Mvutano mkubwa uliibuka jana kati ya mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano kupitia Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willibrod Slaa, na Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Kyela (OCD), aliyetambulika kwa jina moja la Male, baada ya kutoa taarifa ya kukataa kuilinda helikopta inayotumiwa na mgombea huyo.
Mvutano huo ulianza saa 11:00 jioni jana baada ya Dk. Slaa kuwasili katika uwanja wa Mwakangale mjini Kyela kuhutubia mkutano wa kampeni.
Mkutano huo ulikuwa ni wa mwisho baada ya kuhutubia mikutano mitano ya kampeni katika maeneo kadhaa mkoani Mbeya katika wilaya za Mbarali na Kyela. Mgombea huyo alipangiwa kulala Kyela.
Baada ya kuhitimisha mkutano wa Kyela, Dk. Slaa aliwaeleza wananchi kwamba helikopta hiyo ingelala uwanjani hapo, lakini baadaye akawaambia kuwa alipata taarifa kutoka kwa OCD kwamba polisi hawatailinda kwa maelezo kuwa helikopta hiyo si mali ya serikali bali mali ya mtu binafsi.
Taarifa hiyo ilimfanya Dk. Slaa aje juu na kutoa sauti kali kwamba anataka apewe taarifa hiyo kwa maandishi ili aipeleke kwa Inspekta jenerali wa Jeshi la Polisi (IGP), Said Mwema.
Pamoja na Dk. Slaa kutaka ampe taarifa kwa maandishi, OCD huyo alimwonyesha saa akimtaka ateremke jukwaani kwa kuwa muda wa mkutano ulikuwa umekwisha hivyo ashuke akamshitaki kwa kujiongezea muda wa kampeni. Wakati huo ilikuwa saa 12:10 jioni.
Hali hiyo ilimlazimisha mchumba wa Dk. Slaa, Josephin Mushumbusi na wafuasi wengine wa Chadema waliokuwa wamepandwa na jazba kumfuata OCD, ambaye baada ya kuona hivyo, alianza kuondoka uwanjani hapo.
Kufuatia hali hiyo, Dk. Slaa alimuita jukwaani askari anayemlinda na kuwatangazia wananchi kuwa alipewa askari huyo na IGP amlinde wakati wa kampeni.
“OCD anasema hatalinda ndege yetu wakati mshahara anaolipwa unatokana na kodi zetu,” alisema huku watu wakiitikia kwa kuonyesha kukerwa na kitendo hicho.
Ilimlazimu askari anayemlinda Dk. Slaa kumfuata OCD huyo na kuondoka naye wakiteta kwa faragha.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Advocate Nyombi, akizungumza kwa simu na NIPASHE kama anahusiana na tukio hilo, alisema kitendo cha OCD ni chake binafsi na hakiwakilishi Jeshi la Polisi.
Nyombi alisema wao wana maelekezo ya namna ya kutoa ulinzi kwa wagombea wote wa urais na kuahidi kuwa itaendelea kulindwa.
Katika hatua nyingine, Dk. Slaa amesema akiingia madarakani atakagua Sh. bilioni 21, maarufu kama “Mabilioni ya JK” zilitolewa na serikali kwa wajasiliamali kila mkoa, ili kujiridhisha kama ziliwanufaisha walengwa (wananchi) au la.
Amesema atafanya hivyo kwa vile fedha hizo ni mali ya umma na kwamba, kuna taarifa zinazodai kuwa zimewanufaisha watu wachache.
Dk. Slaa alitoa ahadi hiyo wakati akihutubia mkutano wa kampeni za kuusaka urais wa Jamhuri ya Muungano, mjini Songea juzi jioni.
“Rasilimali zinagawiwa ovyo tu bila mpangilio. Hizi fedha ni za umma, lakini hakuna anayejua nani kanufaika nazo. Nitazishughulikia na kuhakikisha zinarudishwa katika matumizi ya umma,” alisema Dk. Slaa na kushangiliwa na umati watu waliofurika katika mkutano huo.
Aliitaka serikali kutaja makampuni yaliyofaidika na Sh. trilioni 1.3 zilizotolewa na serikali kwa ajili ya kuokoa makampuni dhidi ya mtikisiko wa kiuchumi duniani.
No comments:
Post a Comment