NAIBU Spika, Job Ndugai amedai kuwa Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye anatumia
fedha za wananchi kulipwa 'mshahara' mkubwa kuliko yeye wakati hafanyi kazi yoyote.
Amedai pia kuwa kiongozi huyo mstaafu anatumia fedha nyingi za walipakodi kuliko wabunge, huku akidai kuwa masuala yanayoendelea serikalini yanatokana na misingi iliyowekwa na viongozi wastaafu, akiwamo Sumaye.
Ndugai alisema hayo jana alipozungumza na gazeti hili kwa simu, kutoa maoni yake kutokana na kauli ya Sumaye iliyotaka Serikali iachane na nyongeza ya posho za wabunge kutoka Sh 70,000 hadi Sh 200,000 kwa siku kwani suala hilo linaweza kumweka pabaya hata Rais.
Sumaye alisema hayo juzi kupitia kipindi cha Dakika 45 kinachorushwa na kituo cha
televisheni cha ITV alipokuwa akizungumzia mambo mbalimbali ya Chama Cha Mapinduzi
(CCM) na Serikali kwa nchini na mambo mengine ya Afrika.
Ndugai alisema anamheshimu sana Sumaye na anauthamini uhuru wake wa kutoa maoni, lakini alimtaka awe makini katika kukosoa walioko madarakani, kwani wanafuata misingi iliyowekwa wakati wa utawala uliopita.
Alisema posho za wabunge zilikuwa zikiongezwa tangu Sumaye akiwa mbunge na hata akiwa Waziri Mkuu, hivyo kama hoja yake ni kiwango cha posho aseme, ili kuangalia kila anayelipwa kutokana na kodi za wananchi nani anapata zaidi.
Alisema kama suala ni matumizi mabaya ya fedha kwa wanaolipwa na Mfuko Mkuu wa Serikali, basi hata yeye analipwa malipo ya kustaafu kama kiongozi wakati wastaafu wengine hawalipwi.
“Mfano wa malipo anayolipwa ni asilimia 80 ya mshahara wa Waziri Mkuu aliyeko madarakani kwa sheria aliyoitunga yeye (Sumaye) akiwa madarakani, huku mimi nikiwa mmoja wa waliopitisha bungeni, ambao ni mkubwa kuliko hata mshahara wangu Naibu Spika … mbona hajataka malipo hayo yapunguzwe au kuondolewa?” Alihoji Ndugai.
Alidai kwamba kuna vipengele vingine vingi vya malipo kwa viongozi wastaafu ambavyo hawezi kuvisema, kwani hata daraja la ndege wanazopanda wabunge na Sumaye, bado anawazidi kwa viwango vya nauli.
“Mimi napanda daraja la pili wakati yeye anapanda daraja la kwanza, sasa kama ni kubana matumizi ya kodi za wananchi, nani anatakiwa kubana wakati anafanyiwa yote hayo akiwa amestaafu?” Aliendelea kuhoji.
Alidai kwamba kutokana na hali hiyo, wapo watu ambao wakilalamikia posho kubwa za wabunge wanaeleweka, lakini si Sumaye ambaye anatumia fedha nyingi kuliko posho hizo za wabunge.
Alimtaka Sumaye awe wa mwisho kupinga posho hizo, kwa kuwa pia si jambo jipya lipo kwa baraka za viongozi wastaafu.
Alisisitiza, kuwa hoja ya posho isiwe kwa wabunge tu bali kwa wote wanaolipwa kupitia
kodi za wananchi, wakiwamo wastaafu na viongozi wote wa nchi, kwa kuangalia nani
analipwa nini na kwa kiasi gani.
Aliwataka viongozi wastaafu kuacha kugombanisha wananchi na viongozi walioko
madarakani, bali wawaache wafanye kazi, kwa kuwa changamoto zilizopo sasa ni tofauti
na za zamani.
Alisema yeye akiwa kiongozi wa Bunge, ameamua kuzungumzia suala la posho tu na si
mengine yaliyozungumzwa kuhusu CCM na Serikali yake.
Akizungumzia maoni yake kuhusu nyongeza ya posho za wabunge, Sumaye alisema kwanza suala hilo halijaeleweka vizuri, kwa kuwa kumejitokeza kupingana kati ya Spika, Anne Makinda na Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashilila, huku Ikulu ikiwa kimya.
No comments:
Post a Comment