Monday, January 23, 2012

Hamad Rashid, Kafulila kususwa bungeni

VYAMA vya CUF na NCCR-Mageuzi, vimeamuru wabunge wake kuwasusa wabunge waliovuliwa uanachama pamoja na Mahakama kuzuia uamuzi wa vyama hivyo kwa muda na kutoa fursa kwa wabunge hao kuendelea na kazi yao ya uwakilishi.

CUF ilimvua uanachama Mbunge wa Wawi, Hamad Rashid Mohamed lakini Mahakama ikatoa amri ya kuzuia uamuzi huo na kesi ipo mahakamani kuhusu hatima ya mbunge huyo.

NCCR Mageuzi nayo mwishoni mwa mwaka jana, ilimvua uanachama Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila ambaye naye alikwenda mahakamani kupinga uamuzi wa chama chake na hivyo kuruhusiwa kuendelea na wadhifa wake.

Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Julius Mtatiro katika mazungumzo yake na gazeti hili wiki hii, alisema wabunge wa chama hicho wataendesha mgomo baridi kwa kumsusia Mbunge wa Wawi, Hamad na mambo yake yote hadi atakaposalimu amri mwenyewe.

“CUF hakina ugomvi na Mahakama wala Bunge kwa sababu kilitekeleza matakwa ya Katiba yake ambayo haimzungumzii mbunge bali mwanachama. Kwa maana hiyo, tuliyemwadhibu kwa kumvua uanachama ni Hamad Rashid kama mwanachama na wala sio Mbunge wa Wawi.

“Ubunge wake ni yeye na Bunge na wala chama hakihusiki naye. Akifanya mikutano ataifanya kama ya Hamad sio ya CUF kwa sababu hakuna kiongozi wa CUF atakayekubali kumwandalia mikutano wala ziara kwa sasa kwa kuwa tayari anahesabika kuwa mwasi aliyefukuzwa katika chama,” alisema Mtatiro.

Mtatiro alisisitiza hata wabunge aliowaita halali wa CUF walioko bungeni hawatampa ushirikiano pia.

Hata hivyo Kiongozi wa wabunge wa CUF bungeni na Mbunge wa Mkanyageni, Mohamed Mnyaa alikataa kuzungumzia mkakati wa kumsusa Hamad kwa madai kwamba suala linapokuwa mahakamani, halipaswi kuzungumzwa.

Naye Msemaji wa NCCR Mageuzi na Mbunge wa Kasulu Mjini, Moses Machali alisema hata kama Mahakama itampa ushindi Kafulila katika kesi iliyopo mahakamani, chama hicho kitaendelea kumtenga na kutompa ushirikiano wa aina yoyote.

“Huyo sio Mbunge sasa tutahitaji kuwa na uhusiano gani wa kibunge huko bungeni? Mimi na NCCR tunamchukulia kama Mtanzania wa kawaida aitwaye David Kafulila,” alisema Machali.
Alionya kuwa NCCR Mageuzi haitahusika na shughuli zote zinazofanywa na Mbunge huyo kwa niaba ya chama ikiwa ni pamoja na kutishia kumfikisha mahakamani kwa kukaidi ukweli kuwa sio mwanachama wa chama hicho.

“Hatutaki atuwakilishe katika jambo lolote na tukimkamata anafanya shughuli za chama tutamchukulia hatua za kisheria ikiwa ni pamoja na kumfikisha mahakamani kwa kuwa kwa sasa yeye ni mwananchi wa kawaida asiye na chama,” alisema Machali.

Naye Kafulila alisema; “naheshimu Mahakama. Siendekezi malumbano. Mimi ni Mbunge na Mjumbe wa Kamati Kuu ya NCCR-Taifa. Sitaki kuzungumza sana, nachapa kazi ili nilete maendeleo kwa walionichagua na taifa. Nawajibika, situkani na sitamtukana mtu wala chama.”

Alidai hata shughuli zote alizozifanya ziliandaliwa na viongozi wa juu wa chama hicho na kwamba hata siku moja hafanyi mambo yahusuyo chama chake bila kushirikishwa.

“Sasa ilikuwaje hawakunikamata nilipofanya ziara na mikutano hivi karibuni baada ya uamuzi wao? Nilizuru kata za Mtego wa Noti, Nguruka, Uvinza, Ilagala, Kazulanimba, Ilalangulu na nyinginezo kwa maandalizi ya wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama Taifa; Stephen Mapunda na Kayombo Kabutali. Wanataka nihitaji ushirikiano gani tena kutoka kwa chama?” Alisema Kafulila.

Hamad kwa upande wake alidai kuwa ataweza yote kwa ushirikiano na wananchi waliomchagua na wala sio viongozi wanaofanya mambo kwa kushinikizwa na kukiuka katika ya chama husika.

“Wananchi walionipeleka bungeni ndio wanaonisapoti na wala sitishiki kwa kutoungwa mkono na viongozi madikteta wa CUF. Wanavunja sheria kwa maneno yao na vitendo visivyozingatia haki lakini mimi nasonga mbele kwa nguvu ya wananchi wangu,” alidai.
,isema hakuna mwenye haki ya kumzuia kuendesha mikutano kwa sababu kama Mbunge anayo nafasi yake ya kufanya shughuli hizo.

No comments: