KATIBU Mkuu wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), Amina Makilagi amesema watashiriki kikamilifu kuhamasisha wajumbe na wanachama kuchagua viongozi wanawake wanaofaa katika uchaguzi mkuu wa 2015.
Alisema hayo juzi jioni wakati wa mahojiano na gazeti hili mara baada ya kumalizika kwa kikao kazi cha siku mbili kilichohusisha makatibu wa UWT wa mikoa na wilaya kutoka mikoa na wilaya za Tanzania Bara.
Viongozi 152 walihudhuria mafunzo hayo mjini Dodoma ikiwa ni sehemu ya mafunzo kuelekea uchaguzi wa ndani ya CCM na jumuiya zake.
“UWT bado ni imara tutashiriki kikamilifu kuhamasisha wajumbe wanawake kujitokeza kwa wingi katika uchaguzi,” alisema.
Alisema kuwa UWT wana msimamo tangu wakati wa Chama cha TANU na imeendelea kuwa na viongozi waaminifu na waadilifu wanaozingatia kanuni za chama.
“Hatuwezi kuingia kwenye makundi au kuingizwa kwenye makundi, wanatuogopa kutokana na msimamo wetu ndiyo maana unaona siku zote kwenye chama chetu tuko shwari,” alisema.
Makilagi alisema kuwa baada ya mafunzo hayo watakwenda kuhamasisha wenzao hata katika suala la mchakato wa kupata Katiba mpya ili Tume
ikifika, watoe maoni yao ili ipatikane Katiba mpya inayoendana na wakati wa sasa.
“Bunge lililomalizika Novemba mwaka jana lilifanya vizuri kupitisha Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba mpya ni vyema tukatumia nafasi hiyo vizuri.
“Tupiganie chama chetu na tupiganie haki za wanawake kuanzia ngazi ya shina hadi mkoa. Yote mliyojifunza kwa lengo la kuongeza uwezo muyazingatie ili kuboresha kazi za chama,” alisema na kuongeza kuwa wako tayari kulima hata kwa jembe la mkono ili kufanikisha sera.
No comments:
Post a Comment