Friday, January 20, 2012

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Ongezeko la bei ya umeme kuongeza makali ya ugumu wa maisha kwa Watanzania masikini!

Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), tumekuwa tukifuatilia kwa karibu masuala yanayogusa jamii hapa nchini ikiwa ni sehemu ya kudai mabadiliko ya mfumo wa uchumi, sera, sheria na bajeti katika kampeni yetu ya kudai haki ya uchumi, na hasa ajira na maisha endelevu kwa wote. Lengo ni kuhakikisha mgawanyo sawa wa rasilimali za taifa kwa manufaa ya wananchi wote wanawake, wanaume, wazee, watoto, watu wanaoishi na ulemavu, hususani wale walioko pembezoni.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji nchini (Ewura), Haruna Masebu ametangaza kupanda kwa bei ya umeme kwa asilimia 40.29 kuanzia Januari 15 mwaka huu. Alisema ongezeko hilo halitawahusu wateja wa hali ya chini, wanaotumia chini ya uniti 50 kwa mwezi pamoja na Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO)

Swali la kujiuliza ni akina nani hawa wanaotumia umeme chini ya uniti 50 katika hali halisi ya maisha ya Mtanzania wa kawaida? Ni mara chache sana kupata watu wanaoangukia kwenye kundi hili, lakini pia kupanda kwa bei ya umeme hata kwa wale ambao hawatumii umeme mwingi kutawaathiri kwani kunapandisha gharama ya vitu vingine vingi ambavyo kila mtu anatumia.

Wananchi ambao kipato chao kinategemea sana umeme kama vile biashara ya samaki, saluni, kuuza barafu, na vinywaji kama maziwa, juice na soda wataathirika kwa kiasi kikubwa kwa ongezeko hilo. Pamoja na watumiaji wa umeme kuwa wachache, kupanda kwa umeme kuna athari kwa watumiao na wale wasiyotumia, gharama za uzalishaji zitapanda juu, na walaji wote maskini na matajiri watahitajika kufidia wazalishaji.

Tumeambiwa watumiaji wa umeme wa majumbani wanaotumia zaidi ya uniti 50 watalipa shilingi 273. Kundi la wafanyabiashara wadogo wadogo bei imepanda kutoka Shilingi 157 hadi Sh 221 kwa uniti, watumiaji umeme kiwango cha kati, bei imepanda kutoka Sh 94 hadi Sh 132 kwa uniti. Watumiaji umeme mkubwa hasa wenye viwanda na migodi, bei imepanda kutoka Sh 84 hadi Sh 118 kwa uniti na malipo ya huduma kwa kundi hili ni shilingi 14,233 kwa mwezi . ZECO wamepandishiwa kwa asilimia 28.21 kutoka awali ambako, walikuwa wakilipa Sh 83 na sasa watalipa Sh 106 kwa uniti.

Kwa kipindi kirefu sasa Watanzania tumekumbana na hali ngumu ya maisha kutokana na kushuka kwa thamani ya shilingi ya Kitanzania dhidi ya dola ya Kimarekani. Kutokana na takwimu za Shirika la Taifa la Takwimu (National Bureau of Statistic Office ) zinaonesha kupanda kwa mfumko wa bei kwa asilimia 5.6 % (2010), asilimia 8.6 % (hadi Aprili 2011), asilimia 19.2% (Novemba 2011). Mfumko wa bei ulipanda hadi kufikia asilimia 19.8% (Desemba 2011). Hii imepelekea kuendelea kupanda kwa bei ya vyakula na bidhaa muhimu mfano sembe, mchele, maharage, sukari, mafuta ya taa, dizeli na petroli. Vile vile, taifa linapita katika kipindi kigumu kiuchumi kutokana na kukosekana kwa rasilimali muhimu na za msingi kwa jamii kama maji, miundombinu ya usafiri, mafuta, umeme na nyinginezo kwa kipindi kirefu

Pia takwimu za Shirika la Taifa la Takwimu (National Bureau of Statistics) za mwaka 2007, kuhusu utafiti katika kaya kuona idadi ya watu wanaotumia umeme ilikuwa : mwaka 1991/92 asilimia 9 %, mwaka 2000/1 asilimia 12%, hadi kufikia mwaka 2007 ilikuwa asilimia 13% ambayo ni sawa na watu millioni 5 (tano) tu kati ya watu millioni 39 waliotumia umeme. Matokeo haya yanaonesha Watanzania walio wengi hawatumii umeme, hata hivyo kundi hili wanapata athari kubwa kwani gharama za uzalishaji zitapanda juu sambamba na ununuzi wa bidhaa mbalimbali.

Tumeshuhudia katika Wilaya za Ilala, Kinondoni na Temeke jijini Dar es Salaam, ongezeko la bei za vyakula mfano, mfuko mmoja wa sukari wa kilo 25 unauzwa sh 80,000 kwa bei ya jumla kutoka sh 40,000 ikiwa imepanda mara dufu huku kilo moja ikiuzwa kati ya sh 2,000 hadi 2,500.

Katika masoko ya Tandika, Kariakoo na Tandale taarifa inaonyesha bei ya vyakula imepanda kwa kasi katika miezi mitatu iliyopita. Kwa sasa gunia moja la mchele linanunuliwa kati ya sh. 100,000 hadi 120,000 kutoka sh 80,000 hapo awali. Wakati kilo moja ya mchele kwa sasa ni kati ya sh. 2,000 hadi 2,500

TGNP tunahoji sababu za serikali kupandisha bei ya bidhaa muhimu kama umeme hali ikijua kabisa kuwa wananchi wengi, hasa wanawake na wanaume walioko pembezoni na wenye kipato cha chini wanazidi kunyonywa na walafi na mabepari wachache wa ndani na nje ya nchi na kupelekea wananchi masikini walio wengi kukosa maisha endelevu, kunyimwa uhuru na hata kushindwa kutumia na kufaidi rasilimali na utajiri wa nchi yao uliowazunguka, mfano madini, misitu na ardhi. Sisi kama wanaharakati na watetezi wa haki na usawa kwa wote tunapinga kabisa ongezeko la bei ya umeme, kwa sababu ongezeko hilo litaathiri sana maisha na kipato cha mwananchi masikini hasa wanawake walioko pembezoni

TGNP tunaidai serikali, kutekeleza yafuatayo ili kukabiliana na matatizo yaliyopo ikiwemo ongezeko la bei ya umeme:-

  • Kusimamia kwa makini tatizo la mfumko wa bei sambamba na ongezeko la bei ya umeme ili shughuli za uzalishaji ziendelee kwa nia ya kuwanusuru wananchi hasa kutokana na hali ngumu ya kiuchumi
  • Kuwaeleza wananchi, ni lini matatizo haya yatamalizika na mbinu mbadala za kumaliza matatizo haya na kwa kipindi gani. Pia kuwepo na mipango mikakati ya muda mfupi na mrefu kuhakikisha matatizo haya yanatatuliwa
  • Kuwawajibisha wataalamu na watendaji wa serikali wanaoshindwa kutimiza wajibu wao na kusababisha matatizo makubwa kama ya ukosefu wa umeme, maji na mfumko wa bei.
  • Kuchukua hatua za haraka za kufuatilia kwa karibu upatikanaji wa vyanzo mbadala vya umeme ikiwa ni pamoja na kuruhusu watu na makampuni binafsi kuzalisha nishati ya umeme, kama ilivyoruhusu kwa sekta zingine kumilikiwa na watu binafsi ili kuweza kuendelea kuzalisha umeme huo na kuchangia maendeleo mbalimbali ya kiuchumi nchini.
  • Serikali ihakikishe masuala ya ufisadi mfano Richmond, Dowans na mengineyo yamepatiwa ufumbuzi wa haraka na pesa zote zimerudi mikononi mwa serikali na kunufaisha Watanzania wote
  • Tunawasihi viongozi wawe na dhamira ya dhati ya kuwasaidia wananchi, na bila kuingiza siasa kwenye masuala ya maendeleo hasa yanayohusu maisha na uhai wa Watanzania walio masikini .

Imetolewa na:

Mary Nsemwa
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji

No comments: