Sunday, October 30, 2011

WANAWAKE WATAKIWA KUTUMIA NAFASI WANAZOPEWA NA UNIFEM

Na Anna Nkinda- Perth Australia
30/10/2011 Wanawake wametakiwa kutumia nafasi zinazotolewa na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Wanawake (UNIFEM) katika kujiletea maendeleo yao na ya mataifa yao kwani lengo kuu la kuanzishwa kwa shirika hilo ni kumuinua mwanamke na kuleta usawa wa kijinsia.

Hayo yamesemwa jana na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika hilo Dk. Noeleen Heyzer wakati akiongea na wake wa wakuu wa nchi wanachama wa Jumuia ya Madola katika mkutano wao uliofanyika Perth nchini Australia.

Dk. Heyzer alisema kuwa hivi sasa katika nchi nyingi Duniani wanawake wanapewa nafasi za kupata elimu, kuwezeshwa kiuchumi, usawa wa kijinsia , kupata afya bora kwa mama na mtoto na upatikanaji wa ajira hii yote ni kumfanya mwanamke aweze kujiinua kiuchumi kwani hapo zamani wanawake walikuwa wameachwa nyuma kimaendeleo tofauti na wanaume.

“UNIFEM inashughulika na masuala ya usawa wa jinsia na uwezeshaji wa wanawake kiuchumi, kisiasa na kijamii hivyo basi ni jukumu lenu kuwahamasisha wanawake katika nchi mnazotoka ili waweze kuzitumia nafasi wanazopewa hii itawasaidia kujikwamua kiuchumi”, alisema

Baada ya Mkurugenzi Mtendaji wa UNIFEM kumaliza kuongea na wake hao wa wakuu wan chi akiwemo Mke wa Rais Mama Salma Kikwete walitembelea Halmashauri ya jiji la Perth upande wa Sekta ya Nishati na Madini na kuelezwa jinsi sekta hiyo ilivyochangia kutoa ajira na kuinua uchumi wa nchi hiyo.

Viongozi kutoka makampuni ya uchimbaji wa madini ambao ni Mtendaji Mkuu wa Chamber of Minerals and Energy of West Australia Reg Howard-Smith, Mkurugenzi Mtendaji wa Argyle Diamonds Kevin McLeish na Josephine Archer ambaye ni meneja biashara kutoka Argyle Pink Diamonds walisema kuwa kutokana na jiografia nzuri mji huo umejaliwa kuwa na madini mengi ukilinganisha na miji mingine.

“Upande wa Magharibi wa Nchi yetu kuna miji minne ambayo ni Kimberley, Pilbara, Yilgarn na Kusini Magharibi ambako kunapatikana madini zaidi ya aina 50 baadhi yakiwa ni dhahabu, almasi, chuma, mchanga mzito wenye madini aina tofauti, base metals, chumvi, chuma cha pua, Ilmenite, Rutile, Alumina, Zircon, Garnet na Tantaluma”, walisema.

Wake wa wakuu wan chi wanachama wa Jumuia ya madola waliweza kujionea aina mbalimbali za madini yanayopatikana katika nchi hiyo pamoja na vito vya thamani na bidhaa zinazotengenezwa kutokana na madini hayo.
Aidha waliweza kutembelea bustani ya kutunza mimea na wanyama wa asili nakuona jinsi viumbe hai vya kale vinavyotunzwa ili visiweze kupotea kwa ajili ya kumbukumbu ya vizazi vijavyo na wageni wanaotembelea nchi hiyo.

Mkutano wa wakuu wa Nchi wanachama ya Jumuia ya madola umemalizika leo na Kaulimbiu ya mwaka 2011 ya Jumuia hiyo ni “Wanawake ni wakala wa mabadiliko”.

No comments: