Tuesday, October 11, 2011

JK akerwa ugoigoi tatizo la umeme

RAIS Jakaya Kikwete amewataka watendaji wake kufanya uamuzi wa haraka bila kigugumizi kukabiliana na tatizo la umeme nchini.

Amesema wanapaswa kutambua kuwa nchi iko katika hali ya dharura kubwa ya upatikanaji wa nishati ya umeme, na hivyo wafanye uamuzi wa haraka, bila kigugumizi, kukabiliana na hali hiyo kwa manufaa ya wananchi.

“Tuko katika hali ya dharura na mimi sioni hisia za uharaka wa kuchukua uamuzi na hatua nyingine muhimu za kukabiliana na udharura wa upatikanaji wa umeme na nyenzo nyingi za kuzalisha umeme.

“Hatuwezi kuendeleza kuwa na kigugumizi katika kuchukua maamuzi ya kuitoa nchi katika changamoto kubwa hizi za upatikanaji wa nishati,” Rais Kikwete aliwaambia watendaji hao wa Serikali yake wanaohusiana na sekta ya nishati.

“Ubwana mkubwa wa kila mmoja wetu utatambuliwa kutokana na mafanikio ambayo kila mmoja wetu ataonesha katika kuchangia katika kukabiliana na hali hii ya upatikanaji wa nishati,” alisema Rais Kikwete katika kikao cha watendaji hao kilichofanyika Ikulu, Dar es Salaam jana.

Kwa mujibu wa Ikulu, Rais alikuwa anazungumza katika kikao alichokiitisha kuzungumzia ujenzi wa bomba la gesi kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam na upatikanaji wa gesi asilia nchini ili kuzalisha umeme.

Umeme umekuwa katika mgawo nchini tangu Novemba mwaka jana kutokana na ukame ulioathiri kina cha maji katika mabwawa yote ya kuzalisha umeme nchini.

Hali hiyo imeilazimisha nchi kuchukua hatua nyingine za kupatikana kwa umeme wa dharura mbali na hatua ambazo tayari Serikali ya Rais Kikwete ilikuwa imeanza kuchukua kuongeza kasi ya upatikanaji wa umeme kutokana na vyanzo vingine mbali na maji.

Miongoni mwa waliohudhuria kikao hicho cha kazi ni Waziri wa Fedha, Mustafa Mkulo; Waziri wa Sheria na Katiba Celina Kombani; Katibu Mkuu Kiongozi, Phillemon Luhanjo na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema.

Wengine ni maofisa kutoka Wizara ya Nishati na Madini, Benki Kuu ya Tanzania, Tume ya Mipango, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC).

Kikao hicho kimejadili, miongoni mwa mambo mengine, ujenzi wa bomba kubwa zaidi la kusafirisha gesi asilia kutoka mikoa ya Mtwara na Lindi kwenda Dar es Salaam linalokusudiwa kujengwa na Serikali kwa fedha nyingi ili kuongeza kasi ya upatikanaji gesi kwa ajili ya uzalishaji umeme na matumizi ya viwandani katika sehemu mbalimbali za nchi badala ya bomba la sasa ambalo ni dogo zaidi.

Shabaha na mipango ya Serikali ni kuhakikisha kuwa bomba hilo linakuwa limekamilika katika muda wa mwaka mmoja ujao tayari kuongeza uwezo wa Serikali kuwapatia wananchi umeme wa uhakika zaidi na kuongeza uzalishaji wa viwanda ambavyo vimeanza kutumia gesi kwa ajili ya uzalishaji badala ya mafuta.

Kikao hicho pia kimejadili upatikanaji wa gesi yenyewe na hatua zinazochukuliwa ili kuhakikisha inapatikana gesi zaidi ili kukidhi mahitaji yanayoongezeka kila siku katika uzalishaji wa umeme na mahitaji ya viwandani.

Katika mjadala wa upatikanaji wa gesi zaidi, kikao hicho kimeangalia jinsi gani Tanzania inavyoweza kuongeza uzalishaji wa gesi hiyo kwa kuchimba visima zaidi na kukarabati visima vilivyoko kwa sasa ili kuongeza upatikanaji wa gesi hiyo asilia.

Kikao hicho pia kimejulishwa juu ya hali ya umeme nchini na jitihada zinachukuliwa na vyombo na taasisi mbalimbali nchini na hasa Tanesco katika kuitoa nchi katika hali ya sasa ya mgawo wa umeme ambao umekuwa unaendelea kwa karibu mwaka mmoja.

Rais Kikwete aliwataka watendaji hao kuelekeza nguvu zao katika kutambua na kufanya kazi kwa karibu zaidi na wawekezaji ambao wamethibitisha kuwa makini zaidi katika uzalishaji umeme kwa sababu inawezekana kuwa Serikali isiwe na uwezo wa kutosha kuwekeza kiasi kikubwa cha fedha za kutosha katika uzalishaji umeme katika miaka mitano ijayo ili kwenda sambamba na mahitaji makubwa na yanayoongezeka ya umeme nchini.

Mapema kabla ya hapo, Rais Kikwete alikutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Ujerumani nchini, Klaus-Peter Brandes.

Katika mkutano huo, Rais Kikwete na Balozi Brandes wamezungumzia hali nzuri ya uhusiano kati ya Tanzania na Ujerumani.

Balozi wa Ujerumani alimshukuru Rais Kikwete na Serikali yake kwa kuandaa safari ya karibuni ya mabalozi wanaowakilisha nchi zao katika Tanzania kutembelea Kijiji cha Butiama ikiwa ni sehemu ya kumbukumbu ya kifo cha Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere miaka 12 iliyopita.

No comments: