Thursday, October 13, 2011

Kisa cha Julius Kambarage Nyerere, 1952 - 7

Harakati za TAA na baadaye TANU ziliendelea. Katika sehemu hii ya makala, mwandishi MOHAMED SAID ambaye amefanya utafiti wa mambo yalivyokuwa Tanganyika kabla na baada ya uhuru, anaendelea kusimulia harakati zilivyokuwa…

INASEMEKANA kwamba ilikuwa wakati huu Abdulwahid kwa mara ya pili alimshauri Nyerere kujiuzulu kufundisha ili ashughulike na kazi za TAA.

Wazo hili halikumvutia Nyerere kama vile ambavyo halikumvutia Chifu Kidaha Makwaia miaka minne iliyopita. Lakini Nyerere alipiga hatua moja mbele kuliko Chifu Kidaha. Angalau Nyerere alikuwa amekubali kuiongoza TAA.

Nyerere alikuwa anajua vyema wakati huo kwamba TAA ilikuwa ikiendeshwa kutoka mifuko ya wazalendo ambao idadi yao haikuzidi watu wanne. Ni dhahiri kuwa Nyerere hakutaka kuishi kwa kutegemea msaada hata ikiwa wafadhili wake walikuwa na nia njema.

Kilichosukuma ule uongozi wa ndani wa TAA kusisitiza juu ya Nyerere kujiuzulu kazi na kuchukua uongozi wa TAA ilikuwa kwanza, ule ukweli kuwa TAA ilikuwa ikifanya kazi kama chama cha siasa na Gavana alikuwa akifahamu hivyo.

Pili, mpango ulikuwa mbioni kusajili chama cha siasa kabla ya mwisho wa mwaka wa 1954.

Wakati huo huo TAA ilikuwa ikishughulikia rasimu ya katiba ya chama kipya na mipango ilikuwa ikiendelea kwa rais wa chama cha siasa kilichokuwa kikitarajiwa kusafiri kwenda Umoja wa Mataifa, New York kutoa madai ya Tanganyika mbele ya Baraza la Udhamini kama Japhet Kirilo alivyofanya miaka miwili iliyopita.

Vilevile ilikuwa muhimu uongozi wa TAA uwe na rais aliyekuwa anafanya kazi ya chama kwa muda wote wakati chama kipo mbioni kuundwa.

TAA ilikuwa inafungua ukurasa mpya, ikijiondoa kutoka zile siasa za baada ya vita, za mapambano; na kuelekea katika siasa za mazungumzo na mapatano. Kulikuwa hakuna wasiwasi wowote kuwa TAA ilikuwa na udhibiti kamili wa siasa nchini kote.

Katika miaka yote 25 ya kuweko kwa TAA hakuna chama chochote kilichozuka kuipinga. Kwa miaka mingi TAA ilidhihirisha uhalali wake wa kuwapo kama mwakilishi wa kweli wa Waafrika.

TAA ilikuwa na mpinzani mmoja tu wa kupigana naye, nayo ilikuwa ni serikali ya kikoloni ya Uingereza.
TAA iliunda itikadi na uongozi wake wenyewe kuwaunganisha watu wote kama chama cha Waafrika kilichoungwa mkono na umma dhidi ya utawala wa Kiingereza.

Sasa Tanganyika ilikuwa ikichemka pole pole kutokana na kampeni za TAA, manungíuniko ya wananchi yakitumika dhidi ya serikali.

Hili lilikuwa jambo jipya kwa serikali ya kikoloni. Kutokana na hali hii ya manungíuniko ya wananchi wa Tanganyika, Gavana Twining katika hotuba yake kwa Baraza la Kutunga Sheria mnamo Mei, 1954 aliwashambulia viongozi wa TAA kwa maneno haya, “Nimefahamishwa juu ya mambo yanafanywa katika baadhi ya sehemu humu nchini na watu wanaojitafutia makuu.

Hawa ni watu wakorofi, ambao baada ya kujiteua wao wenyewe kuwa viongozi wa siasa, wanajaribu kuwachochea watu dhidi ya tawala za kienyeji na wakati mwingine dhidi ya Serikali Kuu, kwa kutumia malalamiko ya sehemu hizo ya kweli au ya kubuni...

Jambo hili haliwezi kuruhusiwa kuendelea na serikali haitavumilia vitendo kama hivyo ambavyo viko kinyume na maslahi ya watu na vimekusudiwa kuiharibu ikiwa siyo kuiangamiza serikali. Heshima kwa serikali, ambayo ni tabia ya asili katika silika ya Waafrika lazima idumishwe…”

Hotuba hii ilijaa vitisho. Baada ya hotuba hii serikali ilichukua mfululizo wa hatua za ukandamizaji na vitisho dhidi ya viongozi wa TAA, ikitumia mbinu zote, zilizokuwa dhahiri na za siri. Wakati huu na hususan baada ya kuchapishwa kwa ile Sekula ya Serikali No.5 ndani ya Government Gazette mwaka wa 1953 na kufuatia kuvunjika kwa Pan African Congress ambao wajumbe kutoka Tanganyika walikuwa Ally Sykes na Denis Phombeah, walikamatwa Rhodesia na kurudishwa nchini.

Serikali ya kikoloni sasa iliimarisha Special Branch kwa kumwaga mitaani makachero na vibaraka. Ally Sykes tayari alikuwa akijulikana kwa msimamo wake wa kupinga ukoloni na Abdulwahid kwa uongozi wake katika TAA waliandamwa na hawakuwa na pa kujificha, walifuatwa fuatwa na makachero kokote walikokwenda.

Makachero walikuwa na kazi kutafuta habari mjini na baadhi yao waliwekwa nje ya ofisi ya Abdulwahid pale katika soko la Kariakoo.

Katika kipindi hiki Abdulwahid alianza kutumia hati mkato katika kumbukumbu zake za mikutano ya TAA na katika kuandika shajara (diary) yake mwenyewe. (Hizi shajara ziko hadi leo na zimehifadhiwa).

Joto la siasa lilikuwa katika kiwango kama hiki wakati wajumbe kumi na saba wa TAA kutoka kwenye matawi majimboni na makao makuu walipokutana mjini Dar es Salaam tarehe 7 Julai, 1954, kujadili katiba mpya ya chama kipya cha siasa - TANU.

Jimbo la Mashariki ambalo lilikuwa na wajumbe wengi kushinda yote liliwakilishwa na, ndugu wawili Abulwahid na Ally Sykes, Dossa Aziz, Tewa Said Tewa, Patrick Kunambi, Kasella Bantu, John Rupia, Julius Nyerere na C. O.Milinga; Jimbo la Kaskazini liliwakilishwa na na Joseph Kimalando na Japhet Kirilo; Jimbo la Ziwa liliwakilishwa na Abubakar Kilanga, L. M. Makaranga.

Katika wanachama kumi na saba waasisi, tisa kati yao walitoka makao makuu, watano kutoka Jimbo la Ziwa, mmoja kutoka Jimbo la Magharibi na wawili kutoka Jimbo la Kaskazini.

Uwakilishi huu wa wajumbe kutoka kwenye majimbo na makao makuu unatoa picha ya hali ya harakati za siasa nchini Tanganyika kabla ya kuundwa kwa TANU.

Mkutano Mkuu wa Mwaka wa TAA ulikuwa na ajenda ndefu. Siku ya kwanza mkutano ulichukua masaa matano na nusu. Siku hiyo ilitumiwa kuondoa matatizo yaliyokuwa yakikiathiri chama.

Ajenda ya kwanza ya mkutano huo ilikuwa idhinisha kufukuzwa kazi kwa Alexander Tobias aliyekuwa katibu mtendaji tangu Juni, 1953. Tobias alikuwa amepoteza majalada na nyaraka muhimu sana za chama zilizokuwa chini ya mamlaka yake kama katibu mtendaji. Kulikuwa na tetesi kwamba majalada hayo aliyakabidhi kwa Special Branch baada ya kupewa fedha.

Ilikuwa katika siku ya pili ndipo wajumbe walikaa chini kuanza kazi hasa ya kujadili ya kuigeuza TAA na kukifanya chama cha siasa TANU bila ya kuficha madhumuni yake na kutangaza dhamiri ya chama ya kuwatayarisha Waafrika wa Tanganyika kujitawala. Julius Kambarage Nyerere, mwanasiasa mgeni katika TAA pale makao makuu akiwa amejiunga na uongozi wa chama miezi 15 tu iliyopita, alichaguliwa Rais wa kwanza wa TANU na John Rupia Makamo wa Rais.

No comments: