NAFASI anayopewa mtu ndani ya jamii ili awatumikie wanajamii wenzake, kwa maana kwamba wenzake wanamuomba awatumikie, ni nafasi ya uwakilishi.
Anayepewa nafasi hiyo anakuwa katumwa kazi, amebebeshwa mzigo kwa niaba ya jamii yake kwa sababu jamii imetambua kwamba yeye anao uwezo ambao wengine hawana wa kuifanya kazi hiyo.
Katika mjumuiko wa kisiasa, kama vile chama cha kisiasa, hali ni ile ile. Nafasi ya uwakilishi hupewa mtu anayeonekana kuwa na uwezo mkubwa kuliko wenzake katika kutimiza jukumu fulani. Chama ama kundi jingine lolote lenye nia moja humteua mtu au huwateua watu kwa misingi ya jukumu lililopo wakati huo.
Majukumu hubadilika, au yakachukua sura mpya, na ikiwa hivyo basi chama pia kitabadilisha mtazamo katika uteuzi wa mwakilishi wake. Kwa mfano, tukiangalia historia ya kisiasa ya Tanganyika tutatambua kwamba Julius Nyerere, kijana kutoka shamba, mtu “wa kuja” ambaye hata Kiswahili chake hakikuwa na lafudhi ya kuvutia kwa watu wa mwambao, aliteuliwa kuwawakilisha wazalendo waliotamani kupata Uhuru, wengi wao wakiwa watu wa mwambao, kwa sababu yeye ndiye alikuwa na sifa zilizotakikana ili kumkabili mkoloni.
Nyerere alikuwa kapata elimu kubwa kuliko wenzake wengi; aliwajua Waingereza labda kuliko mwingine yeyote miongoni mwao; alikuwa na uwezo wa kujenga hoja na zikaeleweka kwa Waingereza; pia alikuwa na ujasiri wa kusema anachotaka kusema bila kumung’unya maneno. Alikuwa ndiye mtu mwafaka wa kumtuma kupeleka ujumbe kwa Waingereza.
Alikuwa na sifa nyingine pia, ambayo hatuisemi sana ingawa ni wazi kuwa ilikuwa na umuhimu wake: Alikuwa Mkristo na dola aliyotumwa kupambana nayo ilikuwa ni dola ya Wakristo. Kwa hiyo ilikuwa ni rahisi zaidi kwa wakoloni kumwamini, na hususan kwa sababu katika miaka aliyokaa nchini mwao kama mwanafunzi walikwisha kumtathmini na kumuona kama mwenzi wao ambaye asingewasababishia mashaka makubwa.
Tunaweza kufikiria mazingira mengine, na bila kwenda mbali. Kama Tanganyika ingekuwa na hali ya kisiasa iliyofanana na Kenya ya wakati ule, katikati ya uasi wa Mau Mau, na kama wazalendo wa Tanganyika wangekuwa wameamua kwamba njia pekee ya kumng’oa mkoloni ni mapambano ya kisiasa, labda wasingemteua Nyerere.
Labda wangemteua mmoja wao mwenye uwezo wa kuongoza wapiganaji wenye silaha ili ajenge jeshi la kupambana na Mwingereza, na labda kwa mantiki hiyo wangemteua Ally Sykes, aliyekuwa katoka vitani.
Pia, katika mazingira inapobidi kuchukua njia ya mapambano ya silaha, huyo ambaye angechukua nafasi ya uongozi asingeteuliwa kwa maana ya kuteuliwa kwa wengi wa wanaharakati kumkubali, au kumpigia kura. Angejitokeza tu, akasimama, akwaambia wenzake kwamba maneno yametosha na hayawapeleki kokote; sasa ni mtutu wa bunduki. Na historia ya harakati za kutafuta Uhuru ingekuwa tofauti kabisa.
Hali kama hiyo ndiyo iliyotokea Kenya. Hakuna kumbukumbu zinazoonyesha kwamba Dedan Kimathi, shujaa wa vita ya Mau Mau alichaguliwa na mkutano mkuu wa wapiganaji. Na mapema kuliko wakati huo, hatuna ushahidi wa kuonyesha kama Kinjeketile, shujaa wa vita ya Maji Maji alichaguliwa na mtu yeyote kuwa kiongozi wa harakati hizo.
Katika historia ya Kenya tunajifunza, kama nilivyosema mapema, kwamba mazingira yakibadilika na aina ya mtu anayetafutwa kuwawakilisha wenzake inabadilika. Ndiyo maana wakati Kenya inaandaliwa kupata Uhuru na wazalendo wa nchi hiyo wanatafuta kiongozi wa kupokea mikoba kutoka kwa Waingereza, hawakutafuta mpiganaji wa Mau Mau, mfuasi wa Kimathi. Walimtafuta Jomo Kenyatta, ambaye hakuwa na uhusiano na Mau Mau na alikwisha kuwakana hadharani.
Ninachosema hapa ni kwamba nchi, jamii, chama cha kisiasa au kundi lolote linalokabiliwa na changamoto katika ustawi, usalama ama maendeleo, humteua mtu, au huwateua watu wa kuwakilisha mjumuiko wao kufuatana na hali waliyo nayo, na sifa za hao wanaoteuliwa hubadilika kufuatana na mazingira ya wakati huo.
Tukirudi katika hali yetu nchini Tanzania, leo tunashuhudia kwamba wanasiasa wetu wanapigana vikumbo wakiwania kuchukua nafasi ya urais. Nimekuwa nikijiuliza, hivi hawa wanasiasa wanapendekezwa na wanajamii wenzao kwa sababu wamewaona wanazo sifa za kusaidia ama chama ama nchi katika nyanja walizozichunguza na kuzitathmini? Au ni watu wanaojipendekeza wenyewe na kukusanya mashabiki wa kuwafanyia kampeni kwa sababu tu wanakinyang’anyiro hao wana malengo wasiyoyatamka hadharani na wakipata nafasi wanayoitafuta watawagawia mashabiki wao sehemu ya ngawira watakayoiteka?
Bila shaka urais umeshuka thamani, umechuja, (wako wanaoiona Ikulu kama kijiwe) iwapo kila mtu anajiona anaweza kuwa rais, hata mbumbumbu wa kisiasa wasiojua hata historia ya chama wanachotaka kukiwakilisha, wasiojua historia ya dunia wala Afrika, wasiojua siasa ni nini mbali na kutafuta nafasi za ulaji na ufisadi.
Kwa sababu katika mlo hakuna uwakilishi, kila mtu atataka kwenda mwenyewe mezani. Haiyumkiniki kwamba watu watasema wanamwachia mmoja wao awakilishe kwenye mlo. Hicho ndicho kiini cha mapambano makali tunayoyashuhudia leo hii.
Mimi si bashiri, na wala sipigi ramli, lakini jinsi tunavyoenenda na siasa hizi bandia, watu watatoana roho, kama hawajaanza bado. Yote hii ni kwa sababu nafasi iliyokuwa ya uongozi na kazi ngumu na majukumu mazito sasa imekuwa nafasi ya kujinufaisha mtu na familia yake na watu wa karibu, ‘washikaji’ wasemavyo watu wa mjini.
Hali ya mikanganyiko iliyoikumba Tanzania hivi leo isingeweza kukupa sura ya nchi ambayo watu watauana ili wapate nafasi ya kuitumikia. Umasikini unaozidi kujichimbia nchini katikati ya utajiri wa ajabu; kukata tamaa kwa wananchi wasiouona vyema mustakabali wao kwa jinsi wanavyoendeshwa; dalili za vurugu zinazotuchungulia kama tutaendelea tulivyo; vijana waliojaa ghadhabu kwa sababu wanaona wamenyimwa haki zao za msingi; rushwa, wizi, ulaghai kila pembe…. Hii siyo hali ya kuwafanya watu wajipendekeza kuongoza. Ni hali ambayo, katika mazingira ya kawaida, ingeilazimisha jamii kuwalazimisha wanasiasa na viongozi wenye sifa, wakubali kubeba mzigo wa kuikwamua jamii, siyo wao wajipendekeze na watoane roho kwa tamaa ya kubebeshwa mizigo mizito.
Hatuleti maana, tumekiuka mantiki.
No comments:
Post a Comment