MADAKTARI bingwa wasiopungua 12 wa idara mbalimbali za Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) jijini Dar es Salaam wanadaiwa kuwa katika mgomo baridi kwa siku kadhaa sasa, kupinga kuhamishiwa mikoani.
Aidha, Taasisi ya Saratani ya Ocean Road, Dar es Salaam nayo imekumbwa na tatizo kama hilo kutokana na madaktari wake kutotibu wagonjwa, kuanzia Jumatatu, bila kueleza sababu.
Hali hiyo, imeelezwa kuzorotesha kwa kiasi kikubwa utoaji huduma katika hospitali hizo, kiasi cha kuathiri wagonjwa kisaikolojia, kwa hofu kuhusu uhai wao.
Habari kutoka kwa wauguzi, madaktari walioajiriwa kwa mkataba waliomba kutotajwa gazetini na baadhi ya ndugu wa wagonjwa katika hospitali hizo, zilisema madaktari bingwa hao hawajawaeleza chochote kuhusu matibabu yao, licha ya kuonekana hospitalini wakati wote.
Walisema kwa nyakati tofauti, kuwa walitangaziwa kuwa madaktari walikuwa na dharura yenye umuhimu wa juu na hivyo kuombwa warejee nyumbani kusubiri siku nyingine, kwa kuwa wasingewahudumia wakati huo.
Ocean Road tangazo hilo linadaiwa kutolewa na muuguzi wa kike ambaye jina lake halikuweza kujulikana, baada ya wagonjwa siku hiyo kuhudumiwa.
Muhimbili, wagonjwa waliokuwa wakisubiri upasuaji Ijumaa walidai kutangaziwa kuwa waendelee kula kama kawaida kwa kuwa operesheni zao ziliahirishwa kwa muda, bila kupewa maelezo ya ziada.
“Mara ya mwisho kuzungumza na daktari ilikuwa Alhamisi ambapo tuliandaliwa kwa kupewa namba na mashuka na kuelezwa kuwa tusile chakula kwa sababu upasuaji ni asubuhi, cha kushangaza, hakuna kilichoendelea kuhusu operesheni hadi daktari aliyepita kuruhusu wenye nafuu jana kutueleza kuwa tuendelee kula tu.”
Pamoja na maelezo hayo, gazeti hili lilishuhudia MNH ikiwa katika ukimya usio wa kawaida kuanzia jana asubuhi hadi saa 8 huku baadhi ya madaktari walio katika mafunzo wakiwa wamesimama katika makundi kwenye korido lililopo kati ya wadi za Mwaisela na Sewahaji, wakizungumza mambo yao.
Wauguzi waliozungumza na gazeti hili walisema hali si nzuri sana, kwa sababu huduma zinazohitaji wataalamu (mabingwa) zimesimama.
"Kama unavyotuona tunawajibika katika nafasi zetu, tatizo lipo kwa baadhi ya madaktari, huduma zilizo ndani ya uwezo wetu zinaendelea, kwenye upasuaji na tiba nyingine ndio kuna tabu,” alisema muuguzi mmoja na kuungwa mkono na mwenzake wa wadi nyingine, aliyedai kuwa wagonjwa wengi wamekata tamaa ya kutibiwa.
Dodoma nako Naye Sifa Lubasi, anaripoti kutoka Dodoma, kwamba madaktari, wauguzi, wafamasia na watumishi wengine wa Hospitali ya Mkoa wa Dodoma wameanza mgomo kushinikiza kupatiwa mazingira bora ya kazi na kutaka Waziri wa Afya kujiuzulu.
Huduma zinazoendelea katika hospitali hiyo ni za dharura tu. Kwa hali hiyo, katika hospitali hiyo wameiomba Serikali kusikiliza kilio chao ili kuendelea kutoa huduma za afya kama kawaida.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Kuratibu Madai ya Watumishi hao, Dk. Yahya Magaso alisema zaidi ya watumishi 100 wa hospitali hiyo wameingia kwenye mgomo wakiwamo madaktari kuishinikiza Serikali kupitia Wizara ya Afya kusikiliza madai yao na kuyafanyia kazi.
Mganga Mkuu wa Hospitali hiyo, Dk. Godfrey Mtei alisema uongozi umekaa na kuwashauri waendele na kazi, lakini hata hivyo alisema bado hawajafikia muafaka na majadiliano bado yanaendelea.
No comments:
Post a Comment