Wednesday, October 5, 2011

Wahariri kujadili kutokomeza ukatili wa jinsia

WAHARIRI 50 leo watakutana jijini Dar es Salaam kujadili jinsi vyombo vya habari vinaweza kutoa mchango mkubwa zaidi kuchangia juhudi za taifa za kutokomeza vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake, wasichana na watoto.

Wahariri hao wanatarajiwa kuangalia ni mambo gani ambayo wao wenyewe na vyombo vyao vitaweza kufanya ili viongozi na wananchi mijini na vijijini wachukue hatua kuepusha vitendo vya ukatili wa kijinsia visitokee katika maeneo yao.

Kadhalika watajadili ni mikakati gani vyombo vya habari vinaweza kuweka ili kuibua matukio ya vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake, wasichana na watoto ili huduma stahili za kimatibabu, kisheria na ushauri zitolewa kwa waathika wa vitendo hivyo viovu.

Chama cha Wanahabari Wanawake (TAMWA) kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia masuala ya idadi ya watu (UNFPA) wameandaa mkutano huo wa wahariri, ikiwa ni sehemu ya mwendelezo wa kampeni ya kitaifa kuzuia vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa sababu vitendo hivyo vinarudisha nyuma maendeleo ya familia na taifa.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa Tamwa, Ananilea Nkya, wahariri hao watakaokutana katika ofisi za chama hicho, watapata fursa pia ya kupata taarifa kuhusu hali halisi ya vitendo vya ukatili wa kijinsia nchini na jitihada kadhaa zinazochukuliwa kukabili tatizo hilo.

Taarifa ya Nkya ilisema vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake, wasichana na watoto ni pamoja na vipigo, ubakaji, ukeketaji, kudhulumu wajane hazi za mirathi, ndoa na mimba za utotoni na kutelekeza watoto kunakoongeza watoto kuishi mitaani.

“Tunaamini kuwa vyombo vya habari vikitumika ipasavyo kufanya tatafiti, kutangaza na kufuatilia hatua kwa hatua kesi za matukio ya ukatili dhidi ya makundi haya wadau watachukua hatua stahiki kupunguza tatizo hilo,” alisema Nkya.

“Utafiti zinaonesha kuwa ukatili wa kijinsia ni matokeo ya kutokuwepo haki sawa katika jamii baina ya wanaume na wanawake na kwamba vitendo hivi vina madhara makubwa kwa afya na ustawi wa wanawake,” alieleza.

No comments: