MTOTO mwenye umri wa mwaka mmoja (jina tunalo) anateseka katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC ya mjini hapa, baada ya kukeketwa kwa ridhaa ya mama yake mzazi.
Mama wa mtoto huyo, Magdalena Julius (19), amekiri kufanya kitendo hicho, akisema alimpeleka mwanawe kwa mganga wa kienyeji ili akeketwe kutokana na kuchelewa kutambaa na pia kuwa na afya isiyoridhisha.
Hata hivyo, tofauti na matarajio yake, mara baada ya kukeketwa hali ya mtoto huyo ilibadilika na kuwa mbaya zaidi kutokana na kuvuja damu nyingi.
Bibi wa mtoto huyo, Rehema Taraa ndiye aliyegundua tukio la kukeketwa kwa mjukuu wake kutokana na mtoto huyo kulia usiku kucha na ilipofika asubuhi, alimpeleka Hospitali ya Wilaya ya Hai na madaktari kubaini mtoto alikuwa ameishiwa damu na maji mwili, hivyo kutakiwa amhamishie Hospitali ya Mkoa wa Kilimanjaro ya Mawenzi.
Akisimulia, bibi huyo alisema madaktari wa Hospitali ya Mawenzi walimpokea, lakini wakashauri apelekwe KCMC kutokana na hali ya mtoto kuzidi kuwa mbaya.
“Huko ndiko walikothibitisha kuwa amekeketwa na kwamba alidhoofika kutokana na kuvuja damu nyingi. Aliongezewa maji na damu ili kunusuru maisha yake.”
Naye Mratibu wa mtandao wa kupiga vita ukeketaji kwa wanawake na watoto wa kike (AFGEM), Honoratha Raymond, naye alizungumzia kitendo hicho, akilaani na kuiomba Serikali kwa kushirikiana na wadau kuvalia njuga unyanyasaji wa kijinsia hasa kwa watoto ambao bado hawana uwezo kiakili wa kujitetea.
Ingawa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kilimanjaro, Absalom Mwakyoma hakupatikana kuzungumzia suala hilo, lakini tayari mama wa mtoto huyo amewekwa chini ya ulinzi wa Polisi, huku akiendelea kumuuguza mwanawe.
www.habarileo.co.tz
No comments:
Post a Comment