Thursday, October 20, 2011

Wananchi watakiwa kusimamia kesi za ukatili zifike mahakamani

Na Ananilea Nkya Mkurugenzi Mtendaji TAMWA.

WANANCHI wa Mkoa wa Kusini Unguja wameshauriwa kusimamia kesi zao zinazohusu ukatili wa kijinsia kuhakikisha zinafikishwa katika vyombo vya sheria. Mkuu wa upelelezi na makosa ya jinai, mkoa wa Kusini Unguja SSP Makaran Khamis Ahmed amesema kesi nyingi za ukatili hazifikishwi Mahakamani kutokana na wananchi kuanzisha tabia ya kuhukumu kesi katika ngazi za shehia, kijiji na familia pamoja na kukubali kuzifuta katika vituo vya polisi.

Makarani alitoa ushauri huo ofisini kwake Mwera alipokutana na wanaharakati kutoka ofisi ya Mkurugenzi wa mashtaka ya jinai (DPP) na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Zanzibar kufuatia wimbi la ongezeko la kesi za ukatili ambazo hazifikishwi mahakamani.

Alisema kuna matatizo katika vituo vya polisi katika mpango mzima wa kushughulikia kesi za udhalilishaji wa kijinsia lakini jamii pia ina tatizo kubwa la kuchelewa kufikisha kesi katika vituo vya polisi kutokana na kuzifanyia maamuzi katika ngazi zisizo rasmi.

“Tatizo hili la jamii wakati mwengine pia huchangia kuharibika kwa uchunguzi, kwa hivyo ni vizuri kuripoti kwa wakati muafaka na kuwabainisha askari wakorofi ambao wanazuia haki kuchukua mkondo wake”, alisema Ofisa huyo wa upelelezi mkoa wa Kusini Unguja.

Ofisa wa TAMWA anayeshughulikia mabadiliko ya jamii Zanzibar Asha Abdi alisema tangu mwaka 2009 hadi sasa zaidi ya kesi 10 zilifikishwa katika vituo mbalimbali vya polisi lakini ni kesi tatu tu ndizo zilizopelekwa mahakamani.

Alisema kutokana na hali hiyo waliamua kufuatilia kesi hizo kwenye ofisi ya Mwendesha mashtaka ambapo pia walielezwa kuwa hazikufikishwa huko na ndipo walipoamua kuzifuatilia kesi hizo katika polisi ya mkoa huo.

Kesi nyingi za ubakaji na watoto wenye umri chini ya miaka 18 kubebeshwa mimba zimetokea katika shehia za Mzuri, Kidimni, Michamvi, K/dimbani, K/mkwajuni, Unguja Ukuu, na Mtende.

No comments: