WATANZANIA kuanzia Jumapili wataanza kutozwa bei mpya ya umeme yenye ongezeko la asilimia 40.29, ili kuliwezesha Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kujiendesha kwa miezi sita, kabla ya mabadiliko mengine yenye nafuu au ghali zaidi kutangazwa.
Ongezeko hilo lisilohusisha Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) lilitangazwa Dar es Salaam jana na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma ya Nishati na Maji Nchini (Ewura), Haruna Masebu, baada ya kufanyia kazi maombi ya Tanesco yaliyopendekeza nyongeza ya asilimia 155 ya bei ya sasa, kwa kila mtumiaji.
Kwa mujibu wa Masebu, Ewura imefikia uamuzi huo baada ya kuzingatia vigezo muhimu na hivyo kuridhia kutoidhinisha ongezeko lolote la bei kwa watumiaji wa yuniti 0-50 za umeme
kwa mwezi, ambao wataendelea kutozwa Sh 60 kwa yuniti, tofauti na Sh 153 iliyopendekezwa na Shirika hilo.
Aidha, alisema wameamua wateja wa Zanzibar wanaouziwa umeme na Shirika la Umeme Zanzibar (Zesco) wapate unafuu kwa asilimia 10 huku wafanyakazi wa Tanesco waliokuwa wakitozana Sh 4 kwa yuniti badala ya Sh 157 waanze kulipa bei iliyoelekezwa kwa kuwa nao ni Watanzania.
Kwa maelezo ya Masebu, Serikali imechangia kwa kiasi kikubwa kufanikisha kupunguza makali ya maisha kwa Watanzania kwa kufuta kodi ya mafuta kwenye mitambo ambapo itakuwa kilipa Sh bilioni 18 ambazo ni gharama za mitambo ya IPTL pamoja na kusamehe deni la Sh bilioni 136 kwa Tanesco.
“Vinginevyo, nyongeza ya bei ingekuwa juu sana leo na kuumiza wengi. Vigezo hivyo ni kati ya vile muhimu tulivyovizingatia na kuamua kukataa pendekezo la asilimia 155 iliyotakiwa na Tanesco.
Kingine ni gharama zile ambazo wafanyakazi walikuwa wamepunguziana. “Tumezingatia, kwamba kama wangekuwa wanalipa kwa muda wote kama wengine, kusingekuwa na haja ya kuongeza bei kwa asilimia kubwa waliyoitaka, kwa kuwa wangekuwa wamesaidia kuchangia gharama za Shirika kujiendesha,” Masebu alisema.
Mkurugenzi huyo alisema kwa kuwa wameshughulikia maombi hayo kama dharura na kutoyaangalia kwa undani zaidi kutokana na muda, wamempa mtaalamu kazi ya kufuatilia mwenendo wa upatikanaji wa umeme huo kwa miezi hiyo sita ya mabadiliko ya bei, huku akilinganisha na upatikanaji wa umeme huo kuona kama una uwiano.
Kadhalika alisema mtaalamu huyo ataangalia mabadiliko ya hali ya hewa kwa kushirikiana na wataalamu wa eneo hilo, ili kuona kama kutakuwa na ulazima wa mitambo ya kuzalisha umeme kwa mafuta kuendelea kutumika au la, pamoja na endapo bei za awali zilizoainishwa na Tanesco kwa Ewura zilikuwa za kweli.
“Mapendekezo yake ndiyo yatatupa mwanga wa ama tuidhinishe ongezeko lingine la bei, kuacha lililopo au kupunguza kabisa. Hayo yote ni baada ya miezi sita kuanzia Januari 15, bei mpya itakapoanza kutumika. Ni kweli Tanesco walipaswa kupewa ongezeko kutokana na gharama walizotumia, lakini si kwa kiasi kile walichopendekeza. Wadau wa umeme nao waliliona hilo,” Masebu alisema.
Mkurugenzi wa Udhibiti wa Uchumi wa Ewura, Felix Ngamlagosi, alisema uamuzi wao ulizingatia kuepusha kuzorotesha uchumi, kwa kuwa hali halisi inajieleza kuwa bei ya umeme ikipanda, gharama za uchumi zitazidi na kuwashinda wengi.
Katika ufafanuzi wake wa bei, Ngamlagisi alisema, bei hiyo mpya itagusa wazalishaji wa viwandani wanaotumia uniti nyingi zaidi, ambao pia ni wengi zaidi ya makundi mengine.
“Watumiaji wa nyumbani wenye maduka na mashine za kusagisha na wanaotumia zaidi ya uniti 50 kwa mwezi, watawajibika kulipa asilimia hiyo 40.29 huku wa Zesco waliokuwa wakilipa Sh 83 kwa uniti wameidhinishiwa kulipa Sh 106 badala ya Sh 212 iliyoombwa na Tanesco.“
Kwa mantiki hiyo, waliokuwa wakiuziwa na Tanesco moja kwa moja na kulipa Sh 195 kwa uniti, sasa watalipa Sh 273 tofauti na Sh 497 iliyopendekezwa na Tanesco.
Waliokuwa wakilipa Sh 2,738 kwa uniti sasa watalipa Sh 3,841 badala ya Sh 3,106 iliyotakiwa na shirika hilo.
Novemba 9 mwaka jana, Ewura ilipokea ombi la dharura kutoka Tanesco la kuidhinishiwa ongezeko la bei za huduma ya umeme kwa wastani wa asilimia 155 ya bei ya sasa kwa madai kuwa wanaingia gharama kubwa katika kipindi hiki cha kuzalisha umeme wa dharura.
Baada ya ombi hilo ukafanyika mchakato wa kukusanya maoni ya wadau kuhusu uhalali wake ambapo Tanesco ilipendekeza bei hizo mpya zianze kutumika kuanzia Januari mosi.
Gharama hizo zinatokana na uzalishaji wa megawati 100 za IPTL kwa kutumia mafuta mazito, Symbion megawati 112 kwa kutumia gesi na Agreko megawati 100 kwa kutumia mafuta.
Viwango vinavyoombwa na Tanesco kwa watumiaji wadogo wanaotumia uniti kati ya 0-50 ni Sh 153 badala ya 60 kwa uniti, na wanaotumia zaidi ya uniti 50 wanunue uniti moja kwa Sh 497 badala ya Sh 195.
Baada ya Tanesco kuwasilisha maombi hayo Ewura, mamlaka hiyo iliitisha taftishi iliyohusisha wadau ambao hata hivyo walipinga kwa madai kuwa ongezeko hilo ni kubwa mno ikilinganishwa na hali halisi ya maisha ya Mtanzania.
Wadau hao pia walisema ongezeko hilo linatishia mustakabali wa uchumi, kwani bidhaa zitapanda bei kwa kila sekta inayotegemea umeme; hivyo kufanya maisha ya Mtanzania kuwa magumu maradufu.
Pia walionya kuwa hali hiyo inaweza kuleta madhara makubwa kwa wananchi mmoja mmoja na kwamba bei hiyo inaweza kuwafanya wawekezaji wasivutiwe tena kuwekeza nchini kwa kuogopa gharama za uendeshaji.
Kwa hali hiyo, waliishauri Serikali iangalie uwezekano wa kupunguza gharama za uzalishaji umeme wa dharura hasa kwenye na matumizi ya nishati kwa kutotoza kodi bidhaa hizo na kulipa kwa niaba ya Tanesco ‘Capacity Charge’ ya mitambo inayozalisha umeme wa dharura.
Wadau hao ambao ni watu binafsi, Shirikisho la Wenye Viwanda, Baraza la Ushauri la Watumiaji wa Huduma zinazodhibitiwa na Ewura na Baraza la Ushauri la Serikali, waliihadharisha Ewura, kuhakikisha wanapitia kwa makini maombi ya Tanesco, ili kuona
kama kuna ulazima wa wao kuruhusiwa kupandisha bei ya umeme kwa kiwango cha asilimia 155.
William Juhuniere akiwasilisha maoni ya Baraza la Ushauri la Serikali, alisema Tanesco wanapaswa kufanya juhudi kukusanya madeni yapatayo Sh bilioni 13.
Alisema kiasi hicho ni kikubwa na hakiwezi kuachwa kikapotea hivi hivi, wakati wadaiwa wanajulikana, na tayari walikwishatumia huduma.
“Hii ndiyo sera ya nchi ya kutimiza dhamira ya Serikali kufanya mashirika haya ya umma kuwa endelevu,” alisema Juhuniere. Pia aliitaka Tanesco iilazimishe Zesco kulipa deni la Sh bilioni 6.4 kwa kuwa uhusiano wa taasisi hizo mbili ni wa kibiashara, hivyo kila upande unapaswa kuheshimu mkataba.
Mwenyekiti wa Baraza la Ushauri la Watumiaji Huduma zinazodhibitiwa na Ewura (EWURA CCC) Profesa Jamidu Katima, alisema Baraza lake linapinga watumiaji wengine kulipia gharama za wafanyakazi wa Tanesco (Sh bilioni 16). Wafanyakazi hao wanapewa uniti 700 kila mwezi bure.
Renatus Mkinga alisema hata kama Tanesco wataruhusiwa kupandisha bei hiyo hawatamaliza matatizo yao na akashauri kuwa jambo la maana, ni Serikali kuliwezesha shirika kuzalisha zaidi
umeme.
Pia alishauri shirika hilo likusanye madeni yake kutoka taasisi za Serikali, ili fedha hizo zisaidie kugharamia mitambo ya dharura.
No comments:
Post a Comment