Monday, January 9, 2012

CUF, NCCR Vyadumaza Demokrasia

WIMBI la wabunge kufukuzwa katika vyama vya siasa vya upinzani na kupoteza sifa za kuwa wabunge, lililoanzia katika chama cha NCCR-Mageuzi na sasa CUF, limeshutumiwa kwa kudumaza demokrasia na kuwatisha wananchi walioanza kuamini vyama hivyo.

NCCR mageuzi mwishoni mwa mwaka jana, kilimtimua uanachama Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila na kufuatiwa na CUF, ambacho wiki iliyopita kilimtimua Mbunge wa Wawi, Hamad Rashid Mohamed.

Lakini uamuzi huo ambao katika vyama hivyo umepewa jina la uamuzi mgumu, umekosolewa kuwa umeonesha udhaifu wa vyama hivyo katika mfumo wa kutatua migogoro ya ndani na kutishia kurejesha historia ya vyama hivyo ya kuibuka na kubomoka ambayo CCM waliviita ‘vyama vya msimu’.

Mbali na udhaifu huo, vyama hivyo pia vimekosolewa kwa kuwa na uchanga katika kujiendesha kitaasisi ambapo imeelezwa kuwa vimegeuka taasisi za vikundi vya watu wasiotaka kupingwa kifikra.

Udhaifu wa kutatua migogoro Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) Idara ya Siasa, Audax Kweyamba alipozungumza na gazeti hili jana alisema vyama vingi havijajenga mifumo ya kudhibiti migogoro na havina mbinu za kuitatua.

Kwa mujibu wa Kweyamba, udhaifu huo umesababisha vyama hivyo kutatua matatizo yao kwa kufukuzana kwa kigezo kidogo cha kupishana fikra na mitazamo.

Wamiliki wa vyama
Pia Mkuu wa Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. Benson Bana alisema mfumo wa uongozi wa kitaasisi ndani ya vyama hivyo vya siasa ndio chachu kubwa ya migogoro.

Kwa mujibu wa Dk. Bana, baadhi ya viongozi katika vyama hivyo wamekuwa wakihodhi nafasi na kuwa kama wamiliki wa vyama hali ambayo inawanyima wengine kutoa mitazamo na fikra zao.

“Endapo mbunge huyu ambaye anakipatia chama husika ruzuku akijaribu kutoa mtazamo wake na ukawa hauendani na Mwenyekiti au Katibu ambao si wabunge, matokeo yake ni
kufukuzwa,” alisema Dk. Bana.

Udhaifu wa Katiba
Dk. Bana alisema pamoja na ukweli kuwa kila chama kina kanuni na miiko yake ikiwa ni pamoja na heshima ya kukosoana na kufukuzana, bado kosa kubwa lipo kwenye Katiba.

Alisema kitendo cha chama kumfukuza uanachama mbunge na kumuondolea sifa ya kuwa mbunge, kinawanyima haki wananchi waliomchagua na kuwaweka katika wakati mgumu hali ambayo inapaswa kuangaliwa kwa umakini.

Wajifunze kutoka CCM
Dk. Bana ameshauri vyama hivyo ikitokea mwanachama ametoa mtazamo wake na ukawa hauendani na Mwenyekiti au Katibu wajifunze ‘kuvumiliana’ kama CCM.

Alishauri katika mchakato wa kupata Katiba mpya, kipengele kinachovipatia vyama vya siasa nguvu ya kumuondoa mbunge wadhifa wake, kiangaliwe kwa kuwa bado Tanzania haijafikia mfumo wa kuchagua viongozi kwa kigezo cha chama pekee.

Mbali na Dk. Bana kuvitaka vyama hivyo kujifunza CCM, Kweyamba alisema katika eneo la kutatua migogoro vyama vya CCM na Chadema angalau vyenyewe vimejitahidi na kuonesha mfano mzuri wa kuzungumza matatizo yao na kukanyana lakini si kwa mbinu ya kufukuzana
uanachama.

Alisema wakati umefika kwa viongozi wa siasa kufikiria zaidi maendeleo ya vyama hivyo kwa kutafuta njia nzuri za kumaliza migogoro yao bila kuathiri jamii inayowazunguka.

“Waangalie mbele na athari za kumfukuza mtu hasa mbunge, Watanzania walishaanza kujenga imani na vyama vya upinzani lakini sasa wanajenga uoga kwa yanayotokea, wananchi hawana furaha na vyama hivi na hasa ukizingatia historia yake ya tangu zamani,” alisema Kweyamba.

Alisema hali hiyo ya migogoro kwa ujumla inadumaza demokrasia badala ya kuijenga kama ilivyo dhana nzima ya kuwa na vyama vya siasa vya upinzani.

“Na sisi kama wanataaluma lazima tuzungumze kwani hali ikiendelea hivi tutarudi nyuma kisiasa,” alihadharisha Kweyamba.

No comments: