KAMATI ya Hesabu za Mashirika ya Umma(POAC) imelitaka Baraza la Ushauri la Watumiaji wa Huduma zinazothibitiwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Madini (Ewura -CCC), kuangalia namna ya kupunguza makali ya bei ya umeme kwa wananchi na si vinginevyo.
Agizo hilo la POAC limekuja kipindi ambacho wananchi wengi wamekuwa wakilalamikia ongezeko la bei ya umeme kwa asilimia 40.29 viwango vipya vya bei ya umeme vilivyotangazwa na Ewura na kuanza kutumika Januari 15 mwaka huu.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo, Deo Filikunjombe alisema baraza hilo linapaswa kuangalia hali halisi ya Watanzania, kabla ya kuunga mkono ongezeko la bei hiyo, jambo ambalo lingeweza kuwasaidia wananchi wa kawaida.
“Ewura –CCC liko kwa ajili ya kutetea maslahi ya Ewura, na si kubariki ongezeko la umeme ambalo limesababisha wananchi kulalamika, kutokana na hali hiyo tumelitaka baraza hilo kujiendesha kwa utaratibu wake kuliko kubebwa na Ewura,”alisema Filikunjombe.
Aliongeza kwamba hadi sasa baraza hilo linadhaminiwa na Ewura katika shughuli zake zote zikiwamo malipo, jambo ambalo limesababisha kushindwa kutoa hoja yoyote ya kimaslahi yanayohusu wananchi.
Filikunjombe alisema kutokana na hali hiyo tutaiomba Serikali kurekebisha sheria ili baraza hilo liweze kufanya kazi bila ya kushirikiana na Ewura.
Alisema kutokana na hali hiyo wamelitaka baraza hilo kufanya kazi bila ya kufungamana na upande wowote ili liweze kutenda haki kwa wananchi pindi Ewura na Serikali wanapopanga kuongeza bei ya umeme.
Kwa mujibu wa Filikuonjombe,mbali na suala hilo, kamati hiyo imewaagiza watendaji wake kutumia Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya katika matibabu ili kupunguza kutumia gharama kubwa wakati wa matibabu.
Awali, Serikali ilitoa Sh200 bilioni kwa ajili ya kununua umeme, ambazo ni sawa na asilimia 60 ya umeme, huku Tanesco ikichangia asilimia 40 akisema kama ingeshindwa kutoa kiasi hicho, gharama za umeme zingekuwa kubwa kuliko zilizotangazwa hivi karibuni.
Viwango vipya Katika ongezeko hilo la bei ya umeme ambalo limeanza kutumika Januari 15 mwaka huu, wateja wa hali ya chini wanaotumia chini ya uniti 50 kwa mwezi, wataendelea kulipa Sh60 kwa uniti wakati watumiaji wa majumbani wanaotumia zaidi ya uniti 50, bei hiyo imepanda kutoka Sh195 hadi Sh273 kwa uniti.
Watumiaji wa kawaida wakiwamo wenye biashara ndogondogo, bei imepanda kutoka Sh157 hadi Sh221 kwa uniti wakati watumiaji umeme mkubwa wa kati, bei imepanda kutoka Sh94 hadi Sh132 kwa uniti, wakati watumiaji umeme mkubwa hasa wenye viwanda na migodi, bei imepanda kutoka Sh84 hadi Sh118 kwa uniti.
Shirika la Umeme Zanzibar (Zeco), litauziwa umeme kwa Sh106 kwa uniti kutoka Sh83 ikiwa ni ongezeko la asilimia 28.21.
No comments:
Post a Comment