Friday, January 13, 2012

Salma: Juhudi bado zatakiwa kumuinua Mwanamke

MKE wa Rais, Salma Kikwete amesema pamoja na mafanikio ambayo dunia imepata katika kumuinua na kumuendeleza mwanamke, bado juhudi zinatakiwa kuhakikisha naye anapata fursa sawa ya kumiliki utajiri.

Alisema hayo Dar es Salaam juzi katika viwanja vya Ikulu alipokutana na wenzi wa mabalozi nchini kwa ajili ya kuuaga mwaka na kuukaribisha mwaka mpya.

Alisema tangu mapambano ya kuhakikisha mwanamke naye anakuwa na haki yaanze, mafanikio mengi yameonekana na sasa anaheshimika duniani kote ikiwamo Tanzania.

“Leo mwanamke anashiriki katika mambo mengi ya maendeleo duniani ikiwamo ngazi za uamuzi na umuhimu wake sasa unaanza kuonekana kuliko ilivyokuwa zamani,” alisema.

Hata hivyo alisema pamoja na ukweli huo, takwimu zinaonesha kuwa katika idadi ya watu duniani, wanawake ni asilimia 50 na wanaofanyakazi ni asilimia 40 duniani kote na kwa upande wa Afrika asilimia 80 ndio wazalishaji wakuu wa chakula lakini ni asilimia moja tu ndio wanaomiliki utajiri.

“Takwimu hizi zinaonesha kuwa bado kuna pengo kubwa katika maeneo mengi linahitaji kufanyiwa kazi ili kupata usawa kwa wanawake duniani, ingawa kwa sasa ninafaraja kujua kuwa katika ripoti ya Benki ya Dunia ya mwaka huu imejikita zaidi katika kuinua wanawake,” alisema.

Alisema kutokana na ukweli huo, Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) chini ya uenyekiti wake, ajenda yake itaendelea kuwa ni maendeleo kwa wanawake ambapo alishukuru ushirikiano wa Serikali na wafadhili mbalimbali wanaoiunga mkono taasisi hiyo.

Mke wa Balozi wa Kenya nchini, Naomi Mutiso akizungumza kwa niaba ya Mwenyekiti wa Chama cha Wake wa Mabalozi nchini, alipongeza juhudi za Mama Salma na WAMA katika kuinua wanawake kiuchumi na kusaidia watoto wa kike kielimu hali ambayo itawakwamua na umasikini.

No comments: