Monday, October 10, 2011

Aonya mchakato wa Katiba kuachiwa wanasiasa

VYAMA vya siasa visiachiwe peke yao kufanya mchakato wa Katiba mpya kwani vimekuwa na mtazamo wa msingi wa Katiba mpya kuwa suala la uchaguzi tu na si rasilimali za Watanzania.

Hayo yalibainishwa juzi na Dk. Alexander Makulilo wakati wa mdahalo wa katiba mpya uliofanyika katika Chuo cha Kikuu cha Mtakatifu Augustine (SAUT), jijini Mwanza uliokuwa umeandaliwa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu.

Alisema vyama vya siasa vimekuwa vikitumia gharama kubwa kwenye uchaguzi ikiwemo kutumia helikopta badala ya kuelimisha wananchi kwa nini Katiba mpya inahitajika huku ya zamani ikiwa na viraka na wananchi kutokuifahamu.

Dk. Makulilo alisema kutokana na hali hiyo dhana ya ushirikishwaji wa wananchi kwenye mchakato mzima wa Katiba mpya, unatia wasiwasi.

Wakichangia katika mdahalo huo wa namna wanavyotaka Katiba mpya iwe, Wilhelmina Mdodo alisema Katiba mpya lazima izingatie rasilimali za Watanzania kwa kupatiwa asilimia kubwa ya mapato na sio yaishie kwa wawekezaji kama ilivyo sasa.

Alisema dhana ya viongozi kuwa wafanyabiashara imezalisha mafisadi na ili kuondokana na hali hiyo, lazima vitenganishwe kwani bila kufanya hivyo nchi itaendelea kukamuliwa na wachache na uchumi hautakua.

Kwa upande wake, Kumbukeni Kondo alisema uzalendo umekufa nchini kwa viongozi kujali maslahi yao na familia zao hivyo katiba mpya iingize suala la uzalendo ili kuleta maendeleo kwa wananchi wake na sio wachache.

Aidha, alisema elimu ya uraia itolewa kwa Watanzania ili waifahamu sambamba na kila kaya kupatiwa nakala ya Katiba na kwamba Katiba mpya ioneshe wazi aina ya mfumo ambao unafuatwa na nchi kama ni wa ujamaa na kujitegemea ama ubepari kama walivyo viongozi.

Baadhi ya washiriki katika mdahalo huo waliitaka Katiba mpya iweke bayana namna Serikali itakavyowahudumia wazee bila kujali walikuwa waajiriwa au la kwani hata wakulima hulima kodi.

Profesa Chris Maina Peter alisema sheria ya mwaka 1997 ya uwekezaji imetoa haki kwa mwekezaji bila wajibu hivyo kutowajibika ipasavyo kwa wananchi.

Aidha, alisema suala la Muungano lisiangaliwe kwa ushabiki, bali kwa nia ya kujenga na kuimarisha Watanzania.

No comments: