Thursday, October 6, 2011

JK aagiza watumishi mafisadi wachunguzwe

RAIS Jakaya Kikwete ameipa jukumu Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kuwachunguza watumishi wa umma ambao sio viongozi wanaotajwa kwa kujilimbikizia mali wakitumia vyeo vyao na ofisi walizokabidhiwa kuwahudumia wananchi.

Mbali na jukumu hilo, pia ameipa jukumu Sekretarieti ya Maadili kukamilisha mchakato utakaowezesha kutungwa kwa sheria itakayotenganisha biashara na uongozi ili itatumike kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.

“Napenda sana hili la sheria ya kutenganisha uongozi na biashara ianze kutumika katika Uchaguzi Mkuu wa 2015…tuwe kama wenzetu wa nchi ya Marekani ambao wameweza kutenganisha mambo haya ya uongozi na biashara,” alisema Rais Kikwete.

Rais Kikwete alisema hayo wakati akifunga mafunzo ya uchunguzi wa maofisa sheria wa Sekretarieti ya Maadili wa Viongozi wa Umma yaliyofanyika katika Chuo cha Maofisa wa Polisi Kidatu mkoani Morogoro.

Alisema haitoshi kwa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kuwachunguza viongozi namna walivyopata mali zao wakati kuna wa watumishi wengi wametajwa kumiliki mali nyingi ambazo hazijapatikana kihalali.

“Sheria ya sasa inawachunguza viongozi pekee, lakini pia tunataka na watumishi wa umma ambao sio viongozi waanze kumulikwa kwa kuwa wengi wanamiliki mali nyingi tofauti na vipato vyao halali,” alisema Kikwete.

Alisema ili kupata ukweli usio na shaka kuhusu umiliki wa mali za watumishi na viongozi, kuna haja hivi sasa kwa Sekretarieti hiyo kushirikisha vyombo vya ulinzi na usalama pamoja wananchi ili wathibitishe mali walizozitaja katika fomu za tamko la rasilimali, maslahi na madeni.

Alisema lengo la kuchukua hatua hiyo ni kufanya kuwepo kwa watumishi wenye maadili na uadilifu na sio wanaotumia ubabe, vitisho na wale wanaopenda rushwa na hivyo kupelekea nchi kukosa maendeleo.

Akizungumzia kuhusu sheria ya kutenganisha biashara na uongozi ambayo ilitakiwa itumike katika Uchaguzi Mkuu uliopita, alisema jambo hilo lilishindikana kutokana na kuingiliana na Sheria ya Gharama za Uchaguzi.

Alisema kwa sasa Sekretarieti hiyo kwa kushirikiana na vyombo vingine, kuwa na muda mzuri wa kuandaa sheria hiyo ya kutenganisha masuala ya biashara na siasa ili sasa itumike kikamilifu katika Uchaguzi Mkuu ujao.

“Kuna watu wanataka kutumia nafasi ya uongozi kulinda maslahi yao, sasa sheria hiyo itakapokamilika itatenganisha biashara na uongozi ili mtu achukue uamuzi wa kuchagua aende wapi,” alisema Rais Kikwete.

Aidha, Rais Kikwete alitolewa mfano kuwepo kwa baadhi ya wafanyabiashara walioingia katika siasa kwa kutafuta hadhi, hali ambayo inalenga kutetea maslahi wakati wa kutoa maamuzi ya msingi katika masuala ya maendeleo.

“Wewe ni kiongozi ambaye unapaswa kutoa uamuzi sahihi na pia mfanyabiashara unapeleka tenda katika Halmashauri na kuwataka waipitie tenda yako, sasa lazima tutenganishe ili mtu abaki sehemu moja,” alisema.

Awali, Kamishna wa Maadili Jaji Mstaafu Salome Kaganda, alisema Sekretarieti ya Maadili imeanza kupata mafanikio baada ya idadi ya viongozi wa umma wanaorejesha fomu kuongezeka kutoka viongozi 6,007 sawa na asilimia 76.8 katika mwaka jana hadi viongozi 8,465 ambayo sawa na asilimia 94 mwaka huu.

Kamishna huyo alisema tangu mwaka 2006 hadi sasa, matamko 1,241 wa viongozi wa umma yamehakikiwa kati ya viongozi 9,016 sawa na asilimia 13.76.

Hata hivyo, katika mwaka 2010/11, jumla ya malalamiko 219 ya ukiukwaji wa maadili dhidi ya viongozi wa Umma yalipokelewa na kuchambuliwa ili kubaini kama yanakidhi matakwa ya sheria ya maadili ya viongozi hao.

Kamishna huyo alisema kati ya malalamiko hayo, 100 yalihusu ukiukwaji wa maadili kwa mujibu wa sheria wakati malalamiko yanayohusu sheria namba 19 yalichunguzwa na kumalizika ambapo mengine yalikwama kutokana na ufinyu wa bajeti.

Alisema uundwaji wa Baraza la Maadili umesaidia kupokea malalamiko 41 dhidi ya ukiukwaji wa maadili kwa viongozi ambapo tayari 24 walipatikana na hatia na kupewa onyo na wengine onyo kali.

No comments: