Wednesday, October 27, 2010

‘Kubalini matokeo, msiporidhika fuateni sheria'

SERIKALI kupitia vikosi vya ulinzi na usalama, imetoa tahadhari kwa waliojipanga kuyakataa matokeo ya uchaguzi, wajiepushe na uvunjifu wa amani na kama hawatoridhika na matokeo hayo, wadai haki yao kwa kufuata sheria na kanuni zilizopo.

Aidha, ili kuwahakikishia amani na utulivu Watanzania katika siku chache zilizobakia za kampeni na baada ya kutangazwa matokeo ya uchaguzi, Jeshi la Polisi limetangaza kushirikiana na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Jeshi la Magereza na Mgambo.

Uthibitisho huo wa utulivu na amani wakati wa uchaguzi, umetolewa jana kwa nyakati tofauti na Waziri wa Mambo ya Ndani, Lawrence Masha, Mkuu wa Jeshi la Polisi, Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP) Said Mwema na viongozi wengine wa serikali.

“Endapo matokeo yaliyotangazwa hayatokidhi matarajio ya mtu au kikundi chochote, ni vyema utaratibu wa kisheria ukafuatwa pasipo uvunjifu wa sheria,” alisema Mwema.

Alisema, ingawa wajibu wa usalama na amani pia ni wa wananchi, Polisi imejipanga kuhakikisha mikutano ya kampeni iliyobakia inamalizika kwa usalama, utaratibu wa kupiga kura unafanyika kwa amani na utulivu na vifaa vya kupigia kura vinalindwa ili visiibiwe, visitekwe wala kughushiwa.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Mbarak Abdulwakil, alisema mchakato wa uchaguzi umekuwa shwari isipokuwa kuna matukio kadhaa yaliyotia dosari.

Aliyataja matukio hayo kuwa ni kuchana mabango ya wagombea, lugha chafu na wanachama wa vyama tofauti kushambuliana na kutoa taarifa za uvumi kwa njia ya simu na mtandao.
Masha ambaye alitoa taarifa yake mkoani Mwanza alisema: Wananchi wote wa Tanzania watapiga kura kwa amani na utulivu Oktoba 31 na wale watakaoleta vurugu, neno langu ni moja kwao ya kuwa wawe tayari kuvuna walichokipanda.”

Alisema, Serikali inawashukuru Watanzania kwa kuonesha ukomavu wa kisiasa katika kampeni na kuhakikisha hakuna mtu aliyepoteza maisha hadi wakati huu.

“Lakini kule Shinyanga mwanachama mmoja wa CCM kwa sababu tu alikutwa ameweka bango la CCM tayari ameuawa hivi tunaelekea wap?”

Alihoji na kuvitaka vyama vya siasa viongozi wao na wananchi kwa ujumla kuheshimu taratibu za uchaguzi.

Alisema serikali haimzuii mtu yeyote kufanya ushabiki ndani ya chama anachokipenda, lakini akasisitiza kuwa ushabiki huo sharti uzingatie sheria na utaratibu.

1 comment:

Anonymous said...

TUKUBALI MATOKEO HATA KAMA TUKIAMBIWA 1+1=1? HAPANA NA HAIINGII AKILINI, LAZIMA HESABU ZITOE MAJIBU SAHIHI NA SIYO MAJIBU YA UCHAKACHUAJI. KAMA CCM ILIWEZA KUCHAKACHUA MAJIBU NDANI YA CHAMA KWANINI ISIWEZE KUCHAKACHUA MAJIBU KULIKONONA ZAIDI? KWANINI JESHI LA WANANCHI LIINGILIE KATI WAKATI HAKUNA VITISHO VYOVYOTE TOKA KWA WAPINZANI ZAIDI YA KUMZIDI JK KATIKA UMAHILI WA KUJIELEZA KWA WANANCHI? WAKATI WAPINZANI WAKIJIELEZA KWA WANANCHI JK AMEKUWA AKITOA AHADI MPYA KILA ANAPOKWENDA! HUYU ALITAKIWA ATUELEZE WANANCHI AMETUFIKISHA WAPI KIUCHUMI NA SASA ANAMATARAJIO YA KUTUENDELEZA MPAKA WAPI.