Tuesday, October 25, 2011

Wanasiasa, matajiri wakwepa deni Posta

MWENYEKITI wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC), Kabwe Zitto, amesema baadhi ya wanasiasa wanakopa na kutumia nyadhifa zao kushawishi wafutiwe madeni yao, ilhali wana uwezo wa kuyalipa.

Zitto alisema hayo jana wakati Kamati hiyo ilipokutana na watendaji wa Benki ya Posta (TPB) Dar es Salaam, walioelezea mpango wa benki hiyo wa kufuta deni la Sh bilioni 1.1 kwa wateja inaowadai.

Mbali na wanasiasa, Zitto alisema mchezo huo pia umekuwa ukifanywa na matajiri na watumishi wenye vyeo vya juu katika mashirika na taasisi mbalimbali nchini.

Kutokana na hali hiyo, Kamati hiyo ilimwagiza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), apitie upya deni hilo ili kujiridhisha, endapo linastahili kufutwa.

Pia Kamati hiyo iliiagiza benki hiyo kutoa orodha yote ya majina ya wadaiwa waliokopa kuanzia Sh milioni 50 na kuendelea, waliowekwa katika mpango wa kufutiwa deni hilo kwa mwaka 2009/10, ili iyapitie na kufanya uamuzi, iwapo walio orodheshwa wanastahili kutodaiwa tena au kuwaanzishia deni upya.

“Kamati inaagiza iletewe orodha ya majina yote ya wadaiwa walioainishwa kuwa wafutiwe madeni ya jumla ya Sh bilioni 1.1 ili iyapitie na kuyachambua kuona kama kuna anayeweza kudaiwa upya, ili hilo lifanyike.

“Hatuwezi kukubali kirahisi tu kwamba wadaiwa hao wafutiwe madeni kwa sababu kufanya hivyo ni kuiathiri benki na kumnufaisha mdaiwa anayejineemesha kwa njia ya ubadhirifu.

“Tuna uzoefu na mambo haya kutokana na tuliyoyaona kipindi cha nyuma. Madudu ni mengi kwenye mashitaka ya umma, wanasiasa na wenye nyadhifa wanatumia mashirika ya umma kujineemesha kwa sababu ya ubinafsi,” alisema Zitto.

Alisema, Bunge kupitia Kamati hiyo ndilo lenye uamuzi wa mwisho wa ama kufutwa kwa madeni au la, na kwamba wadaiwa watakaothibitika kuwa na uwezo wa kulipa madeni yao watadaiwa, hata kama ni kwa kutumia madalali.

Aliiagiza benki hiyo iipe Kamati orodha hiyo wakati itakapokutana nayo tena kupitia hesabu zake za kuishia Desemba.

Zitto pia aliitaka TPB iwasilishe kwa Kamati hesabu za deni la Sh milioni 375 inaloidai Western Union kwa kipindi hicho cha 2009/10 ili ijiridhishe pia kama linastahili kufutwa au la.

Fedha hizo ni malipo ya matumizi ya huduma mbalimbali za benki hiyo. Uamuzi huo ulitolewa baada ya Mtendaji Mkuu wa TPB, Sabasaba Moshingi, kuiambia Kamati hiyo kuwa deni hilo lilionekana kwa makosa baada ya maandalizi ya hesabu za fedha zilizopokewa na benki hiyo na zinazodaiwa kutoainishwa sawasawa.

“Tumeweka deni hilo katika orodha ya yanayostahili kufutwa kwa sababu limetokana na makosa yetu wenyewe katika kuoanisha fedha tulizolipwa na Western Union na tunazodai, deni hilo lililipwa, hivyo halikustahili kuonekana katika hesabu zetu,” alisema Moshingi.

Katika hatua nyingine, POAC imemwita Waziri wa Maliasili na Utalii, Ezekiel Maige, na wajumbe wa Bodi ya Utalii nchini (TTB) wafike mbele ya Kamati hiyo Oktoba 31, kuieleza ni kwa nini haijateua Bodi ya Wakurugenzi wake hadi sasa. Bodi ya awali ilimaliza muda wake wa kazi tangu mwaka 2009, ikiwa ni zaidi ya miaka miwili.

Zitto alimtaka Mkurugenzi Mkuu wa TTB, Dk. Aloyce Nzuki, aeleze ni nani aliyekuwa akiidhinishia fedha za matumizi ya kila siku ya Bodi hiyo ambayo ni zaidi ya Sh bilioni saba, wakati wenye uwezo huo kisheria ni Bodi ya Wakurugenzi ambayo haipo.

Pia alihoji ni vipi matumizi hayo yalikuwa yakiangaliwa kutokana na ukweli kwamba hakuna mwenye uwezo wa kumhoji mwingine, kati ya Menejimenti na TTB, juu ya matumizi ya fedha hizo, jambo ambalo Kamati iliona kama linatoa mwanya wa matumizi yasiyostahili.

kijibu, Dk. Nzuki alisema wamekuwa wakiomba kibali cha kutumia fedha hizo kutoka wizarani na kati ya hizo, Sh bilioni nne zinatoka serikalini, huku Sh bilioni tatu zikiwa ni makusanyo kutoka kwa wakala mbalimbali wakiwamo Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA).

Kamati ilimwagiza Msajili wa Hazina asiidhinishie TTB fedha nyingine hadi hapo majibu ya kuridhisha yatakapotolewa na Waziri kuhusu Bodi ya Wakurugenzi au atakapoiunda.

No comments: