TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), imemtangaza Dk. Dalaly Kafumu wa Chama Cha Mapinduzi
(CCM) kuwa Mbunge mteule wa Jimbo la Igunga mkoani Tabora baada ya kushinda Uchaguzi Mdogo uliofanyika juzi.
Dk. Kafumu alitangazwa mshindi jana alasiri na Msimamizi wa Uchaguzi wa jimbo hilo, Protas Magayane, baada ya kuibuka mshindi dhidi ya wagombea wenzake saba walioshiriki kinyang’anyiro hicho.
Akitangaza matokeo hayo, Magayane alisema Dk. Kafumu ameshinda baada ya kupata kura 26,484 na kufuatiwa na Joseph Kashindye wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo Chadema)
aliyepata kura 23,260.
Aliyeshika nafasi ya tatu ni mgombea wa Chama cha Wananchi (CUF), Leopold Mahona aliyepata kura 2,104; Chausta 182; SAU 83; DP 76; na UPDP kura 63.
Kati ya wapigakura 171,019 waliojiandikisha, ni watu 53,672 tu waliojitokeza kupiga kura huku kura 1,185 zikiharibika na hivyo kura 52,087 kuwa kura halali zilizotoa uamuzi huo.
Uchaguzi Mdogo wa Igunga ulifanyika juzi kujaza nafasi iliyoachwa na Rostam Aziz wa CCM ambaye alijiuzulu wadhifa huo Julai 14, mwaka huu baada ya kuchaguliwa mwaka 1994 katika Uchaguzi Mdogo kutokana na kifo cha mtangulizi wake, Charles Kabeho.
Akizungumzia ushindi huo, Dk. Kafumu alisema pamoja na kupewa maneno mabaya wakati wa kampeni na kutukanwa, atafanya kazi ya ubunge na wananchi wote bila kubagua vyama vyao kwa kuwa maendeleo hayana chama, ni ya Igunga.
Dk. Kafumu alisema hayo jana baada ya kutangazwa mshindi wa kiti hicho na kukabidhiwa cheti cha utambulisho kwa ajili ya kuapishwa katika Bunge lijalo.
Alisema kazi ya kwanza atakayoanza nayo ni kuhakikisha jimbo hilo ambalo ni kame linapata
maji na katika kampeni za CCM, kupitia Ilani ya Uchaguzi ya chama hicho, iliahidiwa kuwa maji
yatatolewa kutoka Ziwa Victoria ambayo kwa sasa yako Shinyanga; karibu na Igunga.
Nao viongozi wa CCM wametamba kwamba wananchi bado wana imani na chama hicho, baada
ya ushindi huo.
Wakizungumza baada ya Dk. Kafumu kutangazwa kushinda kiti hicho, Katibu Mkuu wa CCM, Wilson Mukama alisema chama hicho kilikuwa na mkakati mzuri wa kampeni ndio maana kimeibuka na ushindi.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana Taifa, Martin Shigella alisema Watanzania wanatakiwa kufanya siasa za ustaarabu, amani na upendo kwani siasa za kupiga watu na kumwagiana
tindikali, hazina nafasi sasa.
Shigella alisema Watanzania wanajua historia ya nchi, kwani wanajua tulipo na tunapokwenda,
kwa hiyo waelewa na uamuzi wa wananchi wa Wilaya ya Igunga ndio chaguo lao hilo.
“Vyama vilivyotoa ushindani, bali kufanya siasa zilizojaa upendo amani na mshikamano kwani kwa kufanya hivyo ni busara kuliko siasa za chuki bila sababu,” alisema.
Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF) Tanzania Bara, Julius Mtatiro alisema wamesikitishwa na matokeo hayo kwa madai ni fedha zilichagua mtu na kwamba uchaguzi ulijaa mamluki wa kisiasa.
Alisema kuna kazi kubwa ifanyike kuhakikisha demokrasia inafanyika kwa lengo la kuwasaidia
Watanzania ambao wanataka kupata kiongozi bora kwa kuwa atawasaidia wananchi.
Aidha, Katibu wa Chadema Mkoa wa Kilimanjaro, Basil Lema alisema wanayakubali matokeo,
lakini wanakusudia kuyapinga mahakamani akidai kuwa haki haikutendeka.
Naye mgombea wa CUF, Leopald Mahona alisema matokeo hayo yamemtisha na kudai kuwa wana Igunga hawakuchagua mtu wa kuwaletea maendeleo.
Mratibu wa Uchaguzi wa CCM, Lameck Nchemba, alisema Dk. Kafumu ana uwezo mkubwa kuliko wagombea wote waligombea jimbo hilo, kwani anayafahamu matatizo ya watu wa Igunga na kuwaondolea matatizo yao hasa maji.
Katika hatua nyingine, CCM imeshinda kata 17 kati ya 22 ambazo zilifanya uchaguzi mdogo wa udiwani katika mikoa mbalimbali nchini juzi.
Kwa mujibu wa Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, CCM imeshindwa katika Kata ya Stendi Kuu wilayani Serengeti mkoani Mara iliyochukuliwa na Chama cha Wananchi (CUF).
Nape alisema kata nyingine nne ilizoshindwa zote zimekwenda kwa Chadema ambazo ni
Masekelo (Shinyanga Mjini); Mkoma (Rorya); Nzovwe (Mbeya) na Endasak (Hanang, Manyara).
Alizitaja baadhi ya kata walizoshinda ni katika maeneo ya Dodoma Mjini, Kongwa, Iramba,
Nzega, Mwanza, Tarime, Rorya (kata mbili), Monduli, Lushoto na Mbeya.
No comments:
Post a Comment