Wednesday, January 11, 2012

Wenye hoteli Dom wamkana Makinda

CHAMA cha Wamiliki wa Hoteli na Nyumba za Kulala Wageni mkoani hapa, kimekanusha madai ya kupanda kwa gharama za huduma za malazi zilizoongeza gharama za maisha kwa wabunge kama ilivyotangazwa na Spika wa Bunge, Anne Makinda.

Mwishoni mwa mwaka jana, Makinda alitangaza kuwa posho za wabunge zimeongezwa kutoka Sh 70,000 mpaka Sh 200,000 kwa siku, kutokana na kupanda kwa gharama za maisha, kwa wawakilishi hao wa wananchi wawapo katika vikao vya Bunge.

Alisema sehemu ya gharama hizo ni pamoja na malazi, kwa kuwa baadhi ya nyumba zilizokuwa zimekodiwa na wabunge wa Bunge la Tisa, bado wanazimiliki na hivyo kusababisha wabunge wapya kupanga hotelini, ambako gharama ni kubwa.

Hata hivyo, jana Mwenyekiti wa chama hicho, Chavuma Taratibu, alisema uchunguzi uliofanywa na chama hicho wiki mbili zilizopita, umebaini kuwa kupanda kwa gharama za maisha mjini hapa hakulingani na majiji ya kibiashara ya Mwanza, Arusha, Mbeya, Morogoro na Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa taratibu, uchunguzi huo umebaini kuwa mkoa wa Dodoma una nyumba za kulala wageni 413 zenye vyumba 3,973 ambavyo gharama zake ni kati ya Sh 5,000 na Sh 45,000 kwa siku, kwa kuzingatia ubora wa vyumba na huduma zilizopo.

‘’Kwa nyumba za kulala wageni zenye vyumba vinavyounganisha huduma za vyoo na bafu, gharama yake ni kati ya Sh 10,000 na Sh 20,000 kwa kuzingatia ubora wa vyumba,’’ alisema Taratibu.

Alisema mbali na vyumba hivyo, pia vipo vingine maalumu vyenye hadhi ya juu ambavyo kwa siku ni kati ya Sh 80,000 na Sh 150,000 lakini vyumba hivyo Dodoma viko 25 tu.

Alisema wanafahamu kuwa hakuna mbunge anayeweza kupanga vyumba hivyo maalumu vyenye hadhi ambavyo pia vinatofautiana bei kulingana na umaarufu wa hoteli na ubora wa vyumba vya kulala wageni vilivyopo katika hoteli husika.

‘’Kwa tamko hili, tunapenda kufuta uvumi wa kisiasa kuhusu kuongezeka maradufu kwa gharama za maisha, hatua hiyo inalenga kuvuruga soko la huduma zetu mkoani hapa kwa kuwaogofya wageni na watalii na hivyo kuathiri biashara hizo na huenda hata mapato ya serikali yakapungua kutokana na kodi inayotoza,” alisema Taratibu.

Alisema kelele za kudai posho haziwezi kuthibitishwa kwa kauli zisizofanyiwa utafiti wa kina, licha ya kuwa hali ya uchumi imeyumba kwa nchi nzima, kutokana na kupanda kwa bei ya mafuta, kushuka thamani ya sarafu na uzalishaji duni uliosababishwa na tatizo la umeme uliodumu kwa mwaka mzima uliopita.

Wamiliki hao wa hoteli wanaungana na vyama vya siasa, asasi za kijamii, viongozi wa dini na baadhi ya wananchi, kupinga nyongeza hiyo ya posho.

Baadhi ya vyama vya siasa ikiwamo CCM, vilipinga ongezeko hilo la posho kwa maelezo kuwa haiwezekani lionekane Dodoma peke yake na kwa wabunge peke yao.

CCM katika taarifa yake, ilitaka juhudi zozote zitakazochukuliwa kupunguza makali ya maisha, zisiwe kwa wabunge pekee, bali kwa wananchi wote.

Baadhi ya viongozi wa dini, walisema uamuzi wa wabunge kutaka nyongeza ya posho hizo, ni ishara ya kuongezeka kwa ubinafsi katika jamii.

Pia Waziri Mkuu mstaafu, Fredrick Sumaye, alipinga posho hizo na kuonya kuwa zikisambaa kutoka kwa wabunge, na kuwa madai ya walimu, watendaji wa Serikali na baadae wanajeshi hata Rais hatatawala kwa usalama.

Hata hivyo, Naibu Spika, Job Ndugai, alimtaka Sumaye kuacha kukosoa Serikali iliyoko madarakani badala yake atoe ushauri, kwa kuwa changamoto za Serikali ya sasa ni tofauti na za serikali zilizopita.

Pia alimtuhumu Sumaye kuwa pamoja na kuwa mstaafu, lakini analipwa zaidi ya kutumia kodi hizo hizo za wananchi kuliko Naibu Spika ambaye yuko kazini.

No comments: