Monday, October 3, 2011

Wanawake 20,000 wafunga uzazi

SHIRIKA linalotoa huduma za afya nchini (PSI), limesema limewezesha wanawake 20,000 kutumia njia ya muda mrefu ya uzazi wa mpango ijulikanayo kama lupu au kitanzi kati ya Januari hadi mwezi huu.

Mkurugenzi wa Programu ya Afya ya Uzazi wa PSI, Dk. Nguke Mwakatundu alisema hayo juzi Dar es Salaam katika maadhimisho ya miaka 50 ya Uhuru.

Alisema mpango huo wa uzazi unaingizwa katika kizazi cha mwanamke ambapo kinaweza kukaa kwa miaka 10 hadi 12 kikiwa katika hali salama na isiyomuathiri mtumiaji bila kupata ujauzito.

“Ni njia ambayo haina homoni ni ya muda mrefu ambayo inawekwa mara moja na uwezo wake wa kuzuia ujauzito ni kwa asilimia 99,” alisema Dk. Nguke.

Alisema PSI inawashauri wanawake ambao wana watoto wa kutosha, kutokutumia vidonge wala sindano ambavyo vina homoni zinazoweza kuwaletea mabadiliko mbalimbali katika afya zao.

Aidha, alisema Shirika hilo linasisitiza matumizi ya kitanzi kutokana na kuwa na gharama ndogo kwa wakati mmoja tofauti na gharama za mara kwa mara zinazotozwa kwa njia nyingine zinazotumiwa na wanawake.

Kwa mujibu wa Dk. Nguke, wanawake 0.6 ndio wanaotumia njia ya kitanzi na kwamba matumizi ya uzazi wa mpango wa kisasa ni kwa asilimia 27.

Alisema wanawake wengi wamekuwa wakitumia njia ya sindano kwa asilimia 11, vidonge kwa asilimia saba na wanaofunga vizazi ni asilimia nne.

Hata hivyo, Dk. Nguke alisema zipo taarifa ambazo siyo sahihi za matumizi ya njia hiyo ya uzazi wa mpango wakidai kuwa kuwa ina madhara kwa afya na kwamba inaweza kutoa ujauzito.

No comments: