
“Vipaumbele vikiwa vichache na kutengewa fedha za kutosha, uchumi wa nchi utasonga mbele, la sivyo itakuwa kama kawaida … hayo mengine msiyaendekeze, najua kwa nini wanayasukumia humo,” alisema Chenge.
Mbunge wa Ilala, Musa Azzan Zungu (CCM) alisema, tatizo la Tanzania si mipango bali ni utekelezaji. Na tatizo hilo linatokana na watumishi wengi kutanguliza ubinafsi, roho mbaya na kutochukua uamuzi matokeo yake uchumi wa nchi haupigi hatua.
“Hapa tunaletewa mipango mingi na mizuri, lakini hakuna mkakati wa utekelezaji,” alisema Zungu na kutoa mfano kuwa Kilimo Kwanza licha ya kuwa ni kipaumbele cha Serikali, hakuna mipango ya uzalishaji mazao unaoonekana.
“Leo hii Kilimo Kwanza kimekuwa ni Power Tiller (matrekta madogo) kwa sababu tu ni mipango ya watu na ndiyo maana inapigiwa debe kila kona … usishangae hata Muhimbili tukaambiwa wanapelekewa Power Tiller,” alisema Zungu na kusababisha kicheko kutoka kwa wabunge.
Mbunge wa Magu, Festus Limbu (CCM), alipendekeza kuwepo bajeti ya miaka miwili itakayotumika kurekebisha matatizo ya kiuchumi na vipaumbele vya Taifa vianze kutekelezwa baada ya bajeti hiyo ya miaka miwili.
Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugora (CCM), aliponda Mpango wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umasikini (Mkukuta) kwa madai kwamba umeshindwa kupunguza umasikini miongoni mwa wananchi, lakini pia umeshindwa kukuza uchumi wa Taifa.
Mbunge wa Mbozi Mashariki, Godfrey Zambi (CCM), aliunga mkono kupunguzwa kwa vipaumbele, lakini akaitaka Wizara kuhakikisha vipaumbele vyake vinafanana na ahadi za Rais Jakaya Kikwete ambazo alizitoa wakati akiomba kura za Watanzania.
Kuhusu mfumuko wa bei, Mbunge wa Viti Maalumu, Leticia Nyerere (Chadema), alisema bei za vyakula ziko juu na akataka Serikali ieleze mkakati wake wa kukomesha mfumuko huo, kwa sababu hawana uwezo tena wa kununua.
Mbunge wa Kigoma Mjini, Peter Serukamba (CCM), alihoji iweje takwimu za Serikali zinaonesha mfumuko mdogo wa bei, asilimia 5.6 Desemba mwaka jana, wakati gharama za maisha zinazidi kuongezeka kila kukicha. “Wachumi twambieni ukweli nasi tuwaambie wananchi, kuwa hali ya uchumi ni mbaya.”
Wabunge wengine pia walihoji kuongezeka kwa deni la Taifa kutoka dola milioni 9.3 za Marekani hadi dola milioni 11 sawa na asilimia 18, lakini Waziri Mkulo alisema deni hilo linahimilika.
Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema), alitaka kujua sababu ya Tanzania iliyokuwa kwenye Mpango wa Kupunguziwa Madeni kwa Nchi Masikini (HIPC) deni lake lizidi kuongezeka kila mwaka.
Mbunge wa Wawi, Hamad Rashid Mohamed (CUF) alisema deni la nje linaongezeka kwa vile Serikali inakopa fedha hata kwa matumizi ya kawaida, badala ya kukopa fedha kwa matumizi ya miradi ya maendeleo. “Hii ni hatari kwa Taifa,” aling’aka.
No comments:
Post a Comment