JAMII ya Wahadzabe waishio katika Bonde la Yaeda chini, wilayani Mbulu mkoani Manyara, wamepatiwa hatimiliki ya kimila kwa ajili ya matumizi yao ya asili ikiwamo kurina asali, kuwinda na kuchimba mizizi.
Tukio hilo ni la kwanza na la kihistoria tangu Tanzania kupata Uhuru wake kutoka Uingereza miaka 50 iliyopita ambapo lilihusisha pia kukabidhiwa kwa hatimiliki 50 za kimila kwa wakazi wa vijiji vya Domanga na Mongo wa Mono vilivyopo ndani ya bonde hilo.
Mbali na jamii hiyo ya Wahadzabe makabila mbalimbali yanaishi ndani ya bonde hilo ambayo ni Wasukuma, Watatoga na Wairaq ambao kiasili ni wafugaji na wakulima.
Akikabidhi hati hizo mwishoni mwa wiki iliyopita Kamishna Msaidizi wa Ardhi, Kanda ya Kazkazini, Doroth Wanzala alisema kuwa upatikanaji wa hati hizo utawasaidia wakazi hao kuepukana na migogoro ya ardhi inayowakumba mara kwa mara.
Alisema kuwa hati hizo zitawasaidia pia kutambua mipaka yao ya ardhi, hivyo kupunguza tatizo la migogoro katika maeneo hayo na kurahisisha mipango ya matumizi bora ya ardhi.
Awali,akisoma risala mbele ya mgeni rasmi, kwa niaba ya Ofisa Mtendaji wa kijiji hicho, Endeko Endeko alisema kuwa mwaka 1998 vijiji vya Mongo wa Mono na Domanga vilianzisha mpango wa matumizi bora ya ardhi uliokamilika mwaka 2000.
Alisema kuwa baada ya mpango huo kukamilika, vijiji vyao vilitunga sheria ndogondogo za vijiji kwa lengo la kulinda mpango huo, shughuli ambazo zilifanywa na Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu kwa kushirikiana na Shirika la Ujamaa Community Resource Team(UCRT) kama mwezeshaji.
Hatahivyo, Endeko alisema kuwa zipo changamoto zinazowakabili katika vijiji vyao na kutaja uvamizi wa maeneo aliodai unafanywa na watu kutoka mikoa ya jirani ya Singida na Shinyanga.Mratibu wa UCRT, Edward Loure alisema kuwa upatikanaji wa hatimiliki hizo za kimila utawasaidia wakazi wa maeneo hayo kuondokana na tatizo sugu la migogoro ya ardhi linalowakabili kwa muda mrefu.Zoezi la kukabidhi hati hizo lilifadhiliwa na shirika hilo la UCRT lenye makao makuu yake mkoani Arusha.
No comments:
Post a Comment