Monday, January 16, 2012

Wanasheria wafungua kesi kupinga Mchakato wa Katiba



Na Fredy Azzah
CHAMA cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS), kimewateua mawakili wanne watakaosimamia kesi ya kupinga sheria ya kuundwa kwa katiba mpya iliyopitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka jana.

Rais wa chama hicho, Francis Stolla, aliliambia gazeti hili jana kuwa Mawakili hao ni pamoja na Profesa Gamalieli Simbo, Wakili Richard Rweyogeza, Silwami Gallapi Mwautembe pamoja na Fulgence Massawe.

“Tumewapa na hadidu za rejea, moja ni kuhakikisha kuwa hii kesi inafunguliwa kabla ya huu mwezi kwisha,” alisema Stolla.Alisema kuwa, majukumu mengine ya mawakili hao ni kufanya utafiti juu ya kesi hiyo na kuandika mashtaka pamoja na kuisimamia kesi hiyo.

“Kesi ikiisha itabidi pia waje kutoa ripoti katika chama,” alisema Stolla.
Alieleza kuwa, mawakili hao wataisimamia kesi hiyo bila kupewa malipo yoyote na chama hicho kwa kuwa na wao ni wanachama.

“Gharama ambazo chama kitatoa ni zile za ada ya kufungua kesi pamoja na kutoa fotokopi za nakala mbalimbali,” alieleza Stolla. Aliongeza kuwa, kwa kuwa kesi hii ni ya kikatiba chama hicho hakitatoa notisi kwa serikali kabla ya kuifungua.

"Hii ni kesi ya kikatiba, haihitaji kutoa taarifa kwa Serikali. Tunatumia sheria ya haki za msingi na wajibu wa kutekeleza ya mwaka 1994," alisema Kwa mujibu wa Stolla, kesi hiyo ni dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

“Tumeunda kamati ya kushughulikia katiba, yenye wajumbe wanane. Kwa sasa wajumbe hao wako katika mchakato wa kuandaa hati ya mashtaka. Wakimaliza, tutateua mawakili watatu wa kuisimamia kesi hiyo mahakamani kwa niaba ya chama,” alisema Stolla.

“Kwa sababu sheria inasema ukitaka kiishtaki serikali inabidi umshitaki Mwanasheria Mkuu, kwa hiyo tutafanya hivyo lakini kesi hii ni ya kikatiba na mlengwa wetu ni Bunge,” alisisitiza. Alisema hatua ya kulishtaki inatokana na dhamana ya chombo hicho ya kutunga sheria. "Tunalishtaki kwa sababu sheria hiyo iliyoitunga ni mbovu,” alisema.

Stolla alisema sababu za kufungua shtaka hilo ni pamoja na sheria hiyo kukiuka katiba ya Tanzania ya mwaka 1977. Alitaja ibara zilizokiukwa kuwa ni pamoja na ile ya 18 inayowapa nafasi wananchi kutoa maoni yao na ibara ya 22, inayotaka wananchi washirikishwe kwenye masuala muhimu na yenye maslahi kwao.

Kwa mujibu wa Stolla sababu nyingine ya kufungua kesi hiyo, ni sheria hiyo kukiuka taratibu za utungwaji wa sheria, ikiwa ni pamoja na kupitishwa na Bunge baada ya kusomwa mara mbili, badala ya mara tatu kama inavyotakiwa kisheria. “Mara ya kwanza walipowasilisha hati ya dharura bungeni, kelele zilipigwa kuwa iondolewe na utaratibu wa kutungwa kwa sheria hii uwe wa kawaida. Pia kutaka ule muswada uandikwe kwa lugha ya Kiswahili, mambo yale yalitekelezwa,” alisema.

Alisema kuwa baada ya kuandikwa kwa lugha ya Kiswahili ambayo Watanzania wengi wanaielewa, muswada ulipaswa kurudishwa kwa wananchi ili waujadili lakini jambo hilo halikufanyika. “Siku ile wanasoma ule muswada wa Kiingereza kwa mara pili, waliusoma ule wa Kiswahili kwa mara ya kwanza lakini wakadai kuwa ni mara pili. Halafu wakaja kusoma tena mara ya pili na kuupitisha.

Sheria inataka usomwe mara tatu, kwa hiyo ni wazi kuwa huu ulipitishwa baada ya kusomwa mara mbili badala ya mara tatu kama inavyotakiwa,” alifafanua Stolla. Alisema sababu nyingine ni sheria hiyo kuwa na vipengele vinavyozuia watu au asasi nyingine nje ya tume itakayoundwa kuwaelimisha wananchi juu ya katiba.

Stolla alisema katika kifungu cha 22, sheria hiyo inaweka makosa ya jinai na adhabu kwa mtu ama taasisi, itakayofanya kampeni ya kuhamasisha juu ya katiba. “Kwa sheria hii midahalo kama inayofanywa sasa hivi inaharamishwa, ni tume ya katiba mpya tu ndiyo itahamasisha kwa mikutano maalumu, kwa hiyo sisi tunadhani kuwa hali hiyo inanyima uhuru wa kutoa maoni,” alieleza.www.mwananchi.co.tz

No comments: