Thursday, October 27, 2011

Ongezeko la watu Duniani ni zaidi ya bilioni 7

Bi. Christine Mwanukuzi kutoka UNFPA akiwasilisha mada

Martha Samwel akichangia mjadala

Ongezeko la watu linakadiriwa kufikia bilioni 7. Hayo yalisemwa jana na mtoa mada wa shirika la kimataifa la watu Duniani (UNFPA) Bi. Christine Mwanukuzi kuhusu ongezeko la watu Duniani katika semina za Jinsia na Maendeleo (GDSS) zinazofanyika kila siku ya jumatano katika ofisi za Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP).

Akizungumzia ongezeko hilo Bi. Christine Mwanukuzi amesema Tanzania kuna idadi ya watu milioni 44.4 na ongezeko hili la idadi ya watu haiendi sambamba na mgawanyo wa rasilimali uliopo, ni wachache wanaofaidi na kuna tofauti kubwa kati ya walionacho na wasionacho, vifo vya wakinamama wakati wa kujifungua na watoto chini ya miaka 5 kuzidi kuongezeka.

Bi. Christine aliweka bayana matokeo ya utafiti wa UNFPA unaoonyesha kuwa idadi ya watu ni milioni 3.7, watu bilioni 1 hulala njaa kila siku, watu bilioni 2 katika bilioni 7 wanaishi chini ya kipato cha dola 1 ya kimarekani kwa siku, inakadiriwa watu 7,000 hufa kila mwaka kutokana na matatizo haya na vifo 578 ikiwa ni vya wakinamama wakati wa kujifungua nchini Tanzania

Akichangia mjadala huo wa wazi Bi Martha Samwel ambaye ni mshiriki wa semina hizo alisema kulingana na maazimio ya sera ya Maputo, ifikapo mwaka 2015 bajeti ya kila nchi inatakiwa iwe imewekeza asilimia 15 katika sekta ya afya, mpaka sasa katika nchi ya Tanzania hatujafikia hata asilimia 10 na ongezeko la vifo vya wanawake wakati wa kujifungua ni kubwa, je tukifika bilioni 7 huduma za afya zitakuwaje? Vifo vya wanawake wajawazito vitakuwa kwa wingi kiasi gani? Serikali iliangalie hili kwa umakini ili kuwekeza katika rasilimali watu

Wengi wa waliochangia mjadala huo hawakuridhishwa na jinsi serikali inavyolipa umuhimu suala zima la afya ya uzazi na sekta nzima ya afya na kuitaka serikali kuchukua jukumu lake la kutoa huduma za msingi kwa jamii ambayo ni walipa kodi.

Semina za jinsia na maendeleo ni za wazi kwa yeyote na hufanyika kila siku ya jumatano saa tisa kamili alasiri mpaka saa kumi na moja jioni katika viwanja vya Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) na kushirikisha wadau wote katika kada mbalimbali.

No comments: